Na Mwandishi Wetu.Mwaka 2004 utaendelea kubaki katika kumbukumbu za nchi yetu kama mwaka wa mageuzi katika sekta ya nishati ambapo kwa mara ya kwanza Tanzania ilianza kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia. Miaka kumi na nne baadae, Tanzania imeendelea kuwa kinara katika nchi za Afrika Mashariki ambazo zinatumia gesi asilia kuzalisha umeme ambapo hadi sasa zaidi ya asilimia 50% ya umeme unaozalishwa nchini unatokana na nishati ya gesi asilia. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mitambo ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi II, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. John Pombe Joseph Magufuli alisema “nishati ya umeme ni injini na muhimili muhimu katika ukuzaji uchumi na ustawi wa maisha ya binadamu, umeme unachochea shughuli za uzalishaji na hivyo kutoa fursa za ajira na kuboresha maisha ya watu”. Mh. Rais pia aliongeza “Azma na dhamira yetu ya kujenga uchumi wa viwanda haiwezi kutimia bila ya kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika”. Mitambo ya kufua umeme ya Kiyerezi II ina uwezo wa kuzalisha megawati 240 za umeme na inategemea gesi asilia inayozalishwa na kusambazwa na TPDC kupitia kampuni tanzu ya Gasco inayosimamia shughuli za ukusanyaji na usambazaji wa gesi asilia nchini. 

Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani alieleza mipango ya Wizara ya Nishati katika kufikia Tanzania ya viwanda kwa kutumia gesi asilia kuzalisha umeme wa uhakika. Dk. Kalemani alisema “ufunguzi wa Kinyerezi II ni muendelezo wa miradi ya umeme wa gesi asilia, baada ya mradi wa leo tunategemea kutekeleza miradi mingine miwili hapa Kinyerezi ambayo yote itatumia gesi asilia na kuzalisha megawati 600, isitoshe tunatarajia kuzalisha umeme wa gesi asilia pale Somangafungu megawati 320 na kule Mtwara megawati 300”. Ni wazi kabisa kwamba mchango wa gesi asilia hususan kwenye upatikanaji wa umeme wa uhakika hapa nchini ni jambo lililo wazi na la kujivunia.

Sehemu ya mitambo ya kituo cha kupokea gesi asilia Kinyerezi, kituo hiki ndicho kinachopokea gesi na kuipeleka katika mitambo ya kufua umeme na nyingine kupelekwa katika viwanda. 

Nae Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba alisema “TPDC imejipanga vema kuhakikisha gesi asilia inaendelea kupatikana kwa wingi ili kuwezesha Tanzania ya viwanda sio tu kwenye umeme bali hata kwenye viwanda moja kwa moja ambapo hutumika kama chanzo cha nishati au malighafi”. Mhandisi Musomba alieleza namna ambavyo TPDC kupitia kampuni tanzu ya Gasco walivyohakikisha wanafanya kazi usiku na mchana ili kuwezesha kuwashwa kwa mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi II. 

TPDC ambalo ni Shirika la Mafuta la Taifa ndio mmiliki wa leseni zote za utafiti na uendelezaji wa gesi asilia na mafuta nchini. Katika kutekekeleza majukumu yake, TPDC huingia mikataba ya kugawana mapato ijulikanayo kama “Production Sharing Agreement (PSA)” na kampuni za kimataifa za mafuta na gesi (IOC) ambazo hujulikana kama mkandarasi. Kazi ya mkandarasi huyu ni kufanya kazi za utafiti na uendelezaji wa mafuta na gesi kwa kushirikiana na TPDC ambapo TPDC husimamia maslahi ya nchi na kuhakikisha tozo zote pamoja na hisa za Serikali katika mikataba hiyo zinalindwa na kulipwa kwa wakati.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: