Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (aliyesimama) akifafanua hoja za wabunge kwenye semina ya Sekta ya Uvuvi kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Katikati Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa na kushoto Katibu Mkuu Uvuvi, Dkt. Yohana Budeba.(Picha na John Mapepele).
Mbunge wa Kiteto, Mheshimiwa Emmanueli Papian akichangia hoja kwenye semina ya Sekta ya Uvuvi kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.(Picha na John Mapepele).
Mbunge wa Kyerwa mkoani Kagera, Innocent Bilakwate akichangia hoja kwenye semina ya Sekta ya Uvuvi kwa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Picha na John Mapepele)

Na John Mapepele, Dodoma.

BUNGE limejitosa kuunga mkono vita dhidi ya uvuvi haramu iliyotangazwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kutaka viongozi wa ngazi zote wanaoshiriki au kufadhili uvuvi haramu watajwe kwa majina ili Taifa liweze kuwafahamu.

Hali hiyo itasaidia kumaliza kabisa tatizo la uvuvi haramu lililosababisha nchi ishindwe kunufaika na rasilimali hizo muhimu za uvuvi licha ya kuwa na eneo kubwa la maziwa,mito na bahari lenye jumla ya kilomita za mraba 346,337 sawa na asilimia 36.7 ya eneo lote la Tanzania ni maji.

Wakichangia mjadala katika semina kwa wabunge kuhusu vita dhidi ya uvuvi haramu iliandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kufanyika ukumbi wa Pius Msekwa bungeni jijini Dodoma baadhi ya wabunge hao waliitaka Serikali kuchukua hatua kali zaidi kwa watu wote wanaojihusisha na kufadhili uvuvi haramu ili nchi iweze kunufaika na rasilimali hiyo muhimu.

Mbunge wa Kyerwa mkoani Kagera, Innocent Bilakwate alisema mambo mengi katika Taifa letu kwa miaka mingi yamekuwa hayaendi kwa sababu ya viongozi waliopewa dhamana kushindwa kuchukua hatua

“Naomba Serikali iendelee kuchukua hatua kali zaidi za kupambana na uvuvi haramu na niombe waheshimiwa wabunge tushirikiane katika vita hii mambo mengi yameharibika kwa ajili ya sisi wanasiasa hivyo ni wakati wa kumuunga mkono Mhe Waziri na Mhe Rais katika kulinda rasilimali zetu za uvuvi”alisema Bilakwate.

Naye Mbunge wa Kiteto, Emmanueli Papian alisema anaamini suala la uvuvi haramu litafika mwisho na heshima ya Tanzania itarudi kutokana na maamuzi magumu yanayochukuliwa na Serikali huku akiitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutaja hadharani orodha ya viongozi wote wanaoshiriki na kufadhili uvuvi haramu ili Taifa liweze kuwafahamu kwa majina watu wanaohujumu rasilimali na kisha hatua stahiki zichukuliwe bila kujali nafasi za vyeo vyao .

Pia Mbunge huyo pia aliitaja nchi ya Uganda kama kielelezo cha mapambano dhidi ya uvuvi haramu kutokana na juhudi kubwa wanazofanya Serikali ya nchi hiyo na kuiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwachukua baadhi ya wabunge na waandishi wa habari kwenda nchini Uganda kuona namna wanavyoshughulikia uvuvi haramu.

“Kule Uganda wameweka Sheria kali ambazo zimetokomeza kabisa uvuvi haramu, naamini hili suala hili la uvuvi haramu litafika mwisho katika nchi yetu na heshima inarudi kutokana na maamuzi magumu yanayochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano ni vema tukubaliane hapa Waziri taja hadharani viongozi wanaofadhili uvuvi haramu”alisisitiza

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji, Mahmoud Mgimwa, alimhakikishia Waziri Mpina kuwa Bunge linaunga mkono vita dhidi ya uvuvi haramu na kutaka orodha ya wabunge wanaotuhumiwa kujihusisha au kufadhili uvuvi haramu itajwe ili Bunge liweze kuwafahamu na hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: