Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Ruth Msafiri akichangia jambo katika uzinduzi wa Kampeni ya Huduma, Elimu na usajili wa Walipakodi wapya Mkoani Njombe.
Mkurugenzi wa huduma na elimu kwa mlipakodi wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard kayombo akisoma hotuba ya uzinduzi wa Kampeni hiyo.
 Sehemu ya wafanyabiashara walioshiriki kwenye Uzinduzi wa kampeni ya huduma,elimu na usajili wa walipakodi wapya.

Wadau mbalimbali wakitoa maoni yao Kwa uongozi wa TRA wakati wa hafla hiyo.​
Sehemu ya Wafanyabiashara wa Mkoa wa Njombe wakiwa katika Picha ya Pamoja na Uongozi wa TRA


Mkoa wa Njombe leo umezindua rasmi kampeni ya huduma, elimu na usajili wa walipa kodi wapya lengo ikiwa ni kuwatambua rasmi walipakodi lakini pia kuwapatia elimu ili kuwawezesha kulipa kodi kwa hiari na kufanikisha adhma ya Serikali ya kukusanya mapato ambayo yanahitajika katika kuleta maendeleo ya Nchi na Wananchi kwa ujumla.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa kampeni hiyo.

“Leo tumezindua rasmi kampeni hii katika Mkoa wa Njombe na itadumu kwa muda wa wiki nzima. Niwaombe Wafanyabiashara na Wananchi wa Mkoa wa Njombe kufika kwenye vituo kwa ajili ya kupata uelewa wa masuala ya kodi, kuelezea kero na changamoto zinazowakabili lakini pia kutupa mrejesho na maoni katika huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania.”Alisema Kayombo.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Njombe katika uzinduzi huo Mkuu wa Wilaya ya Wang’ing’ombe Ally Kassinge amesema kuwa kampeni hii ni muhimu hususani katika Mkoa wa Njombe ambao ni miongoni mwa Mikoa mipya nchini kwani kupitia kampeni hiyo walipa kodi wapya watatambulika na pia itawawezesha kupata leseni za biashara na kupata mikopo katika taasisi za fedha nchini na kuwataka wafanyabiashara katika Mkoa wa Njombe kuchangamkia fursa hiyo.

“Naomba wafanyabiashara kutumia fursa hii adhimu ya kupata elimu ya masuala ya kodi yaliyokuwa yanawatatiza lakini pia ni fursa kwenu kueleza uhalisia wa mazingira ya biashara katika Mkoa wetu na ambaye hatasajiliwa na kupata namba ya utambulisho wa mlipakodi(TIN) atakuwa amekosa fursa ya kuchangia maendeleo ya Mkoa na Taifa kwa ujumla. Alisema Mkuu wa Wilaya

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi Ruth Msafiri amesema kuwa Kampeni hiyo imeamsha ari mpya katika Halmashauri zake kwani zoezi hilo lilishaanza na wilaya yake imeanzisha kituo cha uuzaji wa mazao ya misitu (mbao) na ameiomba TRA kuhakikisha wanawapatia mashine zenye kutoa risiti za kielektroniki “EFD Mashine” katika kituo hicho kijulikanacho kama Soko la UWAMIMA ili serikali iweze kukusanya mapato yake kiuhakika.

Ikumbukwe kwamba lengo la serikali ya awamu ya tano kupitia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.John Pombe Joseph Magufuli ni kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wadogo wadogo wanatambulika rasmi na kupatiwa vitambulisho ikiwa ni pamoja na kutafutiwa maeneo rafiki kwa biashara zao.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: