Maneja wa Tanesco mkoa wa Manyara Gerson Manase akiongea na waandishi wa habari hawapo kwenye picha hivi karibuni katika kampeni ya kuhamasisha wananchi kuacha kufanya shughuli za kibinadamu karibu na miundombinu ya shirika hilo.

Na Mwandishi Wetu,

Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Manyara limewatahadharisha wakazi wanaoendelea kufanya shughuli za kibinadamu karibu na miundombinu ya shirika hilo na kusema kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Tahadhari hiyo imetolewa na meneja wa Tanesco mkoa huo hivi karibuni, Gerson Manase kupitia kampeni maalumu inayofanywa na Tanesco makao makuu ikiwa na lengo la kuhamasisha juu ya athari za kuhujumu miundombinu ya shirika na kufanya shughuli karibu.

“Kuanzia sasa mkazi yoyote atakaye kiuka sheria na kufanya shughuli za kibinadamu karibu na miundombinu ya umeme, tutafyeka mazao yake yote na hatua nyingine za kisheria zitafuata,” alisema meneja huyo

Kwa sasa Tanesco Manyara inahudumia wilaya tatu ikiwemo Babati, Mbulu na Kateshi ambapo kuna wateja wapatao 28,000 na lengo ni kuongeza idadi zaidi.

Mitambo iliyosimikwa ina uwezo wa kuzalisha megawati 50 ila kwa sasa matumizi ni megawati 15 tu na kukaribisha wawekezaji kwani umeme upo wa kutosha.

Alisema wakazi hao walishalipwa fidia zao na shirika ili kupisha maeneo hayo ambayo ni hatarishi kwa maisha yao lakini kuna baadhi bado wanafanya shughuli za kilimo.

Aidha, alisema katika maeneo hayo kuna vyombo vya moto huwa vinatakiwa kupita kwa ajili ya ukaguzi wa miundombinu sasa wakati mwingine inashindikana kutokana na watu kupanda mazao katika njia hizo, matokeo yake kazi zinashindwa kufanyika kwa wakati.

Meneja alisema, “Tunatoa wito kwa wakazi wote waheshimu sharia kwani tulishaandika barua kwa wenyeviti wa vijiji kuhusiana na amza yetu. Lengo la shirika sio kumkomoa mtu ila na kuhakikisha maisha ya watu yanakuwa salama na umeme unapatikana kwa wakati,”

Katika hatua nyingine meneja huyo aliomba wakazi kuachana na tabia ya kuhujumu miundombinu hiyo na kuongeza mkoa huo umekithiri kwa wizi wa nyaya za umeme.

Alisema wizi huo unarudisha jitihada za shirika nyuma na maendeleo kwa ujumla kwani serikali inatumia gharama kubwa kwa ajili ya marekebisho.

Akitolea mfano hivi karibuni kuna wizi wa transformer ulitokea na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wateja na shirika kwa ujumla, “Vitendo hivi vinaweza kuleta maafa makubwa, badala ya kuhujumu tunaomba washirikiane na sisi kukomesha wizi huu,”

Naye Kaimu Meneja Kitengo cha Mawasiliano Tanesco Leila Muhaji alisisitiza kwamba zoezi la uhamasishaji linafanyika nchi nzima lengo ni kutoa elimu ya madhara yanayoweza kupata watu wanaojaribu kuiba vifaa au kufanya shughuli karibu ya miundombinu ya umeme.

“Hili ni shirika lenu tunaomba ushirikiano wenu ili kuhakikisha tunakuwa na umeme wa kutosha na kuvutia wawekezaji wengi nchini, serikali inatumia fedha nyingi kwa ajili ya kufanya marekebisho,” alisema Muhaji.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: