Na January Makamba.

Huyu Bwana Mkubwa huwa ananipa visa vingi vyenye kufikirisha. Kabla ya Eid nilienda kumjulia hali. Tukaanza kuzungumza jinsi ya kukabiliana na kudhalilishwa. Akanipa kisa hiki:

Wakati akiwa na miaka kama 12, baba yake (babu yangu, Mzee Rajab) alipata mtoto wa kike (mdogo wake Mzee Makamba, shangazi yangu). Utaratibu kwetu ni kwamba mwanamke akijifungua anachinjiwa mbuzi au kondoo kwa ajili ya supu. Wakati shangazi anazaliwa, Mzee Rajabu hakuwa na mbuzi wala kondoo. Kwahiyo akaamua kwenda kwa mpwa wake Mzee Kasim Juma ambaye alikuwa ana mbuzi wengi. Mzee Rajabu is a very proud man kwahiyo alipata shida sana kwenda kutafuta mbuzi kwa mtu mwingine. Lakini kwa kuwa aliona anaenda kwa ndugu yake, na mbuzi anaichukua kwa mkopo, akaona sio tatizo sana. Akaamua aende tu kuzungumza na mpwa wake.

Kufika akamkuta Mzee Kasim amekaa nje na kundi la mbuzi ndio wamerudi malishoni. Basi akaanza mbali kuelezea shida yake, huku Mzee Kasim akisikiliza kwa makini sana. Babu akatoa maelezo marefu sana.

Baada ya kumaliza, Mzee Kasim akamwambia “Ndugu yangu Rajab, mke wako umempa mimba, imekaa miezi tisa, hadi mtoto anazaliwa hujaandaa mbuzi; samahani sana siwezi kukukopesha wala kukupa mbuzi”. Babu akapandwa na hasira akafoka kwamba “sasa umeniacha najieleza nusu saa nzima wakati unajua hunisaidii kwanini usingeniambia tu, nisijidhalilishe”. Mzee Kasim akasema “ningekukatisha ingekuwa udhalilishaji zaidi”. Babu akaondoka kwa hasira. Alipofika nyumbani tu kitu cha kwanza ni kutangaza kwamba “kuanzia sasa na sisi familia yetu tunaanza kufuga, na wakati wote, hata nikifa, mji huu usikose kitoweo. Na mtu yoyote akiwa na shida kubwa - msiba, uzazi, maulidi - asaidiwe”. Hiyo ilikuwa ni mapema miaka ya 1950. Hadi leo kwenye compound ya familia kuna ng’ombe, mbuzi na kondoo. Na tunawagawa kweli, lakini hawaishi. Hawaongezeki sana lakini hawaishi.

Kila siku tunakutana na udhalilishaji. Usiache udhalilishaji upotee hivi hivi. Ufanyie kazi. Never fail to seize an opportunity that may arise from being ridiculed. Lakini pia tuwapende ndugu wanaotuambia ukweli mchungu. Urafiki na undugu kati ya Mzee Rajab na Mzee Kasim haukutetereka. Happy Father’s Day to all the fathers out there.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: