Mwandishi Wetu, Dodoma.

Wabunge wakiongozwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai wanatarajia kuosha magari ili kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vya mfano kwa watoto wa kike na wenye uhitaji maalumu.

Tukio hilo litakalofanyika kesho Jumamosi Juni 8, katika Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma, limeandaliwa na Spika Ndugai ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Umoja wa Wabunge Wanawake (TWPG), katika kampeni yao ya ujenzi wa vyoo hivyo, litahusisha uoshaji magari ya wabunge na watu mbalimbali.

Hata hivyo, tukio hili ni utangulizi wa harambee iliyoandaliwa na TWPG, itakayofanyika Juni 22 mwaka huu, jijini Dodoma ili kuchangisha fedha za kujenga vyoo vya kisasa katika majimbo yote nchi nzima ili kumkomboa mtoto wa kike apate mahitaji muhimu na kwa utulivu, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais John Magufuli.

Akizungumzia tukio la kesho, Spika Ndugai amewataka watu mbalimbali kujitokeza kuosha magari yao ili kuchangisha fedha za ujenzi wa vyoo hivyo.

“Natoa wito kwa wote wenye magari, wafike pale kwa wingi hata kama una gari lako umelipaki siku nyingi limechafuka sana na vumbi, lilete kazi hiyo ataifanya Spika pamoja na wenzake wote bungeni,” amesema.

Aidha, ametoa wito kwa wakazi wa Dodoma na mikoa jirani wafike kwa wingi uwanjani hapo kuosha magari yao.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: