Na. Andrew Chimesela - Morogoro.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe ameunda kamati ya wajumbe kumi kwa ajili ya kuchunguza wizi wa mafuta ambao umeota mizizi katika mradi wa ujenzi treni ya mwendo kasi hapa nchini (standard Gauge Railway - SGR) kipande cha Morogoro.

Dkt. Kebwe ametoa agizo la kuunda kamati hiyo Julai, 16 mwaka huu alipofanya ziara ya kushtukiza katika kambi ya Ngerengere akiongozana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kwa lengo la kujiridhisha kutokana na taarifa alizonazo za uwepo wa changamoto hiyo ya wizi wa mafuta katika mradai huo mkubwa.

Aidha, Dkt. Kebwe na Wajumbe wa KUU walitaka pia kujiridhisha jinsi kampuni hiyo inavyopokea mafuta, inavyotoa na jinsi inavyofuatilia matumizi ya mafuta hayo kwa waendesha mitambo mbalimbali katika eneo hilo la Ngerengere.

Baada ya kumaliza kikao cha ndani kati ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na uongozi wa Kamapuni inayoendesha mradi huo wa SGR, ndipo Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akatoa agizo kwa Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Lucas Mwaisaka kuunda Kamati ya Uchunguzi.

Kamati hiyo ya Wajumbe kumi imepewa siku saba na kuwasilisha taarifa yake Julai 24 mwaka huu, taarifa hiyo pamoja na hadidu nyingine za rejea ieleze mlolongo mzima wa upokeaji na utoaji wa mafuta, kuchunguza watu wanaojihusisha kwa ufisadi huo wa mafuta kama wako ndani au nje ya kampuni hiyo. 

Hata hivyo Dkt. Kebwe alimuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro kuanza mara moja oparesheni itakayofanyika usiku na mchana ya kuwasaka wahusika wa wizi wa mafuta hayo, huku akitaka meneja wa Kampuni ya ujenzi wa SGR kukaa pamoja na Kamanda huyo ili kukubaliana namna polisi watakavyoshiriki katika ulinzi wa mafuta na mali nyingine za mradi huo. 

Naye Meneja wa Earth Works Joao Sousa alisema kwao ni vigumu kujua kama mafuta hayo yanaibiwa wakati wa kazi ama wakati wa chakula cha mchana ambapo waendesha mitambo wengi wanapata chakula na mitambo inakuwa imezimwa na mitambo mingine inakuwa maeneo ya mbali na maeneo wanayopata chakula cha mchana.

Akijibu swali la Mkuu wa Mkoa juu ya upotevu wa mafuta, Msimamizi wa Walinzi katika Kampuni hiyo Evance Mwakitwange alitaja moja ya sababu za wizi huo kuwa ikiwa ni pamoja na uchache wa walinzi ukilinganisha na wingi wa mitambo na eneo kubwa linaloegeshwa mitambo hiyo. lakini pia alieleza kuwa usumbufu mkubwa katika kulinda mitambo hiyo wanaupata wakati waaendesha mitambo wanapokwenda kupata chakula cha mchana.

Alisema wamejitahidi kupambana sana na tatizo la wizi wa mafuta lakini suala la kutoegesha pamoja mitambo hiyo wakati wa chakula cha mchana ni changamoto pamoja na kuwa walishatoa ushauri kwa uongozi kuegesha pamoja mitambo hiyo lakini ushauri wao haujafanyiwa kazi.

Aidha, Mwakitwange ameyataja maeneo ambayo yanaongoza kwa wizi wa mafuta kuwa ni eneo la kilometa 157, 158 na kilometa 160 ambavyo viko eneo la Mikese huku akibainisha kuwa jitihada zao katika kuepusha wizi huo walitoa taarifa Kituo cha Polisi na kuomba msaada zaidi.

Wajumbe walioteuliwa kwenye kamati hiyo ni pamoja na mjumbe mmoja kutoka Ofisi ya RPC, RSO na TAKUKURU kwa ngazi ya Mkoa. Wajumbe wengine ni kama waliotajwa hapo juu lakini ni kwa ngazi ya Wilaya. Mjumbe mwingine atatoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na watatu watatoka upande wa Kampuni inayoendesha mradi wa SGR.

Kwa taarifa zilizomfikia mwandishi wa habari hizi, hadi msafara wa Mhe. Mkuu wa Mkoa unarejea Ofisini kwake tayari mtu mmoja kati ya wanaotuhumiwa kujihusisha na mtandao wa wizi wa mafuta katika kampuni hiyo alikuwa ametiwa nguvuuni na jeshi la polisi kwa mahojiano.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: