Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (katikati) akimsikiliza Mtaalam wa kutengeneza mvinyo wa kiwanda cha CETAWIKO cha Jijini Dodoma, Bw. Erick Shulz (kushoto) namna mvinyo unavyotengenezwa kiwandani hapo wakati alipotembelea kiwanda hicho kwa ajili ya kutambua changamoto zinazowakabili Wawekezaji.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (kulia) akimsikiliza Mtaalam wa kutengeneza mvinyo wa Kiwanda cha Kutengeneza Mvinyo (CETAWICO) cha Jijini Dodoma, Bw. Erick Shulz namna mvinyo unavyochambuliwa kwa kutumia mtambo maalum kiwandani hapo wakati alipotembelea kiwanda hicho kwa ajili ya kutambua changamoto zinazowakabili Wawekezaji.
Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Kutengeneza Mvinyo (CETAWICO), Bw. Fiorenzo Chesini (kulia) akimuonyesha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (katikati) kifaa maalum kutumikacho kupimia kiasi cha ukali wa mvinyo wakati alipotembelea kiwandani hapo kwa ajili ya kutambua changamoto zinazowakabili Wawekezaji.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere (kulia) akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Kutengeneza Mvinyo (CETAWICO), Bw. Fiorenzo Chesini akimueelezea namna ya baadhi ya mashine za kiwandani hapo zinavyofanya kazi mpaka kuhakikisha kuwa mvinyo mzuri unapatikana, wakati alipotembelea kiwandani hapo kwa ajili ya kutambua changamoto zinazowakabili Wawekezaji. (PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-TRA).

Na Rachel Mkundai.

KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bwana Charles Kichere ameahidi kushughulikia changamoto za kikodi zinazoikabili sekta ya uzalishaji mvinyo nchini ili kuwawezesha wawekezaji na Wakulima wa zao la zabibu kuweza kunufaika.

Kauli hiyo ameitoa Jijini Dodoma alipotembelea kiwanda kinachozalisha mvinyo cha Central Tanzania Wine Company CETAWICO ambapo alipata fursa ya kuzungumza na mwekezaji wa kiwanda pamoja na wakulima wa zabibu ambao ndiyo wazalishaji wa malighafi kiwandani hapo.

“Nimezumgumza na mwekezaji wa kiwanda hiki na changamoto ninazoziona ni za kisera, na hivyo nitaziwasilisha Wizara ya Fedha na Mipango ili ziweze kufanyiwa kazi”, amesema Kamishna Kichere.

Aidha, Kamishna Kichere amemtaka mwekezaji wa kiwanda hicho kuwasilisha changamoto hizo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ili zipatiwe ufumbuzi kwa upande wa masuala ya kibiashara.

“Ni vema changamoto hizi pia uziwasilishe katika wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ili ziweze kushughulikiwa sambamba na masuala ya sera za kodi ambayo yatashughulikwa na Wizara ya Fedha na Milanzi”, amesisitiza Kichere.

Kwa upande wake mwekezaji wa kiwanda hicho, Bw. Fiorenzo Chesini amemshukuru Kamishna Mkuu wa TRA kwa kumtembelea kiwandani hapo na kusema kuwa, kwa kushirikiana na Serikali changamoto za kikodi na nyinginezo zinazoikabili sekta ya uzalishaji mvinyo zinaweza kutatuliwa.

“Kwa kutembelewa na Kamishna Mkuu wa TRA, nina uhakika changamoto zetu sasa zitatatuliwa na sisi tutaendelea kufanya uwekezaji Tanzania na kununua zabibu nyingi kutoka kwa wakulima”, amesema Bw Chesini.

Kwa upande wao baadhi ya Wakulima wa zao la zabibu katika kijiji cha Hombolo Mkoani Dodoma wameiomba Serikali pamoja na mwekezaji wa kiwanda hicho kutafuta suluhu ya changamoto mbalimbali katika sekta hiyo ili mwekezaji aweze kununua zabibu zao katika msimu ujao.

“Msimu wa mavuno unakaribia sana kufika hapo mwezi Agosti na kama unavyoona zabibu zimeshakomaa ila hatuna uhakika kama mwekezaji atanunua zabibu zetu, tunaomba serikali itusaidie kumaliza changamoto ili tuweze kuuza zabibu zetu msimu ujao”, alisema mkulima Fred Mwaluko.

Hivi karibuni kumekuwepo na malalamiko juu ya uwepo wa kodi kubwa kwenye pombe kali zinazozalishwa nchini kulinganisha na pombe kali zinazoingizwa kutoka nje ya nchi ambapo kiwanda cha CETAWICO ndicho kinachotengeneza sehemu kubwa ya malighafi inayotumika kutengeneza baadhi ya pombe kali za hapa nchini ambapo malighafi hiyo pia inatokana na zao la zabibu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: