Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akiondoka kuendelea na ziara yake baada kujibu kero mbalimbali za wananchiwaliosimamisha msafara wake katika kijiji cha Kisumba katika wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa jana. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura na Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Rukwa, Albinus Mugonya ambaye amebeba mabango yenye kero za wananchi hao.

Sehemu ya wananchi hao wakimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla akijibu kero mbalimbali za wananchi wa kijiji cha Kisumba katika wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa baada ya msafara wake kusimamishwa na wananchi hao jana.

Na Hamza Temba, Kalambo, Rukwa.

Msafara wa Waziri wa Maliasili, Dk. Hamisi Kigwangalla umelazimika kusimama kwa muda baada ya kusimamishwa na kundi kubwa la wananchi wa kijiji cha Kisumba kilichopo wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa wakiwa na mabango yanayoeleza kero zao mbalimbali.

Miongoni mwa kero hizo ni pamoja na wanyamapori jamii ya Tembo kuvamia mashamba yao na hivyo kukosa chakula na kukosekana kwa huduma muhimu ya maji iliyotokana na kuchakachuliwa kwa mradi wa maji wa jumla ya shilingi milioni 663 kijijini hapo.

Mkazi wa kijiji hicho, Leonard Kiombe, alisema mara nyingi wamekuwa wakiwasimamisha viongozi kwa sababu ya kero ya maji, "tulipata mradi wa milioni 663 wakasema zaidi ya vijiji 6 vitapata maji lakini kijii cha kisumba mpaka sasa hatuna maji, mradi umechakachuliwa na maji hayatoki" alisema.

Akijibu kero hizo, Waziri Kigwangalla amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha Taasisi za Uhifadhi wa Wanyamapori pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS wanashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kutengeneza vikundi vya wananchi wa vijiji vyote vinavyopakana na Hifadhi ya Msitu wa Kalambo na Pori la Akiba Lwafi ili wawezeshwe fedha za mikopo ama mizinga ya kufugia nyuki ambayo wataipanga pembezoni mwa mashamba yao ili kuzuia tembo wasiingie kwenye mashamba.

Alisema teknolojia hiyo imethibitika kusaidia kudhibiti tembo wasilete madhara kwenye makazi ya watu kwa kuwa nyuki hufukuza tembo na endapo tembo nao wakinusa harufu ya nyuki huwa sio rahisi kusogelea maeneo hayo, hivyo ameagiza mradi huo utekelezwe ndani ya kipindi cha miezi miwili kabla mvua za masika kuanza.

Waziri Kigwangalla pia ametoa wito kwa wananchi hao kuacha kufanya shughuli zao kwenye maeneo ya hifadhi ikiwemo maeneo ya mapito ya wanyamapori kwakuwa kufanya hivyo ni kuhatarisha maisha na ustawi wao.

Akizungumzia kero ya maji, Dk Kigwangalla aliwaahidi wananchi hao kuiwasilisha kwa waziri husika ili iweze kuapatiwa ufumbuzi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: