Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere (kulia) akizungumza na wananchi waliotembelea Banda la TRA katika Maonyesho ya 42 ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba kwa ajili ya kulipa Kodi ya Majengo wakati Kamishna Mkuu huyo alipotembelea banda hilo kuona huduma mbalimbali zinazotolewa kwa wananchi.
 Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere (katikati) akikagua bili ya Kodi ya Majengo aliyopewa mteja (kulia) wakati alipotembelea banda la TRA katika Maonyesho ya 42 ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba kuona huduma mbalimbali zinazotolewa kwa wananchi. Kushoto ni Meneja wa Huduma wa TRA Bi. Honester Ndunguru.
 Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere (katikati) akijibu hoja za mteja aliyempigia simu wakati alipotembelea banda la TRA katika Maonyesho ya 42 ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba kuona huduma mbalimbali zinazotolewa kwa wananchi. Kushoto ni Afisa Kodi Bi. Levina Shirima na kulia ni Meneja wa Huduma Bi. Honester Ndunguru.
 Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere akimsikiliza Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Temboni iliyopo jijini Dar es Salaam Ally abdallah (kulia) wakati alipotembelea banda la TRA katika Maonyesho ya 42 ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba kuona huduma mbalimbali zinazotolewa kwa wananchi. Kushoto ni Mwanafunzi mwenzake Safinia Shani.
Baadhi ya wateja wakitoka katika Banda la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) lililopo mkabala na banda la Azam ndani viwanja vya Sabasaba. (PICHA ZOTE NA VERONICA KAZIMOTO).

Na Veronica Kazimoto, Dar es Salaam.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere ametoa wito kwa wananchi kujenga tabia ya kulipa kodi mbalimbali kwa wakati ikiwepo Kodi ya Majengo ili kuepuka usumbufu unajitokeza tarehe za mwisho za kulipa kodi hizo.

Akizungumza leo na wananchi waliotembelea banda la TRA katika maonyesho ya 42 ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba, Kamishna Mkuu huyo amesema kuwa, wananchi wengi husubiri tarehe za mwisho ili kulipa kodi suala linalosababisha foleni na malalamiko kutoka kwa wananchi hao.

"Tumetangaza kwa muda mrefu kuhusu kulipa Kodi hii ya Majengo lakini hamkutaka kulipa kwa wakati, matokeo yake foleni imekuwa kubwa na sasa mnaanza kulalamika kwamba mnachelewa kupata huduma. Jengeni tabia ya kulipa kodi kwa wakati ili muweze kuondokana na usumbufu huu usio wa lazima," alisema Kichere.

Kamishna Mkuu Kichere ameongeza kuwa, kodi ya majengo ya mwaka 2018/19 inaaza kulipwa tarehe 1 Julai 2018 na mwisho wa kulipa kodi hiyo ni tarehe 30 Juni, 2019. Hivyo, wananchi waanze kulipa mapema ili kuondoa usumbufu wa kukaa kwenye foleni.

Naye mwananchi aliyetembelea banda la TRA kwa ajili ya kulipa Kodi ya Majengo Shabani Mkolimwa, amefurahishwa na huduma alizozipata katika banda hilo na kuiomba Mamlaka kusogeza huduma hizo karibu na maeneo wanayoishi.

"Leo nimefurahi sana kwasababu nimepata huduma za TRA na huduma za benki ndani ya banda moja. Ninaiomba TRA ituletee huduma hizi kwenye Serikali zetu za Mitaa ili iwe rahisi kwetu kupata huduma hizi za TRA kwa haraka," alisema Mkolimwa.

Mamlaka ya Mapato Tanzania imeshiriki katika Maonyesho ya Sabasaba na banda lake lipo mkabala na banda la Azam ambapo pamoja na kupokea maoni kutoka kwa wananchi, huduma mbalimbali zinatolewa ikiwa ni pamoja na Kulipa Kodi ya Majengo, Usajili wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) na Elimu ya Mlipakodi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: