Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii, Kanda ya Kaskazi.

MAHAKAMA kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi imewahukumu washtakiwa watano kunyongwa hadi kufa, huku ikimuachia huru mshtakiwa wa pili ambao kwa pamoja walikuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya kukusudia ya mfanyabiashara wa Madini ya Tanzanite,Bilionea, Erasto Msuya.

Waliohukumia adhabu ya kifo ni mshtakiwa wa kwanza Sharif Athuman ,mshitakiwa wa tatu,Musa Mangu,Mshitakiwa wa tano, Karim Kihundwa, mshitakiwa wa sita, Sadiq Jabir na mshtakiwa wa saba, Alli Majeshi.

Akisoma hukumu hiyo jana ,Jaji Salma Maghimbi wa Arusha alisema mahakama hiyo imejiridhisha pasipo shaka kwamba washtakiwa watano ndio waliohusika kutekeleza mauaji ya kukusudia ya mfanyabiashara huyo lakini imeshindwa kumtia hatiani mshitakiwa wa pili ,Shaibu Said maarufu Mredii kutokana na ushahidi kushindwa kumuunganisha katika tukio la mauaji.

Awali akisoma maelezo ya kila Mshtakiwa kabla ya kutoa hukumu ,Jaji Maghimbi alisema katika shauri hilo namba 12 la mwaka 2014 upande wa Jamhuri uliwasilisha Mashahidi 27 na vielelezo 26 ambapo vielelezo 21 kati ya hivyo ni vya maandishi na vitano ni ushahidi wa vitu.

Jaji Maghimbi mesema upande wa utetezi uliwasilisha Mashahidi nane pamoja na vielelezo vinne vya maandishi huku akitaja baadhi ya vielelezo vilivyo wasilishwa na upande wa jamhuri kuwa ni pamoja na Pikipiki mbili moja aina ya King Lion namba T751 CKB na Toyo namba T316 CLG zinazotajwa kutumika kutumiwana washtakiwa.

Vielelezo vingine vilivyowasilishwa mahakamani hapo ni pamoja na maelezo ya Onyo ,yaliyotolewa na washtakiwa wa kwanza ,Sharif Athuman, wa tatu ,Musa Mangu na wa saba,Alli Majeshi huku maelezo ya ungamo yakitolewa na Karim Kuhundwa.

Aidha Jaji Maghimbi ameeleza kuwa awali shauri hilo lilikuwa na washitakiwa saba ambapo mmoja kati yao, mshtakiwa wa wanne Jalila Zuberi, Mahakama ilimuachia huru Mei 29,2018 kutokana na kutokupatika na kutotajwa mahala popote wakati wa uwasilishwaji wa ushahidi wa upande wa Jamhuri.

Katika maelezo yake Jaji Maghimbi amesema baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashitaka ,kwa mshtakiwa wa kwanza, Sharif Athuman,ushahidi umeonyesha bayana kuwa ndiye mhusika katika kupanga mauaji ya mfanyabishara huyo kwa kuwatumia washtakiwa wengine.

Kuhusu mshitakiwa wa tatu, Musa Mangu, Jaji Maghimbi alisema pamoja na kujua nia ovu ya mauaji dhidi ya Marehemu,mshtakiwa aliendelea kushiriki na hakuonyesha nia ya kujitoa na kwamba katika maelezo yake alijaribu kuonyesha kuwa yeye hakuusika katika mauaji bali watuhumiwa wenzake ikiwemo aliyekuwa bosi wake Sharifu Athuman.

Maelezo kuhusu Mshtakiwa wa tano ,Karim Kihundwa na wa sita Sadiki Jabir ,Jaji Maghimbi alisema mshtakiwa wa tano alikiri kosa la kufyatua risasi na kumuua Msuya na kwamba kwa mujibu wa ushahidi ulitolewa unaonyesha jinsi walivyotoa ushirikino wa kupatikana kwa bunduki walioitumia katika mauaji.

Mshitakiwa wa Sita Sadiki Jabir, hakuonyesha uwoga wowote wakati akitoa maelezo ya ungamo kwa mlinzi wa Amani na kwamba mahakama imeridhika na ushahidi ulitolewa dhidi yao wa kushiiki kufanya mauaji hayo kwa makusudi.

Jaji Maghimbi amesema mshitakiwa wa saba, Ally Majeshi, kulingana na ushahidi ulitolewa ndiye alikuwa mtu wa kwanza kumvuta eneo la mauaji marehemu Msuya na kwamba ndiye aliyetaja fedha walizoahidiwa kulipwa baada ya kutekeleza mauaji hao.

Awali kabla akizungumza kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo Wakili wa serikali, Ignasi Mwinuka, aliiomba Mahakama hiyo itoe adhabu stahiki kwa washtakiwa hao kama sheria inavyoelekeza.

Akiwakilisha Jopo la Mawakili wa upande wa utetezi, Wakil Majura Magafu, alisema kulingana na umri mdogo wa shitakiwa hao Mahakama ione umuhimu wa kuwawaweka katika orodha ya watu wanaostahili msamaha wa Rais haswa ikizingatiwa wamekwisha kaa mahabusu kwa muda wa miaka mitano.

Jopo la mawakili wa upande wa utetezi katika shauri hilo uliongozwa na Wakili Hudson Ndusyepo, Majura Magafu,Emanuel Safari na John Lundu huku upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Abdala Chavula,Omary Kibwana,Kassim Nasir,Neema Mwenda,Wiliam Maugo,Lilian Kyusa,Ignasi Mwinuka,Verediana Mlenza.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: