Msajili wa Vyama vya Siasa Mhe. Jaji Francis S.K.Mutungi akionyesha kitabu chenye kuelimisha uma juu ya makatazo yaliyomo katika Sheria ya Gharama za Uchaguzi wakati wa Mafunzo ya Watumishi yaliyofanyika leo Julai 11, 2018 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Bi. Piencia Kiure, Msajili Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Gharama za Uchaguzi na Elimu kwa Umma akitoa mwongozo wa namna sahihi ya ujazaji wa fomu za gharama za uchaguzi kwa wagombea na vyama vya siasa ambazo hubainisha mapato na matumizi wakati wa uchaguzi.
Mwanasheria Mwandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa Bi. Monica Mwailolo , mmoja wa wakufunzi akiwakilisha mada wakati wa mafunzo.
Baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Msajili wa Vyaa vya siasa wakati wa Mafunzo

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imetoa mafunzo maalumu kwa watumishi wa ofisi yake ili kuwajegea uwezo wa kufanya uangalizi wa uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika tarehe 12 Agosti 2018 katika jimbo la Buyungu na kata 79.

Mafunzo hayo yamefanyika leo Julai 11, 2018 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambapo mada mbalimbali zimewasilishwa zikiwemo mada juu ya Elimu ya Maadili ya Vyama vya Siasa, Haki na wajibu wa Vyama vya Siasa, wajibu wa Msajili wa Vyama vya Siasa, matendo yanayokatazwa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi na Sheria ya Vyama vya Siasa, Umuhimu wa kujaza fomu za gharama za Uchaguzi.

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Mhe. Jaji Francis S.K. Mutungi amewawataka watumishi hao kufanya kazi kwa ueledi na kwa kufuata sheria za nchi.

“ kila mmoja wetu atambue kuwa ofisi yetu imepewa dhamana kubwa ya kusimamia Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 ili kudumisha demokrasia ya vyama vingi nchini, ni wajibu wetu kufanya kazi kwa ueledi na kwa mujibu wa sheria” amesisitiza Jaji Mutungi

Naye Bi. Piencia C. Kiure mmoja wa wakufunzi katika mafunzo hayo ambaye ni Msajili Msaidizi anayeshughulika na masuala ya Gharama za Uchaguzi na Elimu kwa Umma amesisitiza umuhimu wa wagombea na vyama vya Siasa kurejesha fomu za Gharama za uchaguzi zinazobainisha mapato na maksio ya kiwango cha matumizi wakati wa uteuzi,kampeni na uchaguzi ndani ya muda uliotengwa kisheria ili kuepuka ukiukwaji wa sheria ya Gharama za Uchaguzi.

Watumishi pia wamesisitizwa kuhakikisha wanavikumbusha vyama vya siasa na wagombea kunadi sera za vyama vyao kwa kusimamia maadili ya vyama vya siasa ili kuendelea kudumisha amani ya nchi.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni taasisi yenye wajibu wa kisheria wa kufanya uangalizi wa mwenendo wa chaguzi zinazofanyika kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wagombea na vyama vya siasa vinatekeleza matakwa ya sheria kwa kuepuka vitendo ambavyo vimekatazwa na sheria hizi ili kuimarisha demokrasia ya vyama vingi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: