Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala, akizungumza na wafanyabiashara wa Wilaya hiyo wakati wa Mkutano kati ya Wafanyabiashara hao na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (hayupo pichani).
Mfanyabiashara wa Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma Bw. Musa Ndiliwe, akieleza kuhusu kuimarishwa kwa mazingira bora ya kibiashara katika Soko la Ujirani mwema kati ya yao na wenzao wa Nchini Burundi kwa lengo la kukuza biashara, wakati wa mkutano kati ya wafanyabiashara hao na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) Wilayani hapo.
Wafanyabiashara Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma wakimsikiliza kwa Makini Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (hayupo pichani), alipofanya mkutano ulioangazia namna bora ya kuboresha mazingira ya kibiashara katika Wilaya hiyo.
Maafisa wa Wizara ya Fedha na Mipango walioko kwenye msafara wa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, wakifuatilia mkutano kati ya Serikali na wafanyabiashara wa wilaa ya Kakonko mkoani Kigoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati), akiwaasa wafanyabiashara wa Wilaya ya Kakonko Mkoani Kigoma (hawapo pichani) kutumia fursa zilizopo katika nchi jirani ikiwemo Burundi kuuza bidhaa zilizoongezwa thamani ili kukuza uchumi wa Wilaya hiyo, alipofanya mkutano na Wafanyabiashara hao Wilayani hapo, kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala, na kulia ni Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kakonko Bw. Kadudusi Bunabuna.
Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA anaye husika na kodi za, ndani Bw. Elijah Mwandumbya, akifafanua masuala mbalimbali ya kikodi kwa wafanyabiashara wa wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, wakati Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji alipokutana na wafanyabiashara hao kujadili fursa na changamoto wanazopata.
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, mkoani Kigoma, Kanali Hosea Ndagala, akiwataka wafanyabiashara wa Wilaya hiyo kuzingatia taratibu za kibiashara na kuhakikisha wanajipanga kuanzisha viwanda vidogo ili kuongeza thamani ya bidhaa wanazouza nje ya nchi, wakati wa mkutano kati ya Wafanyabiashara wa Wilaya hiyo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wa pili kushoto). (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango).

Benny Mwaipaja, Kakonko, Kigoma.

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, amewashauri wakazi wa Wilaya ya Kakongo na mkoa wa Kigoma kwa ujumla kuchangamkia fursa za biashara kati ya mkoa huo na nchi jirani za Rwanda na Burundi kwa kuuza mazao ya kilimo yaliyochakatwa likiwemo zao la muhogo ili waweze kunufaika na biashara hiyo ya mipakani.

Dkt. Kijaji ametoa rai hiyo mjini Kakonko baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa wilaya hiyo, mkutano uliolenga kujadili fursa na changamoto za ufanyaji biashara katika eneo hilo yakiwemo masuala ya kikodi.

"Nakuomba Mkuu wa Wialaya ya Kakonko uwakutanishe na kuwaunganisha wafanyabiashara hawa ambao nafurahi wengi wao ni vijana ili waandae andiko la namna ya kununua mashine za kuongeza thamani ya mazao ili wauze nje yakiwa yamechakatwa badala ya mfumo wa sasa ambao wanauza mazao ghafi nje ya nchi na hivyo kupata hasara" alisisitiza Dkt. Kijaji.

Awali, wafanyabiashara wa Kakonko walimweleza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu kijaji, aliyeambatana na Kamishna wa Mapato ya ndani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Bw. Elijah Mwandumbya, kwamba, bei ya zao la muhogo imeshuka kutoka shilingi 600 kwa kilo katika msimu uliopita hadi kufikia shilingi 150, hali iliyowasababishia wakulima maumivu makubwa.

"Wafanyabiashara wanaonunua mazao yetu kutoka Burundi ni watu wa kati kwa maana ya madalali ambao wananunua mazao yetu kwa bei nafuu na kuyapeleka n hini kwao ambako huyachakata na kuyauza kwa bei kubwa nchini mwao na nchi za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya kongo, hivyo tunaiomba Serikali itupatie mikopo kupitia Benki ys Kilimo ili tusnzishe viwanda vya kuchakata mazao yetu" alieleza mfanya biashara Dkt. Brighton Gwamagobe

Akizungumza katika Mkutano huo, Kamishna wa TRA wa Mapato ya Ndani Bw. Elijah Mwandumbya, pamoja na kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kodi, ametoa wito kwa wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari ili kuiwezesha Serikali kupata fedha za kuhudumia jamii ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya, maji na mambo mengine kadha wa kadha.

Alisema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya ukusanyaji kodi na kutatua kero mbalimbali za wafanyabishara pamoja na kuongeza wigo wa walipa kodi ili kuimarisha mapato ya nchi

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, yuko katika ziara ya kikazi mkoani Kigoma ambapo anakagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayopatiwa fedha na Serikali pamoja na kuzungumza na jumuiya ya wafanyabiashara.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: