Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Magubike wakipatiwa Hati Miliki za Kimila na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mhe. Adam Mgoyi. Picha ya mwisho ni Bw. Jackson Mgoma, akiwa katika furaha baada ya kuipata Hati hiyo.
DC Kilosa Mhe. Adam Mgoyi akiongea na wanachi wa Kijiji cha Magubike (hawapo pichani)katika tukio la kugawa Hati miliki, zoezi linaloendeshwa na MKURABITA kwa lengo la kuwaondolea wananchi umasikini na kuwawezesha kuendesha uchumi kutokana na mali walizo nazo wenyewe. Kulia kwa DC aliyekaa ni Katibu Tawala wa
Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) Bi. Seraphia Mgembe, akisisitiza jambo mara baada ya Hati miliki kutolewa kwa Wananchi wa Kijiji cha Magubike waliorasimishiwa Ardhi.
Huu ndio muonekano wa Hati miliki ambayo kwayo inasaidia kupunguza migogoro ya Ardhi ndani ya Vijiji, inasaidia Mwananchi kumiliki Ardhi yake kisheria na inapandisha thamani ya Ardhi baada ya kurasimisha na kupatiwa hati hiyo.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Magubike Wilayani Kilosa waliopatiwa Hati za haki Miliki wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi (Katikati waliokaa) na Viongozi wa wengine wa Wilaya hiyo na Viongozi wa MKURABITA. Hii ni mara baada ya kukabidhiwa hati za kurasimisha Ardhi kwa lengo la kutambulika kisheria hivyo kusaidia kuondoa umasikini miongoni mwao.
Hongera wananchi Wilayani Kilosa kwa mwamko wa kurasimisha Ardhi yenu hivyo kuwa na ulinzi wa Ardhi hiyo, kuongeza thamani na kusaidia kupunguza migogoro mliyokuwa nayo kwa muda mrefu. Huo ndio muarobaini pekee.

Na Andrew Chimesela – Kilosa, Morogoro

Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) umewezesha wakulima 17 Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro kukopeshwa zaidi ya shilingi 500Mil. baada ya Vijana hao kurasimisha Ardhi yao, kupata Hati, kujiunga pamoja hivyo kukidhi vigezo vya kukopeshwa kitita cha fedha hizo.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi, Agosti 21 mwaka huu mara baada ya kukabidhi hati za haki miliki zaidi ya 300 kwa wananchi wa Kijiji cha Magubike Wilayani humo Mkoani Morogoro.

Akifafanua zaidi, Mkuu huyo wa Wilaya ya Kilosa amesema, fedha hizo zilitolewa kwa wakulima wadogo wa mashamba ya miwa kutoka Benki ya Maendeleo ya Wakulima Tanzania (TAB) ili waweze kupata fedha za kuwasaidia kulima kilimo ambacho ni bora zaidi na chenye tija.

Ameongeza kuwa katika Wilaya ya Kilosa sio Benki hiyo tu inayoonesha nia ya kuwakopesha wananchi wenye hati miliki, bali kuna Benki nyingine ziko tayari kuwakopesha wakulima, nyingine zimekwisha wakopesha, changamoto ilikuwa wakulima wengi kutokuwa na hati miliki.

“Mbali na Banki hiyo, Banki zote hizo zina madirisha ya kukopesha, ndani ya Wilaya ya Kilosa tunayo Banki ya CRDB inafanya kazi kama hizo lakini tunayo Banki ya AZANIA ambayo inatumia njia nyingine, imeanza kuonesha nia ya kuwakopesha, changamoto ilikuwa upatikanaji wa hati hizi za kimila, lakini nyingi zinaonesha nia ya kukopesha kama hati hizi zitaendelea kupatikana” alisema Mgoyi.

Mkuu huyo wa Wilaya ametumia nafasi hiyo, kuwataka wananchi kutoka vijiji 37 ambavyo tayari vimekwisha fanyiwa upimaji wa Ardhi na kuweka mpango Bora wa matumizi ya Ardhi, waliopata hati hizo siku za awali na wale waliopata siku hiyo, kutumia fursa hiyo ili kuondokana na umaskini waliokuwa nao.

Sambamba na kuwashauri wananchi kutumia vema hati zao, Mhe. Adam Mgoyi ameutaka Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kutenga fedha kwa ajili ya kusaidia upimaji wa ardhi ambao utapelekea kuwepo matumizi bora ya Ardhi jambo ambalo litawafanya wananchi wengi kunufaika na hati hizo.

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya hakuridhika na kasi ya wananchi kwenda kuchukua hati ambazo zimekwisha kamilika.

“Lakini wako baadhi yenu, hati zimekamilika kwenda kuchukua tu imekuwa shida. Huu ndio uthibitisho wa umiliki wenu wa Ardhi, Ardhi ya Nyunmba ulionayo, Ardhi ya mashamba. yanakuepusha na migogoro, lakini bado zoezi hili utekelezaji wenu umekuwa chini sana. Ninawasihi nendeni mkachukue hati zenu” alisema Mhe. Mgoyi.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya amebainisha kuwa, Utulivu na amani iliyopo sasa Wilayani humo, baada ya kuwa na migogoro ya Ardhi kwa muda mrefu, amani hiyo inatokana na utekelezaji wa MKURABITA.

Naye Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) Bi. Seraphia Mgembe amewataka Wakurugenzi kuwasaidia wananchi wenye hati katika kuwaunganisha na taasisi za kifedha ili wapate mikopo hivyo kufikia lengo la Serikali la kutaka wananchi waweze kumiliki uchumi wao wenyewe hivyo kumuunga Mkono Mhe Rais ambaye anaimba kila leo kuhusu Tanzania kufikia Uchumi wa Kati.

Kwa upande wao wananchi wa Kijiji cha Magubike wakiwemo Bi. Festa Mgula na Bw. Jackson Mgoma, kwa niaba ya wananchi wengine wameishukuru Serikali kuwa na mpango huo wa kurasimisha ardhi, kwa kuwa wamesema kufanyi hivyo kunapunguza migogoro ya Ardhi ndani ya Vijiji vyao, kumiliki Ardhi yao kisheria na kupanda kwa thamani ya Ardhi yao hasa baada ya kurasimisha na kupatiwa hati ya haki Miliki.

Imeelezwa kuwa katika Wilaya ya Kilosa tayari mashamba 2,000 yamepimwa kati yao 1,804 yametengenezewa hati ya umiliki wa muda.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: