Na Emmanuel J. Shilatu

Kama ambavyo Watanzania tunavyomkumbuka Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa kusaidia ukombozi wa upatikanaji wa uhuru ama kama ambavyo Hayati Moringe anavyokumbukwa kwa mapambano ya ubadhirifu wa mali za umma, pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anazidi kujenga historia ya kipindi chote isiyofutika kutokana na utendaji, uchapakazi na uzalendo wake kwa Taifa.

Haya hapa ni baadhi ya Mambo ya kihistoria na yenye heshima kubwa kwa Taifa ambayo Rais Dkt. Magufuli aliyoyafanya;-

(i) Kuhamia Dodoma

Wazo la Serikali kuhamia kwenye makao makuu ya nchi mkoani Dodoma liliasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere mwaka 1973 lakini lilishindwa kutekelezwa katika awamu zote. Si awamu ya kwanza, wala ya pili, ama ya Tatu au ya nne bali limeweza kufanikiwa kwenye utawala wa Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Magufuli. Leo hii karibia Serikali yote imehamia Dodoma. Wizara, taasisi na idara za Serikali, Waziri Mkuu wameshahamia Dodoma. Mwishoni mwa mwaka huu Rais Magufuli naye atahamia Dodoma. Iliasisiwa na Mwalimu Nyerere, ikahaidiwa kwenye ilani ya uchaguzi, imekuja kutekelezwa vyema na Rais Magufuli. Hii ni historia isiyofutika ya uthubutu, uzalendo alionao Rais Magufuli.

(ii) Ujenzi wa Miundombinu

Hili halina ubishi kwa asilimia kubwa kabisa miundombinu ya nchi hii imejengwa chini ya usimamizi wa Dkt. Magufuli toka alipokuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Waziri wa Ujenzi na sasa Rais wa nchi. Hauwezi ukazungumzia uwepo wa mitandao ya barabara nchi nzima pasipo kumtaja Rais Magufuli; hauwezi kuzungumzia uwepo wa madaraja makubwa ya kisasa kama ya Daraja la Nyerere, Daraja la Mkapa pasipo kumtambua mchango wa Rais Magufuli. Leo hii nchini tunajivunia uwepo wa flyovers. Rais Magufuli ameonyesha uwezo na heshima kubwa ya ujenzi wa Miundombinu nchini ambayo imekuwa msaada mkubwa wa kimawasiliano, usafirishaji wa Watu na mizigo, kukuza utalii, kuimarisha shughuli za kibiashara na kuongeza mapato ya nchi.

(iii) Kulifufua Shirika la Ndege

Tangu mwaka 1977 nchi yetu ilikuwa na shirika la ndege linalosua sua na linalojiendesha kihasara kubwa. Mara baada ya Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Magufuli imefanikiwa kununua ndege mpya 7 na mpaka sasa zimeshawasili ndege mpya 4 ikiwamo ndege kubwa aina ya Boeing 787-8. Wale baadhi wanaosema ndege si kipaumbele wala muhimu kwa Watanzania inabidi watambue Leo hii makusanyo ya mapato ndani ya Shirika la ndege (ATCL) yametoka Tsh. Milioni 700 mpaka kufikia Tsh. Bilioni 4.5. Hii ndio faida ambayo Watanzania tumeipata ya kuwa na kiongozi mwenye maono na mtazamo wa mbali zaidi, Rais Magufuli.

(iv) Ujenzi wa Stiegler’s Gorge

Utawala wa awamu ya kwanza uliokuwa ukiongozwa na Mwalimu Nyerere ulikuja na wazo wa kujenga Stiegler’s Gorge mnamo mwaka 1981 lakini umeshindwa kufanyika mpaka awamu hii ya 5 inayoongozwa na Rais Magufuli umeamua kufufua na kuliendeleza wazo hili. Mradi wa Stiegler’s Gorge kupitia Mto Rufiji utafanikiwa kuzalisha Megawattz 2100 utakapo kamilika. Ukamilifu wa mradi huu utajenga uhakika wa umeme nchini, utashusha bei ya umeme nchini na pia utamjengea Rais Magufuli heshima kubwa isiyofutika.

(v) Mapambano dhidi ya Rushwa na ufisadi nchini.

Rais Magufuli ameingia kwenye historia ya kiongozi ambaye Serikali anayoiongoza kuwa na mapambano ya dhahiri ya rushwa na ufisadi nchini. Tumeshuhudia Mafisadi Papa ambao walikuwa hawashikiki wala kukamatika wakipandishwa Mahakamani. Katika miaka ya nyuma ilikuwa suala gumu sana kwa Watuhumiwa “Mapapa” kuguswa tu, achilia mbali kupandishwa Mahakamani. Haya ni mapambano ya wazi wazi ya Serikali ya Rais Magufuli ya vita dhidi ya rushwa na ufisadi nchini. Leo hii Tanzania imepanda kwa nafasi 13 katika mwaka 2016 na 2017 na pia ikishika nafasi ya pili (2) kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

(vi) Uwazi wa taarifa na udhibiti wa rasilimali za nchi

Tumeshuhudia Serikali ikiweka uwazi kwenye mikataba na uchunguzi wa rasilimali za Taifa na kuweka makubaliano mapya yenye tija Mathalani tumeona uwazi wa sekta ya madini ya dhahabu, almas na Tanzanite ambapo Taifa tumeona namna ambavyo tulivyokuwa tukiibiwa na Serikali kuweka mikakati mipya ya kutokuibiwa tena. Kama haitoshi tumeshuhudia wawekezaji wakibanwa vilivyo juu ya mikataba isiyokuwa na tija kwa Taifa. Ni Serikali ya Rais Magufuli iliweka uthubutu wa kuwabana wawekezaji wa madini wa ACACIA iliyozaa matunda kwa Serikali ya Tanzania kumiliki asilimia 16 ya hisa katika makampuni ya uchimbaji wa madini, Serikali kupata gawio la faida ya madini ya asilimia 50 kwa 50. Yote haya yamewezekana kwa sababu ya uzalendo wake Rais Dk. Magufuli

(vii) Ujenzi wa Bomba la Mafuta

Serikali ya Rais Magufuli imefanikisha vilivyo kushirikiana na nchi ya Uganda kujenga Bomba la Mafuta linalotoka nchini Uganda mpaka Tanga nchini Tanzania. Ujenzi huo wa bomba la mafuta utazalisha ajira nchini na utaongeza pato la Taifa. Hayo yote yamefanikiwa kutokana na Serikali ya Rais Magufuli kuzidi kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na nchi nyinginezo.

Itaendelea …..

Shilatu E.J
0767488622
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: