Kaimu Kamishna wa Walipakodi Wakubwa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alfred Mregi akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kufungua Semina elekezi ya Msamaha wa Riba na Adhabu kwenye malimbikizo ya kodi kwa wafanyabiashara iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
 Kaimu Kamishna wa Walipakodi Wakubwa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Alfred Mregi akizungumza na wafanyabiashara wakati wa Semina elekezi ya Msamaha wa Riba na Adhabu kwenye malimbikizo ya kodi kwa wafanyabiashara iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
 Wafanyabiashara mbalimbali wakifuatilia kwa makini Semina elekezi ya Msamaha wa Riba na Adhabu kwenye malimbikizo ya kodi iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kutoa uelewa wa kutosha kwa wafanyabiasha hao ili waweze kuwasilisha maombi yao kwa usahihi kwa na kupatiwa msamaha huo. Semina hiyo imefanyika leo jijini Dar es Salaam.
Naibu Kamishina wa Kodi za Ndani Abdul Zuberi akizungumza na wafanyabiashara wakati wa Semina elekezi ya Msamaha wa Riba na Adhabu kwenye malimbikizo ya kodi kwa wafanyabiashara iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam. (PICHA ZOTE NA FRANCO MARWA - MAELEZO).

Na Veronica Kazimoto, Dar es Salaam.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imesema kuwa msamaha wa riba na adhabu wa asilimia 100 kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi unaotolewa ndani ya Mwaka wa Fedha 2018/19 utawasaidia wafanyabiashara kulipa kodi ya msingi na hatimaye kuwapa motisha ya kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati.

Hayo yamesemwa leo na Kaimu Kamishna wa Walipakodi Wakubwa wa mamlaka hiyo Alfred Mregi wakati akifungua semina elekezi ya msamaha wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya kodi kwa wafanyabiashara iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Mregi amesema kuwa dhumuni la semina hiyo elekezi ni kutoa uelewa wa kutosha kwa wafanyabiasha ili waweze kuwasilisha maombi yao kwa usahihi kwa lengo la kupatiwa msamaha huo.

"Leo tumekutana mahali hapa kwa lengo la kutoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu msamaha wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote wenye malimbikizo ya madeni wananufaika na msahamaha huo unatolewa kwa asilimia 100," alisema Mregi.

Naye Naibu Kamishina wa Kodi za Ndani Abdul Zuberi amesema suala la kodi halijachwa kwa TRA peke yake bali taasisi zote za Serikali zinafanya kazi hiyo ya kuhamasisha ulipaji kodi kwa maendeleo ya watanzania wote.

"Sasa hivi kodi za ndani zimezidi kuongezeka kutokana na uhamasishaji ambao unatoa motisha kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa letu," alieleza Zuberi.

Kwa upande wake Mfanyabiashara mkubwa kutoka kampuni ya Super Group of Companies inayozalisha sukari ya Mtibwa na Kagera Ibrahim Ali ameishukuru TRA kwa kutoa semina elekezi na kuongeza kuwa elimu waliyoipata imewasaidia kuelewa mambo mengi kuhusiana na msamaha huo.

Msamaha wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi unatokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli aliyoyatoa katika Mkutano wa Baraza la Wafanyabiashara (TNBC) uliofanyika Ikulu tarehe 20 Machi, 2018 ambapo wafanyabiashara walilalamikia kuwepo kwa malimbikizo makubwa ya madeni ya kodi za nyuma yakijumuisha riba na adhabu.

Kufuatia maelekezo hayo, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifanya marekebisho kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2018 na sehemu ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Mwaka 2015 ambapo katika marekebisho hayo, Waziri wa Fedha na Mipango amepewa mamlaka ya kutoa utaratibu maalum wa kumuwezesha Kamishna Mkuu wa TRA kutoa msamaha wa riba na adhabu wa hadi asilimia 100 kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi tofauti na asilimia 50 ya hapo awali.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: