Msajili wa mashirika yanayotoa msaada wa sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi Felistas Mushi akiongea wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka unaowakutanisha pamoja wakurugenzi na watendaji wa mashirika yanayotoa huduma za kisheria chini ya udhamini wa shirika lisilo la kiserikali la Legal Services Facility – LSF. Mkutano huo unaofanyika jijini Dodoma
 Meneja Mradi wa Legal Services Facility, Ramadhani Masele akitoa mada wakati mkutano wa mwaka uliowakutanisha pamoja wakurugenzi na watendaji wa mashirika yanayotoa huduma za kisheria kwa lengo la kupanga mikakati ya namna ya kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwapatia msaada wa kisheria.
Washiriki katika mkutano wa mwaka uliowakutanisha pamoja wakurugenzi na watendaji wa mashirika yanayotoa huduma za kisheria wakifatilia mkutano jijini Dodoma

Msajili wa mashirika yanayotoa msaada wa sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi Felistas Mushi akiwa katika picha ya pamoja na wakurugenzi na watendaji wa mashirika yanayotoa huduma za kisheria katika mkutano wa mwaka ulioandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Legal Services Facility – LSF jijini Dodoma.

Wadau kutoka Mashirika yanayotoa msaada wa kisheria wanakutana jijini Dodoma kujadili mikakati mbalimbali itayosaidia kuboresha utoaji wa huduma za msaada wa kisheria—lengo kuu likiwa ni kuwakwamua mamilioni ya watanzania wanaokabiliwa na matatizo mbalimbali ya kisheria.

Kongamano hilo linawakutanisha pamoja wakurugenzi na watendaji wa mashirika yanayotoa huduma za kisheria (Regional Mentors Organizations-RMOs) yanayotekeleza miradi ya utoaji wa huduma za kisheria inayofadhiliwa na Shirika la Legal Services Facility (LSF), kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana.

Akiongea wakati wa ufunguzi huo msajili wa mashirika yanayotoa msaada wa sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bi Felistas Mushi. aliwapongeza LSF kwa kusimamia mradi huo kwa takribani miaka 6 sasa na kuwawezesha wananchi hasa maskini kupata haki zao na kutumia fursa hiyo kuwahasa wananchi kuacha mila potofu zinazokandamiza haki za raia kwa ujumla

“Awali ya yote nipende kuwapongeza sana kwa kazi kubwa mnazozifanya katika kuhakikisha tunawawezesha wananchi kupata elimu juu ya maswala ya haki na sheria na kutatua migogoro mbalimbali. Mradi huu umekuwa tija kubwa kwa serikali na wizara kwa ujumla kwani umesaidia kutatua changamoto kubwa zinazowapata jamii husuani maskini zinazosababishwa na kutoelewa misingi ya haki za binadamu, mila potofu na nyingine nyingi”

Napenda kuwaahidi serikali itaendelea kufanya kazi nanyi kwa karibu katika kuboresha mifumo ya upatikanaji wa haki, kuimarisha sera zitakazochochea haki na usawa kwa wote hatimae kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake Meneja Mradi, Ramadhani Masele , kwa niaba ya mtendaji mkuu wa LSF alisema “Tunatarajia kuwa na mijadala kuhusiana na kazi zilizofanywa na wasaidizi wa kisheria na mashirika yanayotoa huduma za kisheria katika swala zima la utoaji wa huduma ya kisheria nchini,” mpaka sasa LSF imeshatoa zaidi ya shilingi billion 10 katika utekelezaji wa mradi huu

Mkutano huu, kwa mujibu wa Meneja Mradi wa LSF, utapitia na kutathimini viwango na ubora wa huduma za usaidizi wa kisheria zilizotolewa na wasaidizi wa kisheria na vituo vya usaidizi wa kisheria, matatizo yaliyowakabili, na jinsi ya kuyatatua –ili kuhakikisha huduma bora za msaada wa kisheria zinawafikiwa wahitaji wengi (wanawake na wanaume maskini), hasa wale waishio vijijini.

Takribani wasaidizi 5000 wameshapatiwa mafunzo chini ya miradi mbalimbali inayofadhiliwa na shirika la LSF. Wasaidizi hawa wanatoa msaada wa kisheria katika wilaya 158 nchi nzima, wakiwasaidia mamilioni ya watanzania maskini wanaokabiliwa na matatizo mbalimbali ya kisheria.

“Ni ukweli usiopingika kuwa wasaidizi wa kisheria wamefanya kazi kubwa, kuwakwamua watu wengi sana kutoka katika matatizo mbalimbali ya kisheria. Tunazo shuhuda na ripoti nyingi zinazothibitisha kazi hizi nzuri zilizofanywa na wasaidizi wa kisheri. Hata hivyo, pamoja na matokeo haya mazuri, lakini bado tunahitaji kuongeza nguvu zaidi na kuwasaidi wasaidizi hawa wa kisheria wafanye vizuri zaidi ya hii waliofanya. Ndio maana tumeitisha kongamano hili ili kujadili kwa pamoja namna ya kuboresha huduma za wasaidizi wa kisheria kuwafikia watu wengi zaidi, hasa hasa maeneo ya vijijini.

Jamii imeshauriwa kutumia watoa huduma wa msaada wa kisheria kila wilaya pindi wanapokumbwa na changamoto mbalimbali zinazopelekea uvunjwaji wa haki. Huduma hizi ni bure na zinapatikana kwa yeyote anayehitaji msaada.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: