Na Karama Kenyunko, blogu ya jamii.

Vijana 13 wanaodaiwa kutuma meseji kwa watu tofauti tofauti wamefikishwa katika mahakama ya hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matano likiwemo la utakatishaji wa fedha wa zaidi ya milioni 154.

Washtakiwa hao wameshtakiwa chini ya sheria ya uhujumu uchumi.

Wakisomewa mashtaka yao kwenye kesi hiyo namba 58 ya 2018 leo Agosti 7, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina, Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na shtaka la kula njama, kuchapisha taarifa za uongo, mashtaka mawili ya  kusambaza na shtaka moja la utakatishaji wa fedha.

Wakili, Kweka amewataja washtakiwa hao kuwa ni Boniface Maombe, David Luvanda, Moshi Sungura, Amos Bosco, Lule Kadenge, Jofrey Kapangamwaka, William Nturo, Regius Mauka, Collins Mwang'omolan Francis Kapalata, Kasonde Kapela, Enock Mwandaji na Pascal Kiatu.

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa serikali Mwandamizi Nasoro Katuga amedai kati ya Machi 6 na Juni 2018, washtakiwa hao walikula njama kwa kutuma meseji zisizotakiwa katika maeneo ya Dar es Salaam, Rukwa na sehemu zingine ndani ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia, washtakiwa hao wanadaiwa kuchapisha taarifa za uongo zikiwa katika muundo wa jumbe fupi (SMS), kupitia mfumo wa kompyuta kwa nia ya kudanganya.

Aidha washtakiwa hao wanadaiwa kusambaza Meseji za kielektroniki zisizotakiwa kupitia mfumo wa kompyuta.

Katuga ameendelea kudai kuwa, washtakiwa hao katika kipindi hicho cha Machi na Juni 2018 katika maeneo hayo kwa njia ya kudanganya na kushawishi, walisambaza jumbe fupi za kielektroniki kwenda kwa watu tofauti tofauti wakionesha kuwa wanayo mamlaka ya kufanya hivyo wakati si kweli.

Washtakiwa wote katika shtaka la tano wanadaiwa kati ya Machi na Juni 2018 mkoani Rukwa na katika maeneo ya Dar es Salaam na sehemu nyingine za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania washtakiwa hao moja kwa moja walijihusisha na muamala wa Sh 154,032, 830 huku wakijua fedha hizo ni zao la kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo wala kutoa dhamana hadi Mahakama Kuu kwa kuwa shtaka la utakatishaji wa fedha ni miongoni kwa mashtaka yasiyo na dhamana.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa kesi hiyo bado Haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Agosti 21, 2018 washtakiwa wamerudishwa rumande.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: