Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt.Kebwe Stephen Kebwe akiteta jambo na Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Mwantyala, ni baada ya kukabidhiwa cheti maalum juzi kwa jitihada za ujenzi wa taifa na miundombinu ya amani nchini.

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

WATANZANIA wametakiwa kutambua kuwa, wao ndiyo wenye jukumu kuu la kuhakikisha wanatumia nguvu, maarifa na rasilimali zao ili kulisaidia Taifa kusonga mbele katika nyanja mbalimbali.

Hayo yalibainishwa jana na Kiongozi Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Joshua Mwantyala muda mfupi baada ya kukabidhiwa cheti maalum na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro kutokana na jitihada ambazo amekuwa akizionyesha katika kusaidia na kuboresha makazi ya jeshi hilo.

"Naishukuru sana Serikali na Jeshi la Polisi kupitia Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt.Kebwe Stephen Kebwe kwa kutambua na kuthamini jitihada zangu za kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo ya Taifa letu la Tanzania.Nitaendelea kujitoa kwa maombi, hali na mali ili kuhakikisha Taifa letu linasonga mbele,"alisema Nabii Joshua.

Alisema, kila mmoja akiwa na shauku ya kulitumikia Taifa kwa moyo wa upendo, hakuna jambo ambalo litashindikana katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs), Dira ya Afrika 2063, Mpango Kazi wa Kuharakisha Maendeleo ya Viwanda Afrika (2008), Sera ya Viwanda ya Afrika Mashariki na mikakati ya utekelezaji wake.

Ukiwemo mwelekeo wa Maendeleo ya Viwanda wa SADC (2013 -2018) na Mkakati wa Maendeleo ya Viwanda wa SADC (2015-2063) na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Nabii Joshua alisema, hayo yote yatafikiwa kwa kila mmoja hapa nchini kushiriki kwa ufanisi mkubwa ili kuhakikisha Tanzania haiachwi nyuma katika jitihada za kutekeleza mipango mikakati yake kwa maslahi mapana ya Taifa.

"Nami nimeamua kwa kushirikiana na Watanzania wote ambao wapo katika Huduma ya Sauti ya Uponyaji na wengine wengi tutazidi kuliombea Taifa letu ili amani, mshikamano na upendo uliopo uweze kudumu. Pia tutazidi kujitoa kwa moyo katika kufanikisha huduma mbalimbali za kijamii ambazo zitatusaidia kufikia malengo haraka,"alisema Nabii Joshua.

Katika hatua nyingine, Nabii Joshua alimpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa jitihada zake na wasaidizi wake za kuwatumikia Watanzania bila kuchoka.

"Kazi wanayoifanya si ndogo, imekuwa na mwanga mzuri kwa Taifa letu, tumeona namna ambavyo Rais Magufuli anafanya kazi mchana na usiku ili kuhakikisha Taifa linasonga mbele, pia jitihada wanazofanya wasaidizi wake akiwemo Mkuu wa Jeshi la Polisi Simon Sirro, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Kabwe, Kamanda wa Jeshi la Polisi na wengine wengi zinatupa ngvu ya kuendelea kujitoa kwa moyo ili kuharakisha maendeleo ya Taifa letu,"alifafanua Nabii Joshua.

IGP Sirro imebainishwa ni miongoni mwa maofisa wa jeshi ambao wamekuwa na mbegu ya uzalendo, ambayo imekuwa ikitoa hamasa hata kwa wadau na wananchi mbalimbali kushiriki katika shughuli za maendeleo kwa jeshi hilo na hata kuendelea kutunza amani na usalama.

"IGP Siro amekuwa na nyota ya tofauti, kwa sababu asilimia kubwa ya nyumba zinazojengwa kwa ajili ya makazi ya askari zinajengwa kwa ushawishi wake kwa wananchi. Ni wazi kuwa, IGP Sirro ameimarika sana na amekuwa akitumia nafasi yake kujenga mahusiano mazuri.

"Uhusiano huo umekuwa ukiambukiza ile mbegu ya uzalendo kwa wananchi, hivyo kujitoa katika kusaidia Serikali ya Awamu ya Tano. Ninafurahi na ninampongeza Rais Dkt. Jonh Magufuli kwa sababu alituletea mtu sahihi kwa maslahi mapana ya Taifa," alisema Nabii Joshua.

Alisema, jitihada za IGP Sirro zimewezesha kufanikisha ujenzi wa makazi ya askari wa Jeshi la Polisi mjini Morogoro ambapo wadau mbalimbali akiwemo yeye wamefanikisha ujenzi wa nyumba hizo ili kuhakikisha askari ambao wamejitoa kwa ajili ya ulinzi na usalama familia zao zinaishi sehemu nzuri.

Katika hatua nyingine, Nabii Joshua aliwaasa Watanzania kuendelea kudumisha umoja, amani na mshikamano hatua ambayo itazidi kuwafanya viongozi waliopo madarakani kufanya kazi kwa ufanisi kwa ajili ya kuharakisha maendeleo.

"Tuzidi kudumisha amani, upendo na mshikamano ninaamini tukifanikiwa kufanya hivyo tutawezesha upatikanaji wa maendeleo ya haraka, hivyo kwa umoja wetu tuzidi kufanya kazi kwa bidii na kujitoa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.

"Ninaamini kwa kufanya hivyo, itakuwa rahisi kwa viongozi wetu kufanya kazi kwa ufanisi kwa ajili ya maendeleo yetu na taifa kwa ujumla," alisema Nabii Joshua.

Alisema, IGP Sirro ana msukumo binafsi ambao unamfanya kulipenda Jeshi la Polisi ndiyo maana hata Rais ametenga fungu kubwa kwa ajili ya kufanikisha maendeleo na miradi ya jeshi hilo hapa nchini.

Hata hivyo, tangu IGP Sirro achukue nafasi hiyo amekuwa akionyesha jitihda mbalimbali kwa kushirikiana na wasaidizi wake ambazo zimewezesha matukio mbalimbali ya uhalifu ikiwemo eneo la Kibiti mkoani Pwani kudhibitiwa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: