Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii.

Raia kumi wa Iran na watanzania wawili, leo Oktoba 30, 2017 wamepandishwa katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mshtaka matatu ya kukutwa na mchanganyiko wa dawa za kulevya za Heroin Bangi na Kuberi zenye uzito wa zaidi ya kilogram 110.

Hati ya Mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi imewataja raia hao wa Iran kuwa ni, Nabibakshsh Bibarde ,40, Mohammadhanif Dorzade, 23, Abdallah Sahib,21, Ubeidulla Abdi, Naim Ishaqa, Moslem Golmohamad, Rashid Badfar, Omary Ayoub, Abdulmajid Asqan na Tahir Mubarak.

Pia watanzania hao ni, Ally Abdallah Ally na Juma Amour Juma.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa imedaiwa kuwa, Oktoba 25 mwaka huu, huko katika Ukanda wa Bahari ya Hindi, upande wa Tanzania washtakiwa walisafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 111.02 aina ya Heroine.

Aidha, siku na mahali hapo hapo, washtakiwa hao walikutwa wakisafirisha gramu 235.78 za Bangi.

Katika shtaka la tatu, watuhumiwa hao wote kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha mchanganyiko wa dawa za kulevya aina ya Bangi na Kuberi zenye uzito wa kilo 3.34.

Hata hivyo, washtakiwa hao ambao walikuwa wakitafsiriwa kwa lugha ya Kiiran kutoka lugha ya kiswahili na mkalimani Meja Ndakeye (45) hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa, mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo ambayo kwa kawaida inasikilizwa mahakama kuu.

Pia Hakimu Nongwa alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kuwapatia washtakiwa hao dhamana sababu kiwango cha dawa wanazotuhumiwa kusafirisha imezidi kiwango ambacho mahakama hiyo inamlaka ya kutoa dhamana.

Kwa mujibu wa upande wa Mashtaka. upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika na washtakiwa wamepelekwa rumande hadi Novemba 13,mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: