Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Njombe, Gualbert Mbujilo (katikati) akipata maelezo ya vifaa vya ujifunzaji kutoka kwa mwalimu kwenye chumba cha darasa la kwanza ikionesha hali halisi ya darasa linalozungumza.Kushoto kwake ni Afisa Elimu Msingi Zegeli Shengelo.
Mwanafunzi Amilton Sanga kutoka shule ya Msingi Ramadhani akikabidhiwa kiasi cha shilingi 50,000/= mara baada ya kuibuka kidedea kwenye ngazi ya Halmashauri katika zoezi la Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Wanafunzi walioshiriki kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Usomaji Vitabu wakiwa wanasoma vitabu vya hadithi mbalimbali kwenye hafla hiyo.
Sehemu ya wazazi,waalimu na waratibu elimu walioshiriki kwenye kilele cha siku ya usomaji vitabu yaliyofanyika katika shule ya Msingi Mabatini Halmashauri ya Mji Njombe.

Hyasinta Kissima-Njombe.

Akizungumza wakati wa Kilele cha Maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Mabatini, Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Njombe Ndg. Gualbert Mbujilo aliwataka wazazi kuhakikisha kuwa wanaona umuhimu wa kununua vitabu kwa watoto wao kwani kupitia vitabu hivyo yapo mafundisho ambayo yamekua yakitolewa lakini sambamba na hilo vitabu vinamjengea mtoto uwezo wa kusoma kwa usahihi na kujiamini.

“Tumeona na tumesikia ni kwa jinsi gani mtoto aliyetusomea hadithi kwenye kitabu licha ya kuathiriwa na Lugha mama lakini amejitahidi kutamka maneno kwa ufasaha, anajiamini vya kutosha na ametuonesha vituo mbalimbali wakati wa kusoma.Hili ndilo Taifa tunalolijenga. Wazazi hakikisheni mnawanunulia watoto vitabu vya hadithi na vitabu vya kujifunzia na kuhakikisha tunatenga muda wa kutosha wa kuwa karibu na watoto wetu na kuwaelekeza”

Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri hiyo Zegeli Shengelo amesema kuwa kueleka kwenye uchumi wa viwanda kutakuwa na mahitaji makubwa sana ya wasomi hivyo ni vyema kufanya maandalizi mazuri kwa watoto wetu kwani msingi mzuri wa mtoto hujengwa kati ngazi za awali za elimu (shule za msingi) na pindi misingi hii inapojengwa vibaya mwendelezo wa mtoto unakua ni wakusuasua na mwisho wa siku mtoto anashindwa kuendelea na masomo kwani msingi wake haukujengwa imara tangu awali.

Aidha Shengelo amelishukuru shirika la watoto dunia UNICEF ambalo lilitoa mafunzo kwa waalimu katika shule ya Msingi Mabatini ambapo kupitia mafunzo hayo waalimu kwa kushirikiana na wanafunzi waliweza kutengeneza muonekano wa madarasa yanayoongea na kutengeneza zana mbalimbali za kujifunzia kwa kutumia rasilimali zinazopatikana katika maeneo yanayowazunguka.

“UNICEF imetusaidia sana kwani kupitia madarasa yanayoongea yamesaidia kuboresha mazingira ya watoto kujifunza kwani mtoto mwenyewe anaweza kujifunza pasipo mwalimu na madarasa haya yamekuwa yanawavutia wanafunzi wengi kupenda kusoma” Alisema Shengelo.

Hafla hiyo pia iliambatana na utoaji wa zawadi kwa Wanafunzi 04 waliofanya vizuri kwenye hatua za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK), pamoja na waalimu 04 washindi wa ufundishaji KKK katika ngazi ya Halmashauri ambapo waalimu walipata fedha taslimu zenye thamani ya shilingi laki moja (100,000/=) na wanafunzi walipewa zawadi ya shilingi elfu hamsini(50,000/=) ,mabegi, kalamu, daftari pamoja na vifaa mbalimbali vya kujifunzia.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: