Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza na wananchi wa kijiji cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo na Solwa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga -Picha na Marco Maduhu - Malunde1 bloG.
Mmoja wa wafanyabiashara wa uchenjuaji dhahabu Sultan Simon akimweleza Mkuu wa wilaya jinsi viongozi wa kijiji cha Nyaligongo wanavyofanya ubadhirifu wa fedha ambapo alisema mwezi uliopita amelipa Shilingi laki moja kwenye akaunti ya kijiji kupitia Benki ya NMB na hivyo akaeleza alisikitishwa na mwenyekiti wa kijiji kudai kuwa hajui kuna pesa kiasi gani kwenye akaunti ya kijiji
Mwananchi Simon Kayanda ,amewasilisha kero ya kutaka kusomewa Mapato na Matumizi na kuutuhumu uongozi wa kijiji kutafuna fedha na wakati kijijini hapo wana Plant 30 za kuchenjulia dhahabu na walikubaliana kila Plant ilipe shilingi 100,000 kila mwezi, pamoja na kodi zingine shilingi 50,000 , lakini kijiji hicho hakina maji, na barabara zake ni mbovu na hawajui pesa ambazo wanazitoa hupelekwa kwenye matumizi yapi.
Mtendaji wa Kijiji cha Nyaligongo Jeremiah Busangija, akijieleza kwa wananchi kuwa akaunti ya kijiji ina shilingi ngapi ambapo alijikanyaga na kudai hajui ,huku akijitetea kuwa mwezi Juni mwaka huu alisomea wananchi wake mapato na matumizi, na hali iliyomlazimu mkuu wa wilaya Josephine Matiro kuagiza uongozi mzima wa kijiji hicho uchunguzwe na mkaguzi wa fedha za ndani CAG pamoja na TAKURURU
Wananchi wa kijiji cha Nyaligongo kata ya Mwakitolyo wakiwa kwenye mkutano wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akitatua kero zao.
---
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro amefanya ziara ya kusikiliza na kuzitatua kero za wananchi katika kijiji cha Nyaligongo Kata ya Mwakitolyo na Solwa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga (Shinyanga vijijini).

Mbali na kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi mkuu huyo wa wilaya alizindua zoezi la upandaji miti katika shule ya msingi Manigana iliyopo katika kata ya Solwa kwa kupanda miti ya259 mihare , pamoja na kuzindua ujenzi wa bomba la maji kutoka Ziwa Victoria katika kijiji cha Mwakatola kata ya Solwa.

Ziara ya mkuu huyo wa wilaya iliyofanyika Novemba 8,2017 ilianzia kijiji cha Nyaligongo ambapo alipokea kero mbalimbali zikiwemo za afya ,elimu,ulinzi pamoja na kero kubwa ya wananchi ya kutosomewa mapato na matumizi ambayo ilizua mtafaruku mkubwa kwa wananchi kuwakataa viongozi wao wa kijiji na kutaka waondoke na mkuu wa wilaya wakidai viongozi hao hawafai.

Asilimia kubwa ya wananchi waliohudhuria mkutano huo walikuwa wakiliuliza swali la kutosomewa mapato na matumizi na kudai kuwa viongozi wa kijiji hicho wamekuwa wakizitafuna fedha wanazolipa ushuru na kutofika sehemu husika na hivyo kukwamisha upatikanaji wa maendeleo kwenye kijiji hicho.

Mmoja wa wananchi hao Abdul Saidi alisema kero kubwa ambayo imekuwa ikisumbua kwenye kijiji hicho ni kutosomewa mapato na matumizi kwa muda wa miaka minne sasa, huku viongozi wao wakiendelea kutoza ushuru lakini hawasomi mapato na matumizi na kutokujua akaunti yao ya kijiji mpaka sasa ina shilingi ngapi.

"Mkuu wa wilaya leo tunaomba uondoke na viongozi wote hawa wa kijiji kwa sababu hatuna faida nao ni kikwazo cha maendeleo yetu wanatafuna tu fedha",alisema Said.

Naye Simoni Kayanda alisema kwenye kijiji hicho kuna plant 30 za kuchenjulia dhahabu na walikubaliana kila mwezi kulipa shilingi 100,000/= kwa kila Plant kupitia akaunti ya kijiji lakini maendeleo kwenye kijiji hakuna na wala kujua akaunti hiyo inafedha kiasi gani.

Hata hivyo Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Jeremiah Busangija aliposimamishwa na mkuu wa wilaya Josephine Matiro kujibu tuhuma hizo za kutosoma mapato na matumizi alianza kujikanyaga na kutokutoa majibu sahihi wala kutokujua akaunti hiyo ya kijiji ina fedha kiasi gani hali iliyozua taharuki kwenye mkutano huo.

Aidha kufuatia sintofahamu hiyo ilimlazimu mkuu wa wilaya kumuagiza mkurugenzi wa halmashauri hiyo ya Shinyanga Bakari Mosinyo kumpeleka mkaguzi wa hesabu wa ndani CAG ili kubaini kama kuna ubadhirifu wa fedha kwenye kijiji hicho ili viongozi hao waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Mkuu huyo wa wilaya aliwaeleza wananchi hao kuwa kwa sasa hawezi kuwawajibisha viongozi hao wala kuondoka nao kwani anataka kwanza ajiridhishe kisheria ndipo ajue wapi pa kuanzia.

Matiro alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wote serikali za mitaa wawe na tabia ya kusomea wananchi wao mapato na matumizi kila baada ya miezi mitatu, ili kuondoa manung'uniko ya wananchi kuwa huenda fedha zao ambazo huchanga za maendeleo kuwa zimeshatafuna na wachache.

"Principle ya maendeleo sehemu yoyote ile lazima viongozi wake wawe wawazi,naomba viongozi kuwa wawazi kwani msipokuwa wawazi wananchi hawa hawawezi kuwaelewa,kama tutabaini kuwa kuna ubadhirifu wa fedha lazima wahusika wachukuliwe hatua za kisheria",alisema Matiro.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya aliagiza Mamlaka ya Uzalishaji na Usambazaji Maji kutoka mradi wa ziwa Victoria KASHWASA ,kumaliza tatizo la maji katika kijiji cha Mahembe ndani ya wiki mbili ili kuwaondolea adha wananchi hao ya kutafuta maji umbali mrefu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: