Hakuna siku niliyojisikia vibaya kama siku moja nipo nyumbani, kama kawaida yangu nilikua nime lewa chakari, nimejilaza kwenye kochi. Hapo ni baada ya kumtukana mke wangu na kuwaambia wote waende jikoni.

Ilikua ni usiku, lakini baada ya muda njaa ilinibana, nilinyanyuka kwa kuyumbayumba kwenda jikoni ili kudai chakula ambacho mke wangu amepika nikiwa hata sijui pesa katolea wapi kwani asubuhi sikuacha chochote.

Baada ya kufika mlangoni nikiwa kabla sijaupiga teke kama kawaida yangu nilisikia sauti ya mtoto wangu wa miaka minne akimuuliza Mama yake. “Mama eti na sisi Baba yetu anakufa lini?”

Nilistuka, nikasimama na kuanza kusikilzia walikua wanazungumza nini. “Wewe mtoto nyamaza usiseme hivyo ni vibaya, tema mate chini!” Mke wangu alimkemea lakini mtoto hakujali.

“Sasa Mama mbona Dadada amesema Baba yake Juma amekufa, ameenda kwa Mungu na hatarudi tena, kwanini na sisi Baba yetu asiende ili tubaki wenyewe…”

Mtoto aliendelea kuongea, mke wangu alijaribu kumkanya lakini hakusikia aliendelea. Mtoto mwingine mkubwa binti yangu wa miaka kumi yeye alimkatisha kumuelewesha.

“Baba Juma anaenda kwa Mungu kwasababu ni mtu mzuri, Baba yeye hataenda kwa Mungu anaenda kwa shetani, haendi mbinguni….” Alimaliza kumuelewesha mdogo wake, mke wangu alichanganyikiwa zaidi, alijaribu kuwakanya lakini yule mdogo aliendelea…

“Heri Baba hata afe, maana anakupiga wewe kila siku ana sisi kutupiga. Mimi ningekua Rambo ningemuua paaap! Paaa! Pigo moja tu anakufa! Nikiwa mkubwa namuulia mbali” Alionge akwa kujigamba.

Mtoto aliendelea kuongea sasa kwa msisimko. Nilijikuta nasimama wima, pombe zote ziliniishia njaa ilikoma, nilianza kutembea kurudi sebuleni, nilishindwa hata kukaa. Niliingia chumbani na kuanza kujiangalia kwenye kioo.

Nimeyafanya nini maisha yangu. niliwaza nikikumbuka zamani nilivyokua nikitamani kuwa na familia nzuri, kua na mke mzuri na watoto ambao wananipenda.

Lakini sasa mtoto wangu mwenywe, mtoto wa miaka minne alikua anatamani mimi Baba yake kufa! Nilitamani kulia lakini nilijua haitasiadia, niliingia bafuni na kuanza kujitapisha, nilitapika pombe yote, nikaingia kwenye friji nikachukua bia zote na wine.

Nikaenda kuzimwaga kisha nikarudi jikoni, nikafungua mlango kistaarabu nikaumbaia mke wangu sasa nimecha pombe, naomba mnisamehe lakini sasa nimemaua kubadiliaka.

Tangu siku hiyo sijawahi kunywa pombe, kumpiga wala kumtukana mke wangu, nina amani na furaha kuliko kipindi chote. Kumbe manyanyaso niliyokua nikimpa mke wangu yalikua yakiniumiza mimi zaidi kuliko mke wangu.

***MWISHO***

Kamwe hakuna furaha ya peke yako, huwezi kufurahi ukiwa mwenyewe, starehe ya peke yako ni starehe ya upweke. Mwanaume unahitaji familia ili uweze kusema unafuraha.

Kama familia yako inalia, mkeo analia basi jua huna furaha. Pia haikufanyi mwanaume kamili, haikufanyi mwanaume zaidi kuwatesa wanao au mke wako, inakufanya mwanaume mpumbavu tu!

Kama wewe ni baba jiulize je kwa unayotenda ipo siku mwanao atayasema haya?

TAFAKARI CHUKUA HATUA.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: