Mshauri wa msuala ya Maji na Mazingira kutoka Shirika la Maendeleo la Ujerumani ‘GIZ’, Tina Eisele akielezea kuhusu mradi wa huduma ya maji na usafi wa mazingira katika maeneo ya wananchi wenye kipato cha chini unaotekelezwa na shirika hilo katika kata ya Ndala na Masekeleo katika manispaa ya Shinyanga kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Shinyanga (SHUWASA). Picha na Kadama Malunde - Malunde1 blog.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiwasisitiza wadau wa maji na mazingira kuhakikisha wanaungana katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi katika kupata huduma za maji safi na mazingira.
Washiriki wa warsha hiyo wakiwa ukumbini. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa SHUWASA ,Injinia Syliveter Mahole akifuatiwa na Erik Norremarle kutoka GFA.
Washiriki wa warsha hiyo wakifuatilia mada ukumbini.
Mwezeshaji katika warsha hiyo, Injinia Mutaekulwa Mutegeki akizungumza ukumbini.
Washiriki wa warsha wakiwa ukumbini.
Washiriki wa warsha wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea ukumbini.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro amefungua warsha ya wadau wa maji na mazingira katika manispaa ya Shinyanga iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani ‘GIZ’ kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Shinyanga (SHUWASA).

Lengo la warsha hiyo ni kuboresha huduma ya maji safi na usafi wa mazingira kwenye kata ya Ndala na Masekelo katika manispaa ya Shinyanga kupitia mradi wa huduma ya maji na usafi wa mazingira katika maeneo ya wananchi wenye kipato cha chini unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani ‘GIZ’ kwa kushirikiana na SHUWASA.

Akifungua warsha hiyo ya siku mbili inayofanyika katika ukumbi wa Karena Hotel Mjini Shinyanga ambayo imekutanisha wataalamu wa maji na mazingira na viongozi kuanzia ngazi ya mtaa hadi mkoa,Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro alisema mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wenye kipato cha chini.

Matiro alilishukuru shirika la GIZ kwa kushirikiana na SHUWASA kuanzisha mikakati ya kushughulikia changamoto za maji na mazingira katika kata ya Ndala na Masekelo wakishirikiana na wadau mbalimbali.

Alisema lengo la serikali ni kusimamia sera za nchi ili kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi na kwamba ipo tayari kushirikiana na wadau wote katika kukabiliana na changamoto zote zinazojitokeza.

“Mimi kama kiongozi mkuu wa wilaya hii,natoa shukrani za dhati kwa shrike la ‘GIZ’ kwa kuchagua mji wa Shinyanga kuwa moja ya miji mitatu nchini iliyopangwa kutekeleza mradi huu ikiwemo miji ya Korogwe na Dodoma,nawasihi kusimamia kikamilifu mradi huu ili uweze kunufaisha wananchi na pale mnapokwama msisite kuwasiliana na serikali”, alisema Matiro.

Naye Mshauri wa masuala ya Maji na Mazingira kutoka Shirika la Maendeleo la Ujerumani ‘GIZ’, Tina Eisele aliishukuru serikali ya Tanzania kwa kuwaruhusu kutekeleza mradi huo ambao unatekelezwa katika maeneo ambako kuna wananchi wenye kipato cha chini.

Eisele alisema takwimu zinaonesha kuwa katika maeneo ambayo kuna wananchi wenye kipato duni,huduma za maji safi na usafi wa mazingira pia ni duni ndiyo maana wameamua kuanzisha mradi huo ambao utawalenga watu wenye kipato duni.

“Kupata maji safi na kuwa katika mazingira bora ni haki ya binadamu,tunataka maeneo yenye wananchi wenye kipato duni waangaliwe kwa jicho kama lile linalotumika kuangalia wananchi wenye kipato kikubwa,na hii ni miongoni mwa makubaliano ya mikataba mbalimbali ya kimataifa”,aliongeza Eisele.

Mkurugenzi wa SHUWASA, Injinia Sylivester Mahole alisema tayari mradi huo umeanza kutekelezwa huku akibainisha kuwa mradi huo utawanufaisha wananchi ambao walikuwa hawajafikiwa na huduma ya maji.

“Miongoni mwa changamoto katika utoaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira ni huduma kutowafikia wananchi wote na hivyo kusababisha makundi ya waliofikiwa na huduma na wasiofikiwa na huduma”,alieleza Injinia Mahole.

“Katika maeneo yanayotakiwa kupewa huduma kuna maeneo yanakaliwa na wananchi wenye kipato cha chini na hivyo kutokuwa na uwezo wa kuunganisha huduma za maji safi na usafi wa mazingira majumbani mwao,hivyo kwa kushirikiana na shirika la GIZ tumeamua kukabiliana na changamoto hii”,aliongeza Injinia Mahole.

Naye Mwezeshaji katika warsha hiyo,Injinia Mutaekulwa Mutegeki alisema kata za Ndala na Masekelo zitatumika kama mfano wa utekelezaji wa mradi huo ambapo pamoja na mambo mengine vituo vya kuchotea maji “Magati” vitajengwa kwenye maeneo hayo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: