Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (aliyesimama mbele), akiongea na wafanyakazi wa Mamlaka hiyo katika mkutano uliofanyika jana kwenye ukumbi wa Transit uliopo kwenye jengo la kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kutoka Makao Makuu na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), jana wakimsikiliza Kaimu Mkurugenzi Mkuu (hayupo pichani) aliyekuwa akiongelea mikakati na masuala mbalimbali yanayohusiana na maendeleo ya taasisi hiyo.
Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Lawrence Thobias (aliyesimama mbele), akizungumza na Wafanyakazi katika mkutano uliofanyika jana kwenye ukumbi wa Transit uliopo kwenye jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).

Na Mwandishi Wetu

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), imesema itahakikisha inapata hati za viwanja vyake vya ndege ili kupunguza uvamizi kutoka kwa wananchi.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela alitoa kauli hiyo jana kwenye mkutano na wafanyakazi uliofanyika katika ukumbi ya Transit uliopo jengo la Kwanza la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI), ikiwa ni moja ya mikakati ya mamlaka hadi kufikia Juni 2018.

Bw. Mayongela alisema tayari wameanza taratibu za kupata hati miliki kwa viwanja 13, vikiwemo vya JNIA na Mwanza zilizofutwa awali.

Hata hivyo, Wananchi wamekuwa na tabia za kuvamia maeneo ya viwanja vya ndege kwa kufanya makazi na mashamba, jambo ambalo ni hatarishi kiusalama.

Bw. Mayongela alisema mkakati mwingine ni kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuimarisha ulinzi kwenye maeneo ya viwanja vya ndege 58 vinavyomilikiwa na serikali na ambavyo havipo chini ya serikali.

“Pia tutaanda kikosi kazi kitachosaidiana na wenzetu wa TANROADS katika usimamizi na uangalizi wa viwanja vya ndege vinavyoendelea kujengwa maeneo mbalimbali nchini,” alisema Bw. Mayongela.

Katika hatua nyingine Bw. Mayongela alisema pia mamlaka inampango wa kuendeleza miundombinu mbalimbali yakiwemo majengo ya abiria, Mizigo, ufungaji wa taa za kuongezea ndege na ufungaji kamera za usalama (CCTV) kwenye viwanja vya Arusha, Mwanza, JNIA na Dodoma.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Lawrence Thobias aliwataka wafanyakazi kufanya kazi kwa uweledi na uwazi, ili kufikia malengo yaliyowekwa na hatakuwa tayari kumfukuza mtumishi kazi kwa masuala yasiyokuwa na msingi.

“Ninafungua milango kwa wafanyakazi mje ofisini kwangu kwani hii ni ofisi ya rasilimali watu na sio rasilimali mtu, naweka milango wazi mje tujadili masuala ya kazi ya kujenga na sio majungu,” alisisitiza Bw. Thobias.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: