Kaimu Mkurugenzi wa Tigo kanda ya kaskazini, Henry Kinabo(kulia) akizungumza na waandishi wa habari jana namna ya kujisajili mbio za Dodoma Marathon zitakazotimua vumbi jumapili ya tarehe 12 mwezi huu, ambapo utaweza kujisajili kwa Tigopesa kwa namba 0674 444 444 kwa punguzo la asilimia 10%. Pembeni ni Meneja wa Maendeleo wa Vision Sports, Raymond Mchani.

Watakaojisajili kupitia Tigo Pesa kupata asilimia 10% punguzo la bei.

Dodoma. Kampuni inayoongoza kwa mageuzi ya kidigitali, Tigo Tanzania wakiungana na Vision Sports wametangaza kuanza kwa usajili wa washiriki katika mbio za Dodoma Marathon. Mji wa Dodoma utageuzwa kuwa kitivo cha mazoezi na furaha kwa familia nzima tarehe 12 Novemba wakati shindano hilo litakapohitimishwa.

Usajili kwa Dar es Salaam unafanyika katika vituo maalum vya Duka la Tigo Shop lililopo Mlimani City, Duka la Simply Elegant lililopo Dar Free Market, Ghorofa ya Chini ya Kibo Complex eneo la Tegeta na Duka la Imalaseko SuperMarket lilipo eneo la Posta katikati ya jiji. Kwa Dodoma, usajili unafanyika katika eneo la Dodoma Hotel, Carnival, Cape Town Complex iliyopo Kisasa na Duka la Tigo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

‘Wale watakaojisajili kwa njia ya Tigo Pesa watapata punguzo la bei la asilimia 10%. Wanaweza kufanya hivyo kwa kutuma kiasi cha shilingi 13,500/- kutoka kwenye simu zao za mkononi kwenda namba ya Tigo Pesa 0674 444 444. Hapo hapo watapokea ujumbe utakaowataarifu kujisajili na eneo ambalo wanafaa kwenda kuchukua vielelezo vyao vya usajili,’ Meneja wa Tigo, Kanda ya Kaskazini, Henry Kinabo alisema.

Kwa upande wake,Meneja wa maendeleo wa Vision Sports, Raymond Mchani kwa niaba ya Ally Nchahaga, Mkurugenzi Mtendaji wa Vision Sports aliwashauri washiriki kusoma vigezo na masharti ya ushiriki pamoja na taarifa nyingine muhimu kutoka kwenye tovuti ya Dodoma Marathon na katika vituo vya usajili. ‘Pia ni muhimu kwa washiriki kuhudhuria kikao cha maelezo kuhusu ushiriki na usalama wa washiriki kitakachofanyika kabla ya mbio kuanza saa kumi na mbili asubuhi, pale katika Uwanja wa Jamhuri, mjini Dodoma.

Tigo inathamini mbio za kilometa 21 za Tigo Dodoma Half Marathon. Dodoma Marathon pia itahusisha mbio ndefu za kilometa 42, mashindano ya kilometa 10 pamoja na yale ya kilometa 5 yatakayohusu wanafamilia na jamii yote kwa ujumla. Zawadi murwa zitatolewa kwa washiriki ikiwemo vyeti vya ushiriki, medali na zawadi za fedha kwa washindi wa mbio zote. Wanariadha mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki katika mbio hizo.

“Tuna furaha kubwa kudhamini shindano hili ambalo linahamasisha watu kuzingatia afya bora kwa kushiriki katika michezo, na pia kuinua vipaji katika michezo,” Henry Kinabo, Meneja wa Tigo Kanda ya Kaskazini alisema.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: