Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo (Disemba 5, 2017) imetangaza orodha yenye wanafunzi 2,679 ambao wamepata mikopo ya elimu ya juu yenye thamani ya TZS 9.6 bilioni kufuatia kukamilika kwa uchambuzi wa rufaa zilizowasilishwa na wanafunzi hao.

Kati ya wanafunzi hao, 1,847 ni wa mwaka wa kwanza ambao mikopo yao ina thamani ya TZS 6.84 bilioni na wengine 832 ni wale wanaoendelea na masomo lakini hawakuwa na mikopo katika miaka iliyopita. Wanafunzi hao wanaoendelea na masomo wamepata mikopo yenye thamani ya TZS 2.76 bilioni.

Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru amesema orodha ya wanafunzi hao na fedha zao zimetumwa katika vyuo walipo wanafunzi hao hivi sasa.

“Hatua hii inafanya jumla ya wanafunzi 33,200 wa mwaka wa kwanza kuwa wamepangiwa mikopo yenye thamani ya zaidi ya TZS 108 bilioni kwa mwaka wa masomo 2017/2018 hadi sasa,” amesema Badru na kufafanua kuwa Serikali imetenga jumla ya TZS 427.54 bilioni kwa ajili ya mikopo hiyo kwa mwaka 2017/2018.

HESLB ilifungua dirisha la rufaa kwa siku saba kuanzia tarehe 13 Novemba, 2017 hadi tarehe 19 Novemba, 2017 ili kuwapa fursa waombaji wote ambao hawakuwa wameridhika na upangaji wa mikopo na kuwasilisha rufaa kupitia vyuo walivyopata udahili.

Wanafunzi waliohamishiwa mikopo yao

Wakati huohuo, Badru amesema HESLB imeanza kuhamisha mikopo iliyokuwa imeelekezwa katika vyuo tofauti na waliko kwa sasa. Mikopo ya wanafunzi 590 wa mwaka wa kwanza yenye thamani ya TZS 1.78 bilioni ambayo awali ilikuwa imepelekwa katika vyuo tofauti na walipo wanafunzi imehamishwa.

“Wanafunzi hao waliohamishiwa mikopo yao ni wale ambao walipangiwa mikopo na kupelekewa fedha zao katika vyuo ambavyo walipata udahili awali, ila baadaye wakaamua kujiunga na vyuo vingine ambavyo nako walipata udahili,” amesema na kuongeza kuwa orodha kamili ya wanafunzi hao pamoja na fedha za wanafunzi hao zimetumwa katika vyuo walipo hivi sasa.

Bodi ya Mikopo inaendelea kupokea orodha za wanafunzi waliosajiliwa katika vyuo mbalimbali na wale wenye mikopo, fedha zao zitahamishiwa katika vyuo walipo katika awamu zijazo.

Mikopo kwa Wahadhiri wa Vyuo Vikuu

Katika hatua nyingine, Bodi ya Mikopo imesema jumla ya wanafunzi 45 wa shahada za uzamili na uzamivu ambao ni wanataaluma na waajiriwa wa vyuo mbalimbali nchini wamepata mikopo yenye thamani ya TZS 441.4 milioni katika mwaka wa masomo 2017/2018.

Badru amesema leo kuwa mikopo hiyo hutolewa na HESLB kwa wanataaluma hao ili kuvijengea vyuo uwezo wa kitaaluma chini ya makubaliano kati ya Bodi ya Mikopo na vyuo hivyo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: