Kamishna wa Kodi za Ndani, Elijah Mwandumbya akizungumza na waandishi habari juu ya usajili wa wafanyabiashara wadogo katika kituo cha Chanika jijini Dar es Salaam.
Mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Regina Urio (kulia) akimhudumia mfanyabiashara (kushoto) aliyefika katika kituo maalum kilichoteuliwa na mamlaka hiyo kilichopo Chanika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kusajili na kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).

Na Mwandishi Wetu.

Wafanyabiashara wanaostahili kulipa kodi kwa njia ya makadirio, watalipa robo ya kwanza ndani ya siku tisini (90) kuanzia siku waliyosajiliwa tofauti na utaratibu uliokuwepo wa kulipa kodi hiyo kabla mfanyabishara hajaanza kufanya biashara husika.

Hayo yamesema leo na Kamishna wa Kodi za Ndani Elijah Mwandumbya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) alipotembelea kituo maalum kilichoteuliwa na mamlaka hiyo kilichopo Chanika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kampeni ya usajili wa walipakodi.

Kamishna Mwandumbya amesema kuwa, hapo awali wafanyabiashara walitakiwa kulipa robo mwaka ya kwanza mara baada ya kusajili na kupata Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi (TIN) suala lililosababisha baadhi ya watu kushindwa kulipa kutokana na msingi mdogo wa biashara zao.

"Niseme tu kwamba, TRA tumeamua kuboresha huduma zetu kwa kuhakikisha kuwa, walipakodi wapya wanalipa makadirio yao ndani ya miezi mitatu tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo mfanyabiashara alitakiwa kulipa kabla ya kuanza biashara yake", alisema Mwandumbya.

Naye Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa mamlaka hiyo Richard Kayombo, amewataka wananchi wanaoishi maeneo hayo kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kujiandikisha na kusema kuwa, zoezi hilo katika kituo hicho litadumu kwa muda wa wiki moja.

"Tukitoka Manispaa ya Ilala tutaelekea Temeke na baadaye tutaendelea kufungua vituo katika maeneo mbalimbali na wakati huo huo ofisi zetu zinaendelea na kazi hii ya usajili kama kawaida" alisema Kayombo.

Mamlaka ya Mapato Tanzania inafanya kampeni ya usajili wa walipakodi nchi nzima kwa lengo la kuongeza idadi ya walipakodi, kupanua wigo wa ulipaji kodi na kuongeza mapato ya Serikali.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: