Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya kazi, Mhe. William Lukuvi akionyesha muonekano wa Hati ya Kielektroniki inavyotarajiwa kuwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwl. Nyerere; Mzee Joseph Butiku alipofika ofisini kwake leo, katika kanda ya ofisi ya Ardhi - Dar es Salaam.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya kazi, Mhe. William Lukuvi akionyesha moja ya ramani za Mipango Miji kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwl. Nyerere, Mzee Joseph Butiku alipofika ofisini kwake leo, katika kanda ya ofisi ya Ardhi - Dar es Salaam
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya kazi, Mhe. William Lukuvi akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwl. Nyerere, Mzee Joseph Butiku na msaidizi wake walipofika ofisini kwake leo, katika kanda ya ofisi ya Ardhi - Dar es Salaam.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya kazi, Mhe. William Lukuvi ametaja maboresho kadhaa yaliyofanyika katika Wizara ya Ardhi.

Mhe. Lukuvi aliyasema hayo alipokutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwl. Nyerere, Mzee Joseph Butiku alipofika ofisini kwake leo, katika kanda ya ofisi ya Ardhi - Dar es Salaam.

Akieleza Maendeleo yanayofanyika sasa katika eneo la Urasimishaji; Mhe Lukuvi alieleza kuwa zoezi la Urasimishaji sasa linaendelea kwa kasi, na kutolea mfano wa Jiji la Mwanza kuwa zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa. Alisema; “Mpaka sasa viwanja 35,000 vimeshapimwa na Hati 12,000 kutolewa katika wilaya za Ilemela na Nyamagana.

Mhe. Lukuvi alisema baadhi ya maeneo mengine ambayo yamefanya zoezi la Urasimishaji kwa kiwango cha kuridhisha ni pamoja na Kimara na Makongo ambapo Wananchi wenyewe wamekuwa wahusika wakuu katika kuhakikisha kuwa wamezingatia miongozo waliopewa na Wizara kufanikisha zoezi hilo, ikiwepo kuzingatia kuainisha miundombinu muhimu kama njia za barabara, maji , umeme n.k.

Akiendelea kufafanua jinsi eneo la Upimaji wa viwanja lilivyoboreshwa. Mhe. Waziri ameeleza kuwa sasa kuna kampuni 48 za upimaji ambazo zimesajiliwa na kuidhinishwa na Wizara, na zinazoendelea sasa na kufanya upimaji wa viwanja katika maeneo mbalimbali nchini.

Aidha, Mhe . Lukuvi ameeleza kuwa katika maeneo ya Vijijini pia kasi ya upangaji wa Matumizi bora ya Ardhi imekuwa ya kuridhisha, tofauti na miaka ya zamani. Hatahivyo alieleza kuwa changamoto zipo, hususani katika mkoa wa Morogoro; katika maeneo ya Mvomero, Kilombero na mengineyo lakini Serikali inaendelea na jitihada za kufanya taratibu za upangaji wa Matumizi bora ya Ardhi na kufanya upimaji wa maeneo kwa kasi kubwa zaidi katika maeneo hayo.

Vile vile Mhe. Lukuvi amesema katika kuboresha ulinzi wa Hati za Ardhi; Hati sasa zipo katika taratibu za kuandaliwa na kutolewa Kielektroniki. Alisema, Hati hizo za Kielektroniki zitathibiti mianya yote ya ulaghai na rushwa, matendo ambayo yamekuwa yakifanywa kwa muda mrefu na matapeli mbalimbali na kusababisha vilio kwa Wananchi wengi. Pia kwa Mfumo huo wa Kielektroniki kila Mmiliki wa Ardhi, atalazimika kuwajibika ipasavyo katika kulipa Kodi ya Pango la Ardhi.

Naye Mzee Butiku amempongeza Mhe. Lukuvi katika juhudi zake za kuendelea kuboresha huduma zinazofanywa na Wizara hiyo na kumsihi kuendelea na jitihada hizo. Alisema; “Nikilinganisha hali iliyokuwepo Wizarani nyakati za nyuma na sasa, maboresho ni makubwa, endelea na juhudi unazozifanya”.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: