OPERESHENI ya nchi nzima kuwabaini waajiri ambao hawatekelezi sheria ya ajira na mahusiano kazini na wale ambao bado hawajajisajili na Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, (WCF), inayoongozwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Anthony Mavunde, imeingia Mkoani Morogoro leo Machi 9, 2018, ambapo waajiri 254 wamechukuliwa hatua mbalimbali za kisheria ikiwa ni pamoja na kutozwa faini.

Akiwa Mkoani Morogoro Mh Mavunde ametoa wito kwa Waajiri nchi nzima kuajiri Maafisa Rasilimali Watu wenye sifa na taaluma husika kuliko hivi sasa ambapo waajiri wengi wanawatumia watu wasio na sifa kufanya kazi za Afisa Rasilimali watu na hivyo kushindwa kutafsiri vyema Sheria mbalimbali za kazi hali inayopelekea kutoa ushauri ambao unaleta athari kwa Mwajiri.
 Mavunde ameendelea kusisitiza kwamba wapo Vijana wengi mtaani wahitimu wa Vyuo ambao wana sifa za kufanya kazi hizo kwa weledi mkubwa hivyo waajiri wawape nafasi tofauti na wanavyofanya sasa kuajiri watu wasio na sifa.

Mavunde ambaye leo amefanya ukaguzi katika Kampuni ya Ulinzi ya Sengo Security,Hotel ya Midland,Kampuni ya Usafirishaji ya HOOD na Kiwanda cha Tumbaku cha ALLIANCE ONE ametoa maelekezo ya Jumla kwa kuwataka Waajiri kutoa mikataba ya Ajira inayokidhi Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6/2004, Kuwataka Waajiri kuzingatia masuala ya AFYA na USALAMA mahali pa kazi kama yalivyoanishwa katika Sheria ya Afya na Usalama mahala pa kazi Na.5/2003 na kuagiza zaidi ya Waajiri 200 kufikishwa Mahakamani kwa kushindwa kujiunga na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.
Aidha Kamishna wa Kazi, Bi. Hilda Kabisa, amesema, Waajiri ni sharti watoe mikataba kwa wafanyakazi inayoonyesha ni muda gani wa kufanya kazi, likizo kwa mfanyakazi, na hata kama mfanyakazi analipwa kwa siku ni sharti mambo hayo yazingatiwe.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi, (WCF), Bi. Rehema Kabongo, amesema Mfuko umjiandaa kabisa, na maagizo ya Mheshimiwa Naibu Waziri yatatekelezwa haraka na tayari baadhi ya maeneo hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa dhidi ya waajiri ambao wameshindwa kutekeleza takwa la kisheria.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: