Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akifungua mafunzo ya TEHAMA kwa waalimu wa shule za sekondari za umma (hawapo pichani) kwenye ukumbi wa Chuo cha Kompyuta ya Sayansi, Habari na Mawasiliano, Chuo Kikuu cha Dodoma.
Mwakilishi wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Bi. Justina Mashiba akisisitiza jambo kwa waalimu wa shule za sekondari za umma (hawapo pichani) kabla ya ufunguzi wa mafunzo ya TEHAMA kwao mbele ya mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani) kwenye ukumbi wa Chuo cha Kompyuta ya Sayansi, Habari na Mawasiliano, Chuo Kikuu cha Dodoma.
Wakufunzi wa mafunzo ya TEHAMA kwa waalimu wa shule za sekondari za umma kutoka Chuo cha Kompyuta ya Sayansi, Habari na Mawasiliano wa Chuo Kikuu cha Dodoma wakitambulishwa kwa mgeni rasmi wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani), chuoni hapo.
Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Msingi wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI Bwana Benjamin Oganga akisisitiza jambo kwa waalimu wa shule za sekondari za umma (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya TEHAMA kwa waalimu hao kwenye ukumbi wa Chuo cha Kompyuta ya Sayansi, Habari na Mawasiliano, Chuo Kikuu cha Dodoma.
Baadhi ya waalimu wa shule za sekondari za umma wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo ya TEHAMA kwa ajili ya waalimu hao kwenye ukumbi wa Chuo cha Kompyuta ya Sayansi, Habari na Mawasiliano, Chuo Kikuu cha Dodoma.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (aliyekaa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na waalimu wa shule za sekondari za umma baada ya kufungua rasmi mafunzo ya TEHAMA yatakayotolewa kwa waalimu hao kwenye ukumbi wa Chuo cha Kompyuta ya Sayansi, Habari na Mawasiliano, Chuo Kikuu cha Dodoma.

Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inatoa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa walimu wa shule za sekondari za umma nchi nzima kwa lengo la kuwawezesha kutumia TEHAMA kwa ajili ya waalimu kufundishia na wanafunzi kujifunzia ambapo itachagiza na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati akimwakilisha Waziri wake, Profesa Makame Mbarawa kwenye ufunguzi wa mafunzo ya TEHAMA kwa waalimu 327 wa shule za sekondari za umma kutoka kwenye shule 109 kwenye mikoa yote nchi nzima ambapo mafunzo hayo yanafanyika kwa siku tano, Chuo Kikuu cha Dodoma mkoani Dodoma. 

Mhandisi Nditiye amefafanua kuwa Serikali imeona ombwe lililoko baina ya shule za umma na zile za binafsi katika masuala yanayohusu TEHAMA na ndio maana imekasimu jukumu hili kwa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ili iweze kuziba ombwe hilo na kuhakikisha kuwa shule zote za umma zinaunganishwa na mtandao wa intaneti na shule hizo zinapatiwa vifaa vya TEHAMA.

Mhandisi Nditiye amesema kuwa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ni kuboresha sekta ya elimu nchini kwa kuhakikisha kuwa walimu na wanafunzi wanapatiwa miundombinu inayohitajika, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kuboresha maslahi ya waalimu ili kuongeza kiwango cha ufaulu kwenye shule za msingi na sekondari za umma.

Wizara hii imepewa dhamana ya kusimamia masuala ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano na kwa misingi hiyo Wizara inaunga mkono jitihada za Mhe. Magufuli kwa kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa waalimu 327 kutoka shule mbalimbali 109 za mikoa yote ili waalimu hawa waweze kutumia TEHAMA kama nyenzo na kichocheo cha kuchagiza kuongeza kiwango cha ufaulu kwa shule za sekondari za umma. 

Naye mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Bi. Justina Mashiba amesema kuwa Mfuko umeandaa mafunzo hayo ambayo yatatolewa kwa waalimu kwenye vituo viwili ambavyo ni Chuo Kikuu cha Dodoma na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam ili kuwawezesha waalimu kupata mafunzo hayo. Mashiba amesema kuwa, “lengo letu ni kuhakikisha kuwa huduma za mawasiliano zinafika katika maeneo yote ya vijijini na tunaendelea na juhudi za kuhakikisha kuwa shule zetu za umma zinaunganishwa na mtandao wa intaneti ambapo shule pia zimekuwa zikipatiwa vifaa vya TEHAMA”. 

Ameongeza kuwa UCSAF itatoa kompyuta 545 kwa shule 109 ambapo kila shule itapata kompyuta tano. Amesema kuwa mafunzo haya ni ya awamu ya pili ya mafunzo kwa waalimu baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mafunzo kama haya mwaka jana ambapo jumla ya waalimu 286 walipatiwa mafunzo haya.

Mhandisi Nditiye amewaeleza waalimu hao kuwa mafunzo ya TEHAMA watakayopatiwa kwa siku tano sio yale ya kawaida waliyozoea kufundishwa, bali mafunzo haya yanaingia ndani zaidi kidogo tofauti na tulivyozoea kujifunza namna ya kutumia kompyuta, bali awamu hii mtajifunza ufundi wa kompyuta, utunzaji wa kompyuta na namna ya kurekebisha hitilafu ndogo ndogo kwenye kompyuta na vifaa vya TEHAMA. 

Amewasisitiza waalimu hao kuwa Serikali kupitia UCSAF imewekeza kwenu kwa ajili ya Taifa lote, muende mkashirikiane na wenzenu ambao hawakupata mafunzo haya, mkawafundishe mlichojifunza, mkatatue changamoto katika matumizi ya vifaa vya TEHAMA mrejeapo kwenye maeneo yenu ya kazi na ikumbukwe kuwa unapopata ujuzi na usipoutumia baada ya muda unapotea.

Amesema kuwa Serikali inatoa mafunzo haya baada ya kubaini changamoto zinazowakabili waalimu katika kutekeleza majukumu yao na namna wajanja wachache walivyoona fursa ya kupata pesa katika shule za umma zenye kompyuta kwa sababu tu ya uelewa mdogo wa masuala ya TEHAMA. “Tunajua kabisa kuna wakati mwingine unataka kuchapisha taarifa ama kazi kutoka katika kompyuta yako unashindwa kwa sababu tu kuna karatasi imekwama ndani au waya wa kuunganisha vifaa hivyo haujakaa sawa lakini kwa kutojua unaanza kumtafuta fundi ambaye akifika lazima umlipe kwa kazi ambayo kwa kweli hata wewe mwenyewe ungeweza kuifanya,”amesema Mhandisi Nditiye.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Msingi kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bwana Benjamin Oganga amesema kuwa TAMISEMI inashirikiana bega kwa bega na UCSAF na Wizara ambapo wataalamu kutoka TAMISEMI wanaratibu mafunzo haya na kitaundwa kikosi maalumu cha kufuatilia utekelezaji wa mafunzo haya kwenye shule zote nchini nzima ambako waalimu wake wamepatiwa mafunzo haya.

Naye Mkuu wa Chuo cha Kompyuta ya Sayansi, Habari na Mawasiliano wa Chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Aloyce Mvuma amemhakikishia Mhandisi Nditiye kuwa Chuo kina wakufunzi wenye weledi wa kutosha wa ngazi ya kimataifa na waalimu hao watapatiwa mafunzo stahiki ya TEHAMA kwa vitendo. Prof. Mvuma amewataka waalimu hao kuwa tayari kuuliza maswali ili waweze kuelewa wanachofundishwa kwa manufaa ya wenzao wanaowawakilisha na kwa manufaa ya taifa letu.

Pia, mwakilishi wa waalimu Bwana Sammy Charles Sanga wa kutoka Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu ameishukuru Serikali kwa kuwakumbuka na kuwapatia mafunzo hayo ambapo yatawawezesha kwenda kufundishia waalimu wenzao na wanafunzi ili kuiwezesha Serikali kufikia azma yake ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi kwenye sekondari za umma. 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya UCSAF Dkt. Joseph Kilongola amemshukuru Mhandisi Nditiye kwa kuyapa uzito mafunzo haya na kufika kuyafungua rasmi kwa niaba ya Waziri wake, Prof. Makame Mbarawa.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: