Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

MRATIBU wa chanjo Mkoa wa Pwani, Abbas Hincha amesema, jumla ya watoto wa kike 18,823 waliopo shule na nje ya shule mkoani hapo wanatarajia kupatiwa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi mwaka huu. Aidha ameitoa shaka jamii kuwa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi ni salama, haina madhara na haiathiri uwezo wa binti kupata watoto hapo baadae .

Akitolea ufafanuzi juu ya suala hilo, wakati wa semina kwa wanahabari kuhusu uanzishwaji wa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi, Kibaha, Hincha alisema tayari wameshapokea chanjo na wataanza kuzitoa katika vituo mbalimbali vya huduma.

Pamoja na hayo ,alivitaka vyombo vya habari kubaini uzushi ama uvumi kuhusu chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi na kutoa taarifa kwa wataalamu wa afya katika mamlaka husika na kutoa mrejesho kwenye jamii baada ya kupata ufafanuzi wa kitaalamu.

Hincha alieleza chanjo hiyo haina madhara na badala yake ina viudhi vichache kama ilivyo kwenye chanjo nyingine ikiwemo kuweka wekundu ama kuweka uvimbe kiasi eneo alilochomwa mhusika mkono wa kushoto. Aliwataka wazazi na jamii kuacha kudanganyana na kuzusha mambo ambayo yatakwamisha juhudi za kutolewa chanjo hiyo .

Mratibu huyo ,alisisitiza serikali imethibitisha usalama wa umadhubuti wa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi ndiyo maana imeiongeza kwenye mpango wa Taifa wa chanjo ili iweze kusaidia kudhibiti tatizo hilo kwa akinamama.

Alisema mwaka 2018 chanjo itatolewa kwa wasichana waliofikisha umri wa miaka 14 na ili kupata kinga kamili walengwa watahitaji kupatiwa dozi mbili.

"Dozi ya pili itatolewa miezi 6 baada ya kupata dozi ya kwanza" alisema Hincha.

Hincha alisema chanjo ya HPV kwa wasichana huwakinga wasipate saratani ya mlango wa kizazi pindi wawapo watu wazima wakiwa na familia zao.

Kaimu mganga mkuu wa mkoa huo ,Hussein Athumani ambae pia anaesimamia masuala ya kinywa na meno Mkoani Pwani,alisema saratani hiyo ina athari kubwa kwa afya ya wanawake ulimwenguni kote. Alisema inakadiriwa kuwa kila mwaka kati ya wanawake 466,000 wanathibitika kuwa na saratani ya mlango wa kizazi na wengi wao wako katika nchi zinazoendelea.

Athumani alisema saratani hiyo inashika nafasi ya pili kwa kusababisha saratani kwa wanawake, nafasi ya kwanza inashikwa na saratani ya matiti .

"Nchini Tanzania saratani ya mlango wa kizazi ni ya kwanza kwa vifo ikifuatiwa na saratani ya matiti " Saratani hizi mbili kwa pamoja husababisha zaidi ya asilimia 50 ya vifo vyote vya wakinamam vitokanavyo na saratani"alibainisha Athumani.

Alifafanua chanjo hiyo inagharama kwani dozi moja ni dollar 15 ambapo dozi mbili ni dollar 30. Athumani alielezea ,wanawake 7,304 nchini wamegundulika kuwa na saratani ya shingo ya kizazi kati ya hao 4,216 asilimia 18 walifariki kutokana na tatizo hilo .

Kwa upande wake ,mgeni rasmi katika semina hiyo ,Gerald Manase kutoka TAMISEMI alisema ,wasichana na wanawake wanaohitaji huduma ya chanjo ambao sio walengwa wa uanzishwaji wa chanjo hiyo inayotolewa na mlango wa Taifa wa chanjo wanaweza kupata chanjo katika hospital binafsi zinazotoa chanjo hiyo .

Dalili za saratani hiyo ni maumivu ya mgongo,miguu ,kiuno,kuchoka,kutokwa damu nyingi bila mpangilio baada ya kujamiiana,uchafu kwenye uke wa majimaji,kuvimba miguu na inasababishwa na virusi vinavyojulikana kitaalamu kama human papilloma virus (HPV).
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: