Wanafunzi wa shahada ya uzamili wa fani za afya wakifuatilia warsha ya maadili ya kitaaluma iliyofanyika katika hospitali ya taaluma na tiba, MAMC
Kutoka kulia, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba, MAMC, Dkt Hendry Sawe, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Huduma za Hospitali, Prof. Said Aboud, Mkurugenzi wa mafunzo ya Uzamili, Dkt Emmanuel Balandya na Mkurugenzi wa Mafunzo Endelevu na Maendeleo ya Uweledi Dkt Doreen Mloka wakifuatilia ufunguzi wa warsha ya maadili ya kitaaluma kwa wanafunzi wa shahada ya uzamili wa afya, MAMC.
Mratibu wa warsha ya maadili ya kitaaluma ya wanafunzi wa shahada ya uzamili wa fani za afya, Dkt Francis Furia akiongoza kipindi majadiliano wakati wa warsha hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano MAMC
Mwanafunzi wa shahada ya uzamili, MUHAS akichangia hoja wakati wa kipindi cha majadiliano katika warsha ya maadili ya kitaaluma kwa wanafunzi wa shahada ya uzamili wa afya ilitolewa na hospitali ya taaluma na tiba, MAMC iliyopo Mloganzila.
---
Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi, MAMC iliyopo Mloganzila imefanya warsha ya mafunzo ya maadili ya taaluma kwa wanafunzi wa shahada ya uzamili.

Akizungumza katika warsha hii Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Huduma za Hospitali, Prof. Said Aboud amesema msingi wa huduma zinazotolewa na hospitali ya Taaluma na Tiba, MAMC umemlenga mgonjwa na hivyo kiwango cha hali ya juu cha maadili ya taaluma kinahitakiwa ili tuweze kufikia lengo hili.

Prof. Aboud amesisitiza kuwa wanafunzi wa shahada ya uzamili katika fani za afya ambao tayari ni madaktari, wafamasia, wauguzi n.k ni nguvu kazi muhimu sana katika hospitali kwa hiyo ni muhimu kuhakikisha wanatoa huduma nzuri kwa wateja ambao ni wagonjwa na pia kuzingatia kutoa taarifa zilizo sahihi na kwa wakati kwa mgonjwa au ndugu wa mgonjwa.

Naye Mkurugenzi wa Mafunzo ya Uzamili, Dkt Emmanuel Balandya amekumbusha kuwa MUHAS inazingatia masuala ya maadili ya kitaaluma kwa umakini sana na ndio maana yamesisitizwa wakati walipoanza mafunzo na kufundishwa katika muhula wa kwanza wa masoma. Na kwa kuwa mafunzo haya ni endelevu, Dkt Balandya ameeleza, imeonekana ni muhimu kuwa na warsha hii katika kipindi hichi cha mpito kutoka masomo ya sayansi za msingi (basic sciences) kwenda kwenye masomo ya sayansi za kliniki (clinical sciences).

Dkt. Balandya amewasisitizia kuwa washiriki wa warsha hii kuwa namna wanavyomjali mgonjwa ni muhimu zaidi kuliko kile wanachokijua. "Tunaweza kushindwa kuhakikisha kuwa wagonjwa wote wanapona lakini tunaweza kubadilisha maisha yao kwa namna tunavyowahudumia kwa kuwajali", aliongeza.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba MAMC, Dkt Hendry Sawe amesema warsha hii ya maadili ya kitaaluma kwa watu wa fani za afya (madaktari, wafamasia, wauguzi n.k) imelenga namna ya kufanya kazi kitaaluma kwa kuzingatia kanuni za ufanyaji kazi za taaluma husika. Hii ni muhimu kwa sababu watoa huduma wa afya wanahusika moja kwa moja na maisha ya watu (wagonjwa).

"Mafunzo haya yamejikita kwa wanafunzi wa shahada ya uzamili kwa sababu wengi wao ni viongozi wajao katika fani mbalimbali za afya nchini", aliongeza Dkt Sawe.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: