Mwandishi Wetu, Nzega.

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema katika Serikali ya awamu ya tano, mawaziri wanaisikia Ulaya kwenye bomba tofauti na zamani na kuwa sasa kazi yao ni kutembelea kwenye Wilaya kutatua kero za wananchi.

Mwalimu alisema hayo alipokuwa akizindua Kituo cha Afya cha Zogolo kilicho kwenye Wilaya ya Nzega ambacho kimeboreshwa kutokana na mchango wa wizara yake wa Sh bilioni 500, nguvu za wananchi na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe.

“Zamani mlikuwa mmezoea kutusikia tunaenda Ulaya, China na kwingineko, siku hizi tunakusikia tu kwenye bomba, sisi zetu ni Zogolo kuangalia kero za wananchi, ndiyo maana leo niko hapa kuwasikiliza na kufungua kituo hiki,” alisema Mwalimu.

Katika hatua nyingine, Mwalimu aliwahamaisha wananchi hao kujiunga na bima mbalimbali za Afya ili waweze kupatiwa matibabu pale wanapougua.

Alisema kwa sasa bima hizo zinapatikana kwa kuanzia Sh 10,000, hivyo kila mwananchi akiamua kujali afya yake ataweza.

“Kuna mpango nataka tuwaletee, kwasababu nyie mnalima sana mpunga, NHIF (Mfuko wa Bima ya Taifa), watakuja ukitoa gunia boma la mpunga ambalo linauzwa kama Sh 50,000 utapata bima ya afya ambayo itakuwezesha utibiwe kwenye karibu hospitali zote nchini zikiwamo za binafsi.

“Ukiwa na bima itakusaidia, unaweza kuumwa kipindi ambacho hauna hata Sh1,000 lakini bima hizi zitakusaidia, zipo mpaka za CHF ambazo kwa Sh 10,000 tu kaya ya watu sita inapata matibabu mwaka mmoja,” alisema Mwalimu.

Kwa upande wake Bashe, alisema kuhakikisha kituo hicho cha afya kinaibuliwa na kufikia hadhi hiyo na kukipatia gari la wagonjwa, ilikuwa ni moja ya ahadi zake Serikali ya awamu ya tano walipoomba kura mwaka 2015.

Alisema jambo hilo limeshatimia kwa asilimia 100 ikiwa sasa hivi wanasubiri maji yanayotoka ziwa Victoria ili kutimiza ahadi nyingine muhimu.

“Waziri nakuomba ukienda kwenye baraza la Mawaziri udukishe shukrani zetu kwa Rais, alitusaidia kupata fedha hizo ambazo zimejenga OPD (jingo la wagonjwa wa nje), kujenga nyumba ya watumishi na kukarabati nyingine sita, wodi ya kina mama imejengwa, hatuna namna nyingine ya kumshukuru.

“Kwa sasa hivi, maji, hospitali, umeme hatudaiwi tena, nimebaki na suala la shule tu ambalo nalo linakaribia kukamilika,” alisema Bashe.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, alisema mkoa huo unaupungufu wa wataalamu wa afya wakiwamo madaktari kwa asilimia 50.

Kutokana na hali hiyo, aliomba serikali kuwasaidia kupata wataalamu hao ili wananchi waweze kupata huduma.

Pia aliwataka watumishi wa afya waliopo kutoa huduma hiyo kwa ufasa ili wananchi waweze kufaidia na kodi zao.

Alisema hatosita kuchukua hatua pale atakapopata malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya kunyanyaswa ama kukosa huduma.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: