Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Makwaia Makani akipokea cheti cha utambuzi wa huduma zinazotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Mwanakwerekwe- Zanzibar, Ali Salim Khamis ambaye mtoto wake alipatiwa huduma ya matibabu katika hospitali hiyo.
Daktari Bingwa wa Upasuaji Watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dkt. Zaitun Bokhary akipokea cheti cha utambuzi wa huduma kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Mwanakwerekwe- Zanzibar, Ali Salim Khamis.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura na Ajali, Dkt. Kefa akipokea cheti cha utambuzi kwa niaba ya Dkt. Juma Mfinanga ambaye ni Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali katika hospitali hiyo.
Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Makwaia Makani akiwa katika picha ya pamoja na Mbunge Ali Salim Khamis wa Jimbo la Mwanakwerekwe na madaktari wa hospitali hiyo.
Cheti cha utambuzi wa huduma kilichotolewa kwa hospitali hiyo.
Cheti cha utambuzi alichokabidhiwa Dkt. Zaitun Bokhary.

Mbunge wa Jimbo la Mwanakwerekwe Mh. Ali Salim Khamis leo ameipongeza Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) pamoja na watalaam wake wote kwa jinsi walivyompokea mtoto wake na kumpa huduma stahiki.

“Leo natoa shukrani zangu za dhati kwa MNH na kukabidhi barua ya shukrani na cheti cha utambuzi wa huduma nzuri aliyopewa mwanangu Muniri Ali Salim tangu alivyopokelewa kupitia Idara ya Magonjwa ya Dharura na kisha kupelekwa Idara ya Upasuaji Kitengo cha Upasuaji wa watoto. Mtoto wetu alikuwa na uvimbe kichwani ambao ulisababisha afanyiwe upasuaji na kutolewa vizuri, sasa mtoto wetu anaendelea vizuri sana,” amesema Mh. Khamis.

Amepongeza kazi nzuri inayofanywa na MNH chini ya usimamizi wa Mkurugenzi Mtendaji, Prof. Lawrence Museru kwa kushirikiana na wauguzi, madaktari na watalaam wengine ambao wamekuwa wakijitoa kutoa huduma nzuri kwa mtoto wake pamoja na wahitaji wengine wanaofika MNH kupata huduma.

“Nimeamua kutoa barua ya shukrani kwenu, cheti cha utambuzi kwa MNH, Idara ya Upasuaji kupitia Kitengo cha Upasuaji Watoto, Idara ya Magonjwa ya Dharura na kipekee kwa Dkt. Juma Mfinanga ambaye ni daktari Bingwa wa Magonjwa ya Dharura pamoja na Dkt. Zaitun Bhokare ambaye ni daktari bingwa wa upasuaji watoto kwa kazi nzuri ambayo imefanikisha matibabu kwa mtoto wetu,” amesema Mh. Khamis.

Akipokea cheti na barua kwa niaba ya MNH, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bw. Makwaia Makani amemshukuru Mh. Khamis kwa utambuzi na kutoa mrejesho chanya kutokana na huduma ya matibabu aliyopatiwa mtoto wake.

“Sisi kama watoa huduma tunapokea maoni aina zote, lakni maoni ya kupongeza ni machache ukilinganisha na maoni mengine. Hivyo hii imetupa hamasa kubwa sana na watalaam wetu wamefurahi,” amesema Bw. Makani.

Daktari Bingwa wa Upasuaji Dkt. Zaituni Bokhari amesema walimpokea mtoto Munira Ali Salim mwezi mmoja uliopita na baada ya kumfanyia uchunguzi waligundua alikuwa na uvimbe kichwani (kichogoni) na hivyo kumpatia huduma ya upasuaji.

Dkt. amesema kuwa baada ya kujiridhisha kwamba ana uvimbe huo kwenye ubongo waliamua kumfanyia upasuaji na kutoa uvimbe huo. Dkt. Bhokari anasema mara baada ya upasuaji mtoto aliendelea vizuri na hatimaye kuruhusiwa kwenda nyumbani.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: