Majaji 10 wa Mahakama Kuu, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka wakiimba wimbo wa Taifa kabla ya kuapishwa na Ikulu jijini Dar es salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 20 Aprili, 2018
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Elvin Claud Mgeta kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Ikulu jijini Dar es salaam leo tarehe 20 Aprili, 2018
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe.Thadeo Marco Mwenempazi kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Ikulu jijini Dar es salaam leo tarehe 20 Aprili, 2018
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Dkt. Ally Saleh Possi kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Ikulu jijini Dar es salaam leo tarehe 20 Aprili, 2018
Viongozi wote walioapishwa wakila kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kikiongozwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela Ikulu jijini Dar es salaam leo tarehe 20 Aprili, 2018\
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiongea machache baada ya kuwaapisha Majaji 10 wa Mahakama Kuu, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Ikulu jijini Dar es salaam leo tarehe 20 Aprili, 2018.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 20 Aprili, 2018 amewaapisha Majaji 10 wa Mahakama Kuu, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka aliowateua tarehe 15 Aprili, 2018.

Majaji walioapishwa ni Mhe. Elvin Claud Mgeta, Mhe. Elinaza Benjamin Luvanda, Mhe. Yose Joseph Mlyambina, Mhe. Immaculata Kajetan Banzi, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Mhe. Paul Joel Ngwembe, Mhe. Agnes Zephania Mgeyekwa, Mhe. Stephen Murimi Magoiga, Mhe. Thadeo Marco Mwenempazi na Mhe. Butamo Kasuka Philip.

Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Dkt. Evaristo Emmanuel Longopa kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Edson Athanas Makallo kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Dkt. Julius Clement Mashamba kuwa Wakili Mkuu wa Serikali na Dkt. Ally Saleh Possi kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.

Baada ya kuapishwa kwao, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kufanya uteuzi wa Majaji hao na kwamba uteuzi huo utasaidia kupunguza mrundikano wa mashauri ya Mahakama Kuu ambapo sasa Jaji mmoja atakuwa akisikiliza wastani wa mashauri 460 kwa mwaka ikilinganishwa na Jaji mmoja kusikiliza mashauri 535 kabla ya uteuzi huo.

Mhe. Prof. Juma amewahusia Majaji wapya umuhimu wa kuzingatia majukumu yao, miiko na kuwa mfano bora wa kusimamia sheria na pia ametoa wito kwa wananchi kuwa makini wanapopata taarifa za mahakama kutoka vyanzo visivyo rasmi kwani kumekuwa na upotoshaji wa makusudi.

“Mhe. Rais Bajeti yetu ya mwaka 2017/18 ilikuwa Shilingi Bilioni 125, bajeti tuliyopangiwa sasa 2018/19 ni Shilingi Bilioni 141, sasa wanaosema bajeti imeshuka, imeshuka kwa namna gani? labda ni kushuka kwa kugeuza. Kwa upande wa bajeti ya maendeleo kwa mwaka 2017/18 ilikuwa Shilingi Bilioni 18, mwaka huu tumepangiwa Shilingi Bilioni 35” amesisitiza Mhe. Prof. Juma.

Akizungumza baada ya salamu za Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Majaji na viongozi wote walioapishwa na ametoa wito kwao kutekeleza majukumu yao kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu, kuweka mbele maslahi ya Taifa na kutenda haki hasa kwa Watanzania wanyonge wakiwemo wajane na watu masikini ambao hudhulumiwa katika vyombo vya kutolea haki.

Mhe. Rais Magufuli ameungana na Jaji Mkuu wa Tanzania kuwatahadharisha Watanzania dhidi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kufanya upotoshaji wa taarifa na kuleta madhara katika jamii na ametaka Majaji na mamlaka nyingine zichukue hatua za kisheria dhidi ya wanaofanya upotoshaji huo.

Mhe. Rais Magufuli ametaja upotoshaji mmojawapo kuwa ni madai kwamba Serikali imeiba Shilingi Trilioni 1.5, na akamuuliza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Juma Assad ambaye amejibu sio kweli kwamba fedha hizo zimeibwa.

“Nilikuwa nasoma mahali wanasema Serikali imeiba Shilingi Trilioni 1.5, siku moja nikampigia CAG, kwamba mbona kwenye ripoti yako uliyonisomea Ikulu hukunieleza huu wizi wa Trilioni 1.5? Kwa sababu ungenisomea siku hiyo hiyo ningefukuza watu, kama nimefukuza wakurugenzi watatu siku hiyo hiyo kwa sababu ya hati chafu, hawa wa Trilioni 1.5 uliwaficha wapi? Nimejaribu kupita kwenye ripoti siioni mahali palipoandikwa zimepotea Trilioni 1.5, Prof. Assad akaniambia hakuna kitu kama hicho, nikamuuliza Katibu Mkuu akasema hakuna kitu kama hicho” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Viongozi wote walioapishwa pia wamekula kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela, na hafla ya kuapishwa kwao imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi, Makatibu Wakuu, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa dini.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: