Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linapenda kutoa taarifa kwa umma kufuatia tukio la moto kwenye ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililotokea mnamo tarehe Aprili 9, 2018 majira ya saa 1:28 usiku mkoani Dodoma.

Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa moto huo ulisababishwa na shoti iliyotokana na Power bank iliyokuwa inatumiwa kuchaji simu. Shoti hiyo ilisababisha kuungua kwa simu, Power bank, sehemu ya meza na kapeti kitendo kilicholeta moshi mkubwa na taharuki miongoni mwa Wabunge. Ukiachilia mbali taharuki kwa Waheshimiwa Wabunge hakuna madhara kwa binadamu yaliyotokana na moto huo. 

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji anatoa rai kwa Watanzania wote kuchukua tahadhari kubwa hasa wanapokua wanatumia vifaa vya kieletroniki ambavyo kwa sasa vipo katika matumizi hadi katika ngazi ya familia. Moto huzuka tu endapo kitapatikana chakula cha moto, joto la kutosha na hewa ya oksijeni (fuel, heat and oxygen). 

Sambamba na hayo Kamishna Jenerali anahimiza uzingatiaji wa kinga na tahadhari ya moto katika maeneo yote. Wamiliki wa maeneo ya umma, binafsi na biashara wanapaswa kufunga vizimia moto kwa kuzingatia ushauri unaotolewa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. 

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lipo imara na litaendelea kuwaelimisha Watanzania kuzingatia kinga na tahadhari ya moto ili kuhakikisha maisha na mali vinakuwa salama.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: