Afisa Utamaduni Sekretarieti ya Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Adorph Halii (kulia) akizungumza wakati wa kikao cha Maafisa Utamaduni wa Mkoa wa Dar es Salaam, wilaya zake pamoja na Bodi ya filamu katika kupitia na kutoa maoni juu ya kanuni maalum za kuendesha vibanda vya kuonyesha filamu leo Jijini Dar es Salaam.
 Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo (kulia) akiwaonyesha wajumbe wa kikao cha kupitia na kutoa maoni juu ya kanuni maalum za kuendesha vibanda vya kuonyesha filamu (hawapo pichani) moja ya kitambulisho kitakachotolewa kwa wadau wa sekta ya filamu kutokana na vigezo vilivyowekwa wakati wa kikao na wadau hao leo Jijini Dar es Salaam.
 Afisa Utamaduni Halmashauri ya Wilaya ya Temeke Bw. Emanuel Ndumukwa (katikati) akichangia mada wakati wa kikao cha Maafisa Utamaduni wa Mkoa wa Dar es Salaam, wilaya zake pamoja na Bodi ya filamu katika kupitia na kutoa maoni juu ya kanuni maalum za kuendesha vibanda vya kuonyesha filamu leo Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Afisa Utamaduni Wilaya Kinondoni Bibi. Joyce Kiriho.
Maafisa Utamaduni Mkoa wa Dar es Salaam katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Bodi ya Filamu baada ya kikao cha kupitia na kutoa maoni juu ya kanuni maalum za kuendesha vibanda vya kuonyesha filamu leo Jijini Dar es Salaam. Waliokaa kushoto ni Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo

Picha/Habari na Genofeva Matemu - WHUSM.

Wadau wa sekta ya Filamu nchini wameiomba bodi ya filamu kunao umuhimu wa kuongezea makali ya kikikanuni katika kusimamia vibanda vinavyoonyesha sinema nchini kwa kuzifanya kanuni maalumu za kusimamia vibanda vya sinema kuzingatia kumuwajibisha mmiliki wa Eneo au kibanda husika badala ya kumuwajibisha aliyeajiriwa kuendesha vibanda hivyo peke yake.

Hayo yamesema na Afisa Utamaduni Sekretariate ya Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Adorph Halii wakati wa kikao cha maafisa utamaduni wa mkoa wa Dar es Salaam na Bodi ya filamu katika kupitia na kutoa maoni juu ya kanuni maalum za kuendesha vibanda vya kuonyesha filamu leo Jijini Dar es Salaam.

Aidha Bw. Adorph amezitaka bodi za filamu katika ngazi za mikoa na wilaya kuwa hai ili ziweze kuunganisha nguvu kwa pamoja kusimamia vizuri vibanda vya kuonyeshea sinema kwani wakilegalega katika kusimamia vibanda hivyo kutapelekea mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii hivyo kuwa na taifa lisilo na maadili kutokana na kuwaacha watoto wadogo kuangalia filamu zisizoendana na umri wao.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo amesema kuwa Bodi ya filamu imekua ikipokea malalamiko mengi sana kuhusu vibanda vinavyoonyesha sinema kuwa vimekua vikisababisha uvunjifu wa maadili katika jamii hivyo kuwataka maafisa utamaduni wa mkoa na wilaya kutoa elimu kwa wamiliki wa vibanda hivyo ili kuweza kuepukana na adhabu zitakazotolewa endapo kanuni hizo zitapita.

“Ni wajibu wa kila mmiliki na msimamizi wa maeneo na vibanda vya kuonyesha sinema kukidhi vigezo vitakavyoainishwa katika kanuni zinazoandaliwa na kuzifuata kwani atakayekiuka vigezo tajwa atachukuliwa hatua kali hii ikiwa ni kurejesha maadili bora na staha katika jamii zetu” amesema Bibi. Fissoo

Naye Afisa Utamaduni Halmashauri ya Wilaya ya Temeke Bw. Emanuel Ndumukwa ameitaka bodi ya filamu kuongeza kipengele cha afisa utamaduni wa wilaya kuwa na sehemu ya kuridhia maombi ya fomu za kuomba ithibati zinazotolewa na Bodi ya Filamu ili kuweza kuleta ufasaha wa kuthibitisha maombi ya wadau kuanzia ngazi ya wilaya. 

Kutokana na vibanda vya kuonyesha sinema kukadiriwa kuwa zaidi ya 30,000 nchi nzima na kuonekana kuwa ni sehemu muhimu ya soko la kazi za filamu, na sehemu ya kufikisha burudani kwa watanzania ipo haja ya kuimarisha maeneo hayo ili yawe salama nayaweze kuwa na tija kwa Sekta ya Filamu nchini.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: