Mwenyekiti ya Jumuiya ya Wanawake wa Tanzania (UWT) Gaudentia Kabaka akizungumza na Waandishi wa habari leo Makao Makuu ya Jumuiya hiyo, Suwata Kariakoo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa UWT Bara Eva Kihwelo (Picha na Bashir Nkoromo).

NA BASHIR NKOROMO.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Gaudentia Kabaka amewataka Wanawake kote nchini wasione fahari kuitwa 'Dume-Jike' bali wawe wanawake wenye msimamo imara na jasiri kwa maendeleo yao na ya nchi kwa jumla.

Gaudentia ameto mwito huo, wakati akiwasilisha salaam maalum za pole kwa ndugu jamaa, marafiki na hasa wanawake wote hapa nchini na duniani kote kufuatia kifo cha Winnie Mandela aliyemwelezea kuwa alikuwa amwanamke shupavu katika kupigania haki na vita dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.

"Tazama Winnie Mandela alikuwa mpambanaji hata kabla ya kuwa mke wa Rais Nelson Mandela, kwa hiyo tukiangalia historia yake tunabaini kuwa hakuhitaji msukumo wa nguvu za mwanaume katika kuonyesha ushupavu wake", alisema.

Alisema Winnie Mandela aliyefariki dunia Aprili 2, mwaka huu, aliendelea kuonyesha ushupavu wake katika kupambana na udhalimu na ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini hata wakati Mandela akiwa gerezani.

"Winnie atakumbukwa na Watanzania na dunia nzima kwa ujasiri wake pia atakumbukuwa kwa umaarufu alioupata hata akiwa bado mwanafunzi, msichana kabla ya kuolewa. Alichukia kuona Mwafrika anabaguliwa, anatengwa asifike kwenye maeneo walipokuwa weupe. 

Kwa hiyo umaarufu wa Winnie haukutokana tu kwa kuwa ni mke wa Rais yaani “First lady “ lakini umarufu wake ulikuwa wa kwake mwenyewe. Alijitambua, akajiamini, akatimiza wajibu wake kama Binadamu, kama Mwafrika, baadaye kama Mke, Mama, Mwanasiasa na Kiongozi" alisema Gaundetia

Tunatambua uwezo tulionao wanawake lakini pia tuwe wastahimilivu tunapokumbana na magumu tupambane hadi mwisho. Kama Winnie Madikizela Mandela aliweza kutetea Waafrika wenzake hata baada ya mume wake kufungwa; kwa sababu hiyo kwa nini sisi wengine tusiweze kujitokeza waziwazi na kuiunga Serikali na Rais wetu Dk. John Magufuli katika juhudi zake za kupiga vita ufisadi, wizi wa mali ya umma, kutowajibika", Alisema Gaudentia.

Alisema, kama Winnie Mandela alivyotimiza wajibu wake katika harakati za Waafrika kuing’oa Serikali dhalimu ya kibaguzi nchini Afrika kwa nafasi yake kama mwanamama, na wanawake wa Tanzania kila mmoja kwa nafasi yake wanaweza kuwa chachu ya kuleta mabadiliko ya kweli hapa nchini.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: