Na JAMII WA JAMII, DAR

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imeamuru Mkurugenzi wa Kampuni ya Tip Top Connection ya jijini Dar es Salaam, Hamis Taletale maarufu Babu Tale, kurudishwa Mahabusu ya polisi. Mpaka msajili wa mahakama hiyo atakaporudi kutoka Dodoma.

Amri hiyo imetolewa na Naibu Msajili wa mahakama hiyo, Lucy Massam baada ya Babu Tale na Mhadhiri wa Dini ya Kiislamu, Sheikh Hashim Mbonde kushindwa kufikia makubaliano licha ya msajili kuwapa muda wa dakika 10 pande zote wajadiliane namna ya kulimaliza suala hilo.

Babu Tale mbaye pia ni meneja wa mwanamuziki maarufu wa 'Bongo Fleva' Diamond Platnumz, amefikishwa mahakamani hapo leo Mei 23/ 2018 akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi kusikiliza kesi inayomkabili.

Babu Tale, amekamatwa kufuatia amri iliyotolewa Februari 16/ 2018 na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Wilbard Mashauri iliyoamuru mtuhumiwa huyo na ndugu yake, Idd Taletale wakamatwe.

Amri hiyo pia, ilielekeza watuhimiwa hao wakikamatwa wapelekwe Gereza la Ukonga wakiwa wafungwa wa kesi ya madai, hadi hapo mahakama hiyo itakapotoa maelekezo mengine.

Hata hivyo, mtuhumiwa Babu Tale baada ya kufikishwa mahakamani hapo jana kesi yake ilishindikana kusikilizwa kwa kuwa Msajili Mashauri yuko Dododoma Kikazi.
Kufuatia kushindwa kufikia muafaka baada ya dakika hizo kumi kuisha, Msajili Massam ameamuru babu Tale arudishwe mahabusu ya polisi mpaka Msajili Mashauri atakaporudi kwa ajili ya maelekezo mengine.

Hata hivyo kipindi chote cha majadiliano
Babu Tale alikuwa katika mahabusu ya mahakama hiyo wakati ndugu zake wanajadiliana na mdai wake kabla ya kuieleza mahakama muafaka watakaofikia na kisha mahakama kutoa maelekezo.

Awali Mahakama hiyo iliwaamuru watuhumiwa hao kumlipa Mhadhiri wa Dini ya Kiislamu, Sheikh Hashim Mbonde kiasi cha Sh250 milioni, baada ya kupatikana na makosa ya ukiukwaji wa haki za hakimiliki kwa kutumia masomo yake kibiashara bila ridhaa yake kinyume cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.

Katika kesi ya msingi, Sheikh Mbonde alikuwa akidai kuwa aliingia mkataba na kampuni ya kina Babu Tale (Tiptop Connection) ili wamrekodi mahubiri yake kisha wayauze na kugawana mapato.
Hata hivyo baada ya kurekodi masomo saba, walimkatia mawasiliano na alipowatafuta na kukutana nao wakamweleza kuwa wameamua kuachana na mpango huo.
Sheikh Mbonde alidai kuwa akiwa kwenye mahubiri Dodoma ndipo akakutana na mikanda ya video katika mfumo wa DVD yenye mahubiri yake huku kukiwa na namba za simu za viongozi hao wa Tiptop.
Sheikh Mbonde alidai baada ya kufanya uchunguzi alibaini kuwa DVD hizo zilikuwa zikiuzwa katika mikoa mbalimbali, ndipo akawafungulia kesi ya madai ya fidia kutokana ukiukwaji wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: