Mchezaji Godfrey Ernest wa timu ya Rema 1000 FC ya Haydom Manyara akimtoka mchezaji wa timu ya Rambo FC pia ya Haydom katika mchezo wao uliofanyika leo kwenye uwanja wa shule ya Msingi Haydom katika Mashindano ya kombe la Kurugenzi Cup 2018 yaliyoandaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ambapo timu ya Rema 1000 FC imeibuka na ushindi wa Magoli 5-3 dhindi ya Rambo FC. (PICHA NA JOHN BUKUKU WA FULLSHANGWE-HAYDOM- MANYARA)
Wachezaji wa timu ya Rema 100 FC ya Haydom wakishingilia mara baada ya mchezaji Raurenc Marco kuifungia timu yake ya Rema 1000 FC goli lao la tano katika mchezo huo uliokuwa mkali dakika zote za mchezo.
Kikosi cha timu ya Rema 1000 FC kikiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa mchezo huo.
Kikosi cha timu ya Rambo FC kikiwa katika picha ya pamoja kabla ya kuanza kwa mchezo huo.
Wachezaji wa timu ya Rambo FC na timu ya Rema 1000 FC wakisalimiana kabla ya kuanza kwa mchezo huo kwenye uwanja wa shule ya msingi ya Haydom.
Mchezaji Ngaja Junior wa timu ya Rambo FC bukta ya bluu na Masoud Juma wa Rema 1000 FC wakizungumza na waamuzi kabla ya kuanza rasmi kwa mchezo huo uiofanyika leo kwenye uwanja wa shule ya msingi Haydom.
Baadhi ya watoto wakigawiwa maputo kwenye benchi la ufundi la timu ya Rema 1000 FC.
Kocha wa Rema 1000 FC Jared Ochieng akitoa maelekezo kwa wachezaji wake huku mmiliki wa timu hiyo Bw.Samson Madawa Bora ambaye pia ni Daktari katika Hospitali ya Haydom akimsikiliza wakati wa mapumziko ya mchezo huo.
Baadhi ya mashabiki wakifuatilia mchezo huo.
Bw. Phars Nyanda Afisa Tehama Teknolojia Habari na Mawasiliano Halmashauri ya wilaya ya Mbulu akitoa maelezo kwa wananchi waliofika kuangalia mchezo huo kuhusu huduma ya upasuaji kwa watu walioungua kwa moto inayotolewa na daktari wa kujitolea Joost Binmerts kutoka Uholanzi akishirikiana na madaktai wa Hospitali ya Haydom.
Bw. Phars Nyanda Afisa Tehama Teknolojia Habari na Mawasiliano Halmashauri ya wilaya ya Mbulu akizungumza na daktari wa kujitolea Joost Binmerts kutoka Uholanzi anayefanya kazi katika Hospitali ya Haydom.
Baadhi ya mashabiki wa mpira waliojitokeza kushuhudia mchezo huo wakifuatilia wakati ulipokuwa ukiendelea.

Baadhi ya mashabiki wakifurahiamoja ya goli lililofungwa katika mchezo huo.
---
Kurugenzi CUP ’18 yazidi kutimua vumbi katika dimba la shule ya msingi Haydom Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, kwa timu ya Rema 1000 FC kwa kuigaragaza pasipo huruma timu ya Lambo FC kwa mabao 5-3.

Katika mchezo huo uliofanyika leo alasiri timu hizo zilitoana jasho, upinzani mkali, katika kulisakata kabumbu na kuonyeshana ufundi, kwenye mashindano hayo yaliyoandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga.

Bao la kwanza la timu ya Rema 1000 FC lilitiwa kimiani na winga machachari wao Shafii Said wenye dakika ya 26 ya kipindi cha kwanza cha mchezo huo.

Mshambuliaji hatari wa timu ya Rema 1000 FC Masudi Juma aliipatia timu yake bao la pili kwenye dakika ya 29 mara baada ya kuwachambua pasipo na huruma walinzi watatu wa timu pinzani na kupachika kimiani bao la kiufundi, hadi mapumziko timu ya Lambo haikuona nyavu ya timu pinzani.

Kipindi cha pili timu ya Lambo FC kupitia kocha wake ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa washambuliaji wawili na kuingiza nguvu mpya ambayo ilibadilisha sura ya mcheo na kuleta maajabu kwenye viwanja hivyo kwa kurudisha mabao mawili na kuongeza la tatu.

Katika dakika ya 53 mshambuliaji wa timu ya Lambo FC Lazaro Zebedayo, aliyeingia kipindi cha pili alirejesha matumaini kwa kupachika bao safi la kichwa baada ya kupokea krosi safi kutoka kwa kiungo mkabaji Patrick Zacharia. Mnamo dakika ya 60 winga machachari wa timu ya Lambo FC Salvatory Zelote aliachia shuti kali umbali wa mita 23 na kutinga kimiani na kumuacha kipa ameduwaa hivyo kufunga bao la pili na kusawazisha na kuwanyanyua mashabiki kwa vifijo na nderemo katika viwanja hivyo.

Timu ya Lambo FC iliamka usingizini baada ya kupata mabao hayo na kuishambulia kama nyuki timu ya Rema 1000 na kufanikiwa kuandika bao la tatu kupitia mshambuliaji wao machachari Lazaro Zebedayo ambaye ndiye mfungaji wa bao la kwanza.

Benchi la ufundi kupitia kocha mkuu wa timu ya Rema 1000 Jerad Ochieng alifanya mabadiliko ya haraka kwa kumtoa kiungo mmoja na washambuliaji wawili na kubadilisha sura ya mchezo kwa muda mfupi.

Baada ya mabadiliko hayo, dakika ya 79 kulitokea piga nikupige katika lango la timu ya Lambo FC na hatimaye mshambuliaji wa timu ya Rema 1000 FC Laurence Marco alizamisha nyavuni mpira uliokuwa ukiambaa pembeni mwa goli hilo.

Bao la nne la timu ya Rema 1000 FC liliwekwa kimiani na nahodha wa timu hiyo Shafii Said baada ya kutokea faulu upande wa kushoto na kupiga shuti kali lililomshinda mlinda mlango, kwa mara nyingine tena dakika mbili baada ya bao la nne kutinga kimiani, mshambuliaji Lawrence Marco alihitimisha karamu ya magoli kwa kufunga bao la kichwa baada ya kupokea krosi safi kutoka kwa kiungo mshambuliaji Masudi Juma.

Mara baada ya mchezo kumalizika Mkurugenzi wa timu Rema 1000 Samson Madawabora hakusita kuonyesha furaha yake katika viwanja hivyo kwa kuwazawadia kila mchezaji wa timu hiyo shilingi elfu 10,000 papo hapo uwanjani.

“Timu yetu ipo vizuri kocha wetu Jerad Ochieng ameshawapa maelezo ya kutosha wachezaji wetu hivi sasa ije timu yeyote tuu sisi sawa tutawafunga tuu kwani tupo vizuri,” alisema Madawabora.

Wakizungumza mara baada ya mchezo kumalizika kocha wa timu ya Lambo FC Paulo Modest alisema kwenye mchezo kuna matokeo matatu kushinda, kushindwa na kutoka sare hivyo anakubaliana na matokeo hayo huku kocha wa timu ya Rema 1000 FC Jerad Ochieng akisema wamejiandaa ipasavyo kwa mpambano ujao.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: