Mwandishi wa habari na mchambuzi wa mambo mbalimbali nchini Tanzania, Mathias Canal (Kushoto) akikabidhiwa tuzo ya cheti cha heshima kwa mchango wa utendaji katika jamii na Mohamed shabani ambaye ni Mkurugenzi wa idara ya jinsia, wazee na watoto wa Asasi ya Wazalendo na Maendeleo Tanzania (AWAMATA).

Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam

Mwandishi wa habari na mchambuzi wa mambo mbalimbali nchini Tanzania Ndg Mathias Canal amepewa tuzo ya cheti na Asasi ya Wazalendo na Maendeleo Tanzania (AWAMATA) ikiwa ni alama ya kutambua mchango wake na kazi za kizalendo na maendeleo anazozifanya nchini.

Akikabidhi tuzo hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti wa AWAMATA Taifa, Ndg Mohamed shabani ambaye ni Mkurugenzi wa idara ya jinsia, wazee na watoto wa asasi hiyo ya AMAWATA Taifa amesema Asasi hiyo imehamasika kutoa tuzo ya cheti cha heshima na pongezi kwa Mathias Canal kwa sababu ni mzalendo na amekuwa akifikiri juu ya maendeleo ya wananchi na kuhabarisha wananchi kuhusu mambo mbalimbali ya kimaendeleo na kihabari jambo ambalo limekuwa ni chachu kwa vijana wengine nchini.

Alisema kuwa Mathias Canal ni moja ya waandishi wabunifu sana na kama mwandishi kijana amekuwa na maono makubwa yenye manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla, ambapo amehamasisha vijana wengine kushirikiana nae katika mtandao wake wa Wazo Huru Blog na WazoHuru.Com chini ya kampuni yake ya habari inayotarajiwa kukamilisha usajili wake hivi karibuni.

“Tumekuwa tukimfatilia tangu akiwa Mhariri na mtangazaji wa redio Free Africa (RFA) na baadaye kuwa mwandishi wa kujitegemea ambapo amefanya kazi na viongozi mbalimbali wa dini, siasa, jamii na serikali kwa ujumla wake, kwa muda mrefu kama asasi tumeshawishika kumpa tuzo hii, kwa ufanyaji kazi ya kizalendo na maendeleo hasa anapoumiza kichwa kwa ajili ya kutengeneza ajira kwa vijana wenzake kupitia mtandao Wazo Huru Blog" Alikaririwa Mohamed

Akipokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Kampuni ya Wazo Huru Media Group (C.E.O), Ndg Mathias Canal amemshukuru Mwenyekiti wa AWAMATA Taifa Ndg Chief Mrindoko Babu Mwidadi sambamba na watendaji wote wa Asasi ya AWAMATA kwa kumpatia tuzo hiyo ya heshima kwani alidhani tuzo hiyo hutolewa kwa viongozi wa serikali pekee.

“Sikufikiria kama ningeweza kupata heshima hii katika umri wangu huu, kwani nimekuwa nikishuhudia viongozi mbalimbali wakipewa tuzo hii akiwemo Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo na hata Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kaka yangu Mhe Antony Mtaka, hivyo hii ni heshima kubwa sana kwangu, imenipa moyo wa kufanya kazi kwa bidii na weledi zaidi kwa manufaa ya Taifa langu” Alikaririwa Canal

Sambamba na hayo pia Canal alitoa wito kwa Vijana wenzake kutimiza wajibu wao, katika kusukuma gurudumu la Taifa mbele ikiwa ni pamoja na kujitokeza katika shughuli mbalimbali za kijamii sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli.

Asasi ya Wazalendo na Maendeleo Tanzania (AWAMATA) ni asasi isiyokuwa ya kiserikali inayojishughulisha na uelimishaji wa uzalendo kwa Watanzania na kufundisha mbinu za kujitegemea ili kuondokana na umaskini pia inatoa tuzo kwa watu wanaofanya vizuri katika masuala mbalimbali ya kizalendo na kuwasaidia wananchi kutoka katika lindi la umasikini.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: