My Rose, Rositha wangu Rose Mwaisango (pichani) jana tumekupumzisha salama nyumbani Ludewa. Umelala hautaamka wala kurudi tena hata siku ya mwisho kwa imani yetu ya Kikristo. Kwenye ibada yako ya mazishi baba yako mkubwa aliokupenda mnooo Father Ngailo alizungumza mambo nitaya-share na ambao hawakuwepo Ludewa mama Gidi. Father alisema haya;

WANAWAKE na WASICHANA: Ndoa ni jambo la heri ikiwa na heri na sio shari. Father ametukumbusha wanawake na wasichana kuwa tusivumilie matendo ya ukatili tunayofanyiwa na wanaume kwa sababu ya ndoa. Ametuasa sana kuvijua VIASHIRIA vya ukatili kwa sababu huwa hauji ghafla.

Amesisitiza wanawake tuondoke haraka sana ndoani tutakapoona hivyo viashiria maana hatukuzaliwa na hawa wanaume....tusisubirie kukutana na ulemavu wa kudumu au kifo. Hata wao kama walezi wa imani wako tayari kusikiliza mashauri haya na kuvunja ndoa za aina hii.

WANAUME na WAVULANA: Father amesema tuwajulishe kuwa mkituchoka na mkiwachoka wake zenu waacheni kwa amani na sio kuanza kuwafanyia ukatili. Mruhusu mwanamke aondoke kwako au ondoka wewe na ukaanze maisha hayo mengine kuliko kusababisha ulemavu au kifo. Ulipokabidhiwa mwanamke au binti huyo, wazazi wake walikuamini kuwa utalinda uhai wa mtoto wao. Mrudishe akiwa mzima na sio akiwa maiti au mwenye ulemavu mkubwa.

WAZAZI na WALEZI: ifike mahali mtoto wa kike anaporudi nyumbani kuwaeleza kuwa maisha yake yapo hatarini basi aeleweke hivyo. Mzazi uwe tayari kupigania uhai wa mtoto wako wa kike wakati wowote. Imekuwa desturi mzazi kumrudisha mtoto na kumwambia kavumilie ndoani maana ndoa ndivyo zilivyo. Akirudi kwa kupigwa kofi moja tu hiyo ni sababu tosha ya kukujulisha kuwa maisha ya mtoto wako yako hatarini...sababu tosha kuwa anaeishi na mtoto wako ni katili. MTOTO KWA MZAZI HAKUI.

VIONGOZI WA DINI: umefika wakati ambao viongozi wa dini wanapaswa kubadili mtazamo wao juu ya ndoa. Ndoa yenye ukatili na manyanyaso sio ndoa tena inayopaswa kuendelea kukingiwa kifua. Ifike mahali binti anapokuja kwa viongozi wa dini kuwa yupo tayari kuondoka kwa mumewe kwa sababu ananyanyasika na anafanyiwa ukatili basi asikilizwe. Mwanaume KATILI habadilishwi kwa MAOMBI akiwa anaendelea kukaa na mkewe ndani

Pumzika ROSE 🌹🌹🌹🌹 @ Ludewa, Njombe.

Ni Mimi Adella Abell.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: