Mmoja ya wakazi wa kijiji cha Madimba akipata huduma ya upimaji wa kisukari katika zoezi la upimaji wa afya bure liliondeshwa kwa udhamini wa TPDC

Na Mwandishi Wetu.

Afya bora na imara ni msingi wa maendeleo ya Taifa lolote duniani, kwa kuzingatia hilo TPDC imeendesha zoezi la upimaji afya bure kwa wakazi wa maeneo ya Vijiji vya Ziwani, Madimba na Msimbati vilivyopo Wilaya ya Mtwara Vijijini Mkoani Mtwara. Zoezi hili lililenga kupima magonjwa yasiyoambukizwa ikiwemo kisukari na shinikizo la damu bila kusahau upimaji wa virusi vya Ukimwi (VVU) kwa hiari na kutoa ushauri juu ya saratani. 

Uendeshaji wa zoezi hili ulienda sambamba na bonanza la mpira wa miguu kwa timu za vijana kutoka katika vijiji hivi vitatu yote yakiwa yameratibiwa na TPDC ikiwa na katika mikakati ya Shirika kujenga mahusiano bora na ujirani mwema na wakazi waishio karibu na miundombinu ya gesi asilia. 

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Meneja Mawasiliano wa TPDC, Bi. Marie Msellemu alisema “zoezi hili la kupima afya ni endelevu ambapo tulianzia katika Visiwa vya Songo Songo na leo hii tupo katika vijiji hivi vya Ziwani, Madimba na Msimbati na baadae tunatarajia kufanya vivyo hivyo Wilayani Kilwa na katika maeneo yote ambapo miundombinu ya gesi asilia inapita”. Bi. Msellemu alieleza kuwa TPDC inatambua changamoto zilizopo katika sekta ya afya na inachojaribu kufanya ni kusaidia kutoa huduma za upimaji kwa wakazi wa maeneo hayo kwa magonjwa yasiyoambukiza, VVU na ushauri juu ya saratani. “Tunatambua kwamba afya ni mtaji na hivyo ni lazima ilindwe na kutunzwa ili iendelee kutusaidia” alisema Msellemu. 
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mngoji na Madimba wakiwa kwenye eneo la kusubiria kabla ya kumuona daktari kwa ajili ya upimaji

Wakazi 418 kutoka vijiji hivi walifanikiwa kupata huduma hizi ambapo kati yao 284 walikuwa wanaume na 134 wanawake. Akitoa maoni yake mmoja ya wananchi kutoka kijiji cha Msimbati, Bi. Zainab Abdallah alisema “zoezi hili ni muhimu na limetusaidia kujitambua afya zetu, tunatoa rai kwa TPDC kufanya zoezi hili kuwa endelevu na kuongeza vipimo kama vile vya macho, moyo na masikio”.

Kwa upande wa michezo, timu ya Luvula Star kutoka kijiji cha Msimbati walifanikiwa kuibuka washindi wa kwanza ambapo walicheza fainali na timu ya Stone Village kutoka Mayaya. Akizungumza baada ya fainali, nahodha wa timu ya Luvula Star Juma Mohamed aliishukuru TPDC kwa kuandaa mashindano hayo na kusema michezo hiyo inawasaidia wao kama vijana kujiepusha na shughuli zisizokuwa na faida kwao na badala yake kuweka nguvu zao katika michezo ambayo inaboresha afya na kuibua vipaji.

Nae Mratibu wa Michezo Kata, Ndg. Dadi Mohamed Lipayaya alitoa wito kwa timu zaidi kushiriki katika mashindano haya mwakani na kuiomba TPDC kuyafanya mashindano haya kuwa endelevu kwani yanatoa fursa kwa vijana kuonyesha vipaji vyao na kukuza michezo nchini.
Meneja Mawasiliano wa TPDC, Bi. Marie Msellemu akigawa jozi ya jezi na mipira kwa Juma Mohamed, nahodha wa Luvula Star baada ya kuibuka mshindi wa kwanza wa fainali za TPDC bonanza.
Timu mbili za Madimba na Myoyo zikiwa katika pozi la pamoja baada ya kumaliza mechi ya fainali baina yao katika mashindano ya TPDC Bonanza.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: