Bi Marie Msellemu, Meneja Mawasiliano TPDC (Kushoto) akikabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 21,151,500/ kwa mkuu wa Wilaya ya Mtwara Ndg. Evodi Mmanda (wa pili kutoka kulia) kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika kijiji cha Mngoji.
---
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kupitia mfuko wake wa uwajibikaji kwa jamii (CSR) limeendelea kusaidia maeneo ya kipaumbele katika ustawi wa jamii ikiwemo afya, elimu na utawala bora. Safari hii mchango wa TPDC umewafikia wana Mngoji ambapo ujenzi wa zahanati ulishaanza na kwa kuzingatia mahusiano na ukaribu wa kijiji hiki na miundombinu ya uchakataji na usafirishaji wa gesi asilia ilionekana ni vyema na sahihi kwa Shirika kutoa mchango wake katika kuinua sekta ya afya Mngoji.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Bi Marie Msellemu ambae ni Meneja Mawasiliano wa TPDC alisema “Sisi kama TPDC tumekuwa na utaratibu wa kuchangia sekta za afya, elimu na utawala bora hususan katika maeneo ambapo tunafanya shughuli za utafiti na uendelezaji wa gesi asilia na mafuta, lengo likiwa ni kujenga mahusiano mema na bora na kuwezesha wananchi wa maeneo hayo kushiriki kikamilifu katika shughuli za kukuza uchumi wa Taifa”. Bi Msellemu aliongeza kwamba pamoja na michango hiyo kupitia mfuko wa uwajibikaji kwa jamii, TPDC pia imekuwa ikihakikisha wazawa wanapewa kipaumbele katika ajira ikiwa ni moja ya majukumu iliyopewa na Sheria ya Petroli 2015 (PA, 2015) ambapo Shirika la Mafuta la Taifa linawajibu wa kukuza ushirikishwaji wa wazawa (Local content).

Akipokea mfano wa hundi ya shilingi milioni ishirini na moja laki moja hamsini na moja elfu na mia tano (21,151,500) ukiwa ndio mchango wa TPDC katika ujenzi wa Zahanati ya Mngoji, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Ndg. Evodi Mmanda aliishukuru TPDC kwa kuendelea kuonyesha ushirikiano wa hali ya juu kwa jamii. Akizungumza wakati wa shughuli za kukabidhi mchango huo kwa Serikali

Alisisitiza matumizi sahihi ya fedha hizo ili kufikia lengo lililowekwa la kuwa na zahanati kijijini hapo jambo ambalo litapunguza usumbufu kwa wananchi wa eneo hilo kusafiri umbali mrefu kufikia huduma za afya. Ndg. Mmanda aliwaasa watendaji wa Kijiji kusimamia vema matumizi ya fedha hizo na kuweka ahadi ya kufuatilia matumizi ya fedha hizo na ujenzi wa zahanati akitolea mfano maeneo ambayo watendaji wamekuwa wakibadili matumizi ya fedha za msaada bila kushirikisha Serikali ya Mkoa wala mdau wa maendeleo alietoa mchango kwa lengo mahususi.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evodi Mmanda akisisitiza jambo wakati wa shughuli za kupokea mfano wa hundi ya shilingi milioni 21,151,500/ kutoka TPDC kusaidia ujenzi wa zahanati Mngoji.

Akizungumzia namna ambavyo mchango huu utawasaidia wana Mngoji, mmoja ya wakazi wa Kijiji cha Mngoji Bi. Zebaki Issa alisema “tunapata shida sana kupata huduma ya afya, tunatoka hapa tunaenda Msimbati, tunatoka hapa tunaenda Madimba ambapo kote kuna umbali kutoka hapa Mngoji, hivyo ujenzi wa zahanati hii ni ukombozi kwa wana Mngoji”. Kijiji cha Mngoji kina wakazi wapatao 2800 na zahanati hii itahudumia sio tu Wananchi wa Mngoji bali pia wananchi wa kitongoji cha Uyui kinachopakana na kijiji hicho.
Sehemu ya jengo la zahanati ya Mngoji ambayo ujenzi wake unaendelea
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: