Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Korea (KOICA) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) leo yameandaa halfa kusherehekea kukamilika na pia kukabidhi programu ya Jumuiya za Kukomesha Njaa Kabisa za Saemaul kwa Serikali ya Tanzania katika mkoa wa Dodoma.

Kupitia programu hiyo, washiriki kutoka vijiji vitatu walipata fursa ya kuimarisha njia zao za kujipatia riziki kupitia vikundi vya ufugaji wakati ambapo zaidi ya miradi 100 ya jamii ilijengwa au kukarabatiwa. Miradi hiyo ilikuwa ni pamoja na maghala, mifumo ya umwagiliaji maji kutumia nishati ya jua, malamba na vituo vya jamii. Miradi hii ilisaidia kuimarisha uwezo wa jamii kuhimili majanga kama vile ukame na mafuriko na kutoa fursa za kiuchumi kwa washiriki katika kipindi cha mwaka mzima.

“Nina furaha leo kupata fursa ya kujionea programu ya Saemaul na zana inazowapatia wenyeji ili kuwawezesha kujitegemea na kujenga maisha bora ya baadae ya familia zao,” alisema Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles John Tizeba. “Hivi sasa mradi unamilikiwa na wakaazi wa vijiji vya Chiboli, Fufu na Suli. Sasa hawa wana wajibu wa kuhakikisha kwamba wanaupenda, wanauthamini na kuutunza ili kuufanya endelevu. Nitapenda kuona miradi hii inaleta mabadiliko chanya katika maisha ya wote wanaoshiriki katika siku zijazo, na ni vyema pia mafanikio yatakayopatikana kwenye mradi huu kuyapeleka na kuyatekeleza mahali pengine katika vijijiji vingine wilayani chamwino.”
Mradi huo uliofadhiliwa na Jamhuri ya Korea na kutekelezwa na WFP na Good Neighbours Tanzania, ulisaidia kaya 2,500 kutoka vijiji vya Chiboli, Fufu na Suli katika Wilaya ya Chamwino.

“Kwa niaba ya Jamhuri ya Korea, KOICA inayo furaha kuona matunda ya modeli ya Saemaul na jinsi inavyowanufaisha watu katika Wilaya ya Chamwino,” alisema Naibu Mwakilishi wa Nchi wa KOICA, Bi. Hyunsun Kim. “Juhudi za jamii ni muhimu ili kufanya maendeleo yawe endelevu. Korea inao uzoefu wa kutumia modeli hii, ambapo ilifanya kazi vizuri na leo sisi ni miongoni mwa mataifa yaliyoendelea sana duniani.”
Programu hiyo ya Saemaul iliyogharimu Dola za Maekani milioni 5 imejengwa kwa kulinganisha na programu kama hiyo iliyotekelezwa katika Jamhuri ya Korea miaka ya 1970, na ambayo ilitoa mchango mkubwa katika kupunguza umaskini vijijini kwa kutumia miradi ya maendeleo iliyobuniwa na kila jamii kwa kuzingatia mahitaji yao. Saemaul ina maana ya “kijiji kipya” katika lugha ya Korea.

Hafla hiyo ilifanyika katika Kijiji cha Suli, Wilaya ya Chamwino, na kuhudhuriwa na Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles John Tizeba, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa, Aziza Mumba, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga, Mkurugenzi wa Nchi wa WFP Tanzania Michael Dunford, Naibu Mwakilishi wa Nchi wa KOICA, Hyunsun Kim, Mkurugenzi wa Nchi wa shirika lisilo la kiserikali la Good Neighbours Tanzania, Namun Heo na wawakilishi kutoka tawala za mikoa.
Kwa kutumia uzoefu wa miaka 30 katika programu za miradi ya umma nchini Tanzania na kwingineko, WFP ilisaidia uwekaji mipango, msaada wa kiufundi, usimamizi wa mradi na ujenzi wa miundombinu ya jamii.

“Kumekuwa na mabadiliko makubwa ya maendeleo katika vijiji hivyo vitatu ndani ya miaka michache iliyopita,” alisema Mwakilishi Mkazi wa WFP Tanzania Michael Dunford. “Nilielezwa na wanajamii, kwamba siku zilizopita, wanaume na wanawake walihama kutoka eneo hili ili kutafuta kazi mahali pangine—hasa nyakati za kiangazi au wakati wa ukame lakini sasa kwa sababu ya miradi hii, kuna kazi nyingi zinazoingiza kipato katika vipindi vyote vya mwaka mzima.

Shughuli nyingine kupitia programu ya Saemaul ni pamoja na kulima na kuchakata ufuta na pia kujenga visima virefu, majengo ya madarasa shuleni na majosho ya ng’ombe.

“Tunatoa shukrani zetu kwa nyakati zote tulizokuwa pamoja katika jamii hizo,” alisema Mkurugenzi wa Nchi wa Good Neighbours Tanzania, Namun Heo. “Mafanikio madogo na makubwa, changamoto na mafunzo yatokanayo yalitufunza thamani ya kushirikiana katika kazi. Nina matumaini watayaendeleza na kisha kushirikisha mafunzo chanya na vijiji vingine kama majirani wema.”
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: