Na Said Said Nguya.

01. Elimu Bure kuanzia Darasa la kwanza mpaka kidato cha Nne ambapo kila mwezi Serikali inapeleka fedha mashuleni shilingi bilioni 23 kwa ajili ya uendeshaji, hii ni sawa na shilingi Bilioni 276 kwa mwaka hivyo kufanya Serikali mpaka sasa toka mwaka 2016 kutumia Kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 680. Hii imesaidia kuondoa ubaguzi katika sekta ya Elimu yaani Masikini na matajiri wote wamepata fursa sawa ya Elimu.

02. Uimarishaji wa Shirika la Ndege (ATC). Mpaka sasa Ndege tatu mpya zimewasili na nne kubwa zipo katika hatua za mwisho kuwasili. Hii itarahisisha na kuimarisha sekta ya Utalii nchini na kuongeza pato la taifa.

03. Kuanza kwa ujenzi wa Reli ya kisasa kiwango cha kimataifa (Standard gauge Railway) inayopitia Mikoa ya Morogoro, Dodoma, Tabora kuelekea Kigoma na Mwanza ambapo kwa sasa ujenzi umekaribia Morogoro. Hii itarahisisha usafirishaji wa watu na mizigo kutoka bandari ya Dar es salaam na kukuza biashara baina ya Tanzania na nchi sita za Kongo, zambia, Burundi, Rwanda, Uganda na Malawi, zinazotegemea bandari ya Dar es salaam hivyo kuongeza pato la taifa. Zaidi kuepuka matengenezo ya mara kwa mara ya barabara zinazoharibiwa kutokana na mizigo mizito kusafirishwa kwa njia ya Malori, na pia itarahisisha usafiri kwa maana inauwezo wa kusafiri umbali wa KM 160 kwa saa, yaani Mwanza - Dar na Dar - Kigoma ni masaa sita tu tofauti na sasa ni zaidi ya masaa 12.

04. Kukamilisha ujenzi wa miradi mikubwa ya ufuaji umeme ikiwemo Kinyerezi II & III, na kuanza ujenzi wa Mradi Mkubwa zaidi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Stiegler's Gorge wenye uwezo wa kuzalisha MW 2100 utakaopelekea kuwa na umeme wa gharama nafuu na wauhakika na kuchochea mapinduzi ya Viwanda na kupunguza gharama za uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kutoķa viwandani na kuleta unafuu zaidi wa maisha kwa wananchi.

05. Kuanza kwa ujenzi wa barabara za juu ( Flyover Ubungo & Tazara) na Mwendokasi katika Jiji la Dar Es Salaam. Hii itapelekea kupungua kwa msongamano unaopelekea watu kupoteza muda mwingi wa kupata huduma, kufanya kazi na uzalishaji Viwandani hivyo kupunguza muda wa kufanya kazi za maendeleo. Barabara ya mwendo kasi kutoka Kariakoo kwenda Mbagala ujenzi utaanza hivi karibuni. Hii itafanya kuwepo na barabara za mwendokasi karibia maeneo yote ya kutokea mjini yaani Mbezi ya Kimara, Morocco, Bunju, Mbagala na Chanika.

06. Kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika Vita dhidi ya Rushwa na Ufisadi. Hii imepelekea mapato serikalini kuongezeka, nidhamu ya matumizi ya fedha, uwajibikaji kuongezeka. Watumishi mbali mbali waliojihisisha na suala la Rushwa na wakwepa kodi wamedhibitiwa na wengine kesi zipo mahakamani. Hii imesaidia kuongeza makusanyo ya ndani ya serikali kutoka wastani wa Bilioni 800 mpaka 1.2 tirioni kwa mwezi hivyo kuweza kumudu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi ikiwemo Elimu bure.

07. Mapambano dhidi ya uporaji wa rasilimali za nchi hususani Madini. Hii imepelekea kupitiwa upya kwa mikataba ya madini na kutungwa kwa sheria mpya za usimamizi wa madini pamoja na kuhuishwa upya kwa mfumo mzima wa uvunaji na biashara nzima ya madini (kupata 50/50) ili kuleta tija kwa Taifa. Zaidi ni ujenzi wa ukuta mkubwa katika machimbo ya Mererani ili kudhibiti utoroshwaji wa madini. Hii imepelekea kuongezeka kwa mapato yatokanayo na madini yakiwemo Tanzanite.

8. Kuongezeka kwa mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kutoka bilioni 346 mpaka kufikia bilioni 483 sawa na ongezeko la bilioni 140 katika kipindi cha miaka miwili. Zaidi kuongezeka kwa wanufaika kutoka 98, 300 mwaka 2015 mpaka kufikia wanufaika 125, 000 mwaka 2017. Hii imepelekea katika awamu ya Tano vijana wengi kutoka katika familia za chini kupata nafasi ya kusoma elimu ya juu na kupelekea usawa katika upatikanaji wa Elimu ikikumbukwa pia uwepo wa Elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne.

09. Kutekeleza ahadi ya serikali kuhamia Dodoma ikiwa ni uamuzi uliofanywa tangu mwaka 1973, ambapo awamu zote tangu enzi za Mwl Nyerere uamuzi huo ulishindwa kutekelezwa sasa ndani ya miaka miwili ya Ndg John Joseph Pombe Magufuli Serikali kwa kiasi kikubwa imehamia Dodoma na Rais mpaka kufika 2020 atakuwa Dodoma. Hii kwa kiasi kikubwa inaenda kuchochea zaidi fursa za kibiashara katika mikoa ya kanda ya kati na uboreshwaji zaidi wa miuondombinu katika mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Iringa , Morogoro na Manyara sambamba na kupandishwa hadhi kwa mji wa Dodama na kuwa Jiji.

10. Kuendelea kuimarika kwa usalama wa raia na mali zao. Zaidi ni kuimarika kwa ulinzi wa mipaka yetu na ulinzi wa Rasili mali zetu. Na kila kilipotokea viashiria vyovyote vya uvunjaji wa amani kwa raia Serikali imekuwa ikisimama imara kuvidhibiti.

Mungu ibariki Tanzania.
Mungu mbariki Rais wetu Magufuli.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: