“Baba Karanga za Diamond! Baba nataka Karanga za Diamond!” Huu ni ule wakati ambao unasimama kwenye foleni na unatamani hata kuwasha gari na kusukuma magari yaliyo mbele yako. Ilikua ni jioni nimetoka kuwachukua wanangu shule na mtoto wangu mdogo wa mwisho alianza kupika kelele za kutaka karanga. Pembeni yangu kulikua na kijana, au niseme mtoto kashikilia Karanga za Diamond kazizungusha shingoni anauza.

Alikua akipita kila gari kuuza, kwa kawaida sipendi kushusha vioo kwenye gari lakini kutokana na kelele nilijua na ile foleni angeanza kulia, nilimdekeza sana hivyo sikutaka alie kwa kitu cha Shilingi elfu moja. Nilishusha Kioo cha gari na kumuita yule kijana. “Karanga bei gani?” Nilimuuliza, “Moja mia tatu, tatu buku, aliongea huku akinionyeshe kama anataka nikate. “Naomba za elfu tatu.” Niliongea huku nikimkabidhi noti ya Shilingi elfu kumi.

“Shikamoo Baba Mdogo…” Ilikua ni salamu yake wakati anaipokea ile pesa, nilistuka kidogo na kunyanyua uso wangu kumuangalia. Sikua namfahamu hivyo nilidhani ni salamu tu za vijana kwakua nilinunua Karanga nyingi. “Umenisahau? Mimi Peter, Peter Jackson…” Sasa aliongea akionyesha kuwa ananifahamu kabisa, alitaja jina la Marehemu Kaka yangu. nilijikuta nakodoa macho kumuangalia vizuri.

Nilistuka kwani mbele yangu ni kama alikua amesimama Jackson, sura yake kipindi tunaenda kuteka maji kule Kijijini Iringa ilinijia. Hapo ndipo nilikumbuka, yule alikua ni mtoto wa Marahemu Kaka yangu, ndiyo najua mnashangaa, mimi niko kwenye Gari nauziwa Karanga na mtoto wa Marehemu Kaka yangu, mnadhani labda ni Kaka wa jirani. Hapana, ni Kaka yangu, tena si tumbo moja tu, hapana yeye ndiyo aliniachia ziwa.

Najua mnashangaa mnajiuliza labda alitutenga tangu zamani. Hapana yeye ndiyo alinisomesha mpaka kumaliza chuo kikuu. Wakati huo yeye akifanya kazi nzuri tu kama Mkatoika kampuni moja, baada ya kuishi maisha ya shida kipindi cha utotoni na yeye kusoma kwa bidii na kufanikiwa kutoka kimaisha hakutusahau ndugu zake. Mpaka anafariki miaka mitatu iliyopita alihakikisha kuwa wote tunasoma na sikusoma tu bali alitutaftia kazi nzuri.

“Wewe unafanya nini huko Barabarani wewe si ulikua shule?” Niliuliza kwa aibu, nilitaka kumfokea lakini nilikumbuka tangu mazishi ya Kaka yangu na kugaiwa kwa mirathi sikugeuka nyuma. Sio mimi tu hata ndugu zangu wengine, kila mmoja alikua na familia yake hivyo kila mtu alikua bize na maisha yake. Baada ya wazazi wetu wote kufariki Kaka yetu yule ndiyo alikua akituunganisha hivyo yeye alipotangulia kila mmoja lishika hamsini zake.

“Niliacha Baba, sasa hivi niko nafanya biashara…” Aliongea kwa uchangamfu kabisa. Nakumbuka wakati Baba yake akifariki alikua akisoma kidato cha kwanza Nairobi na moja ya sehemu za Mirathi ilikua ni kwaajili ya kutunza watoto ikiwa ni pamoja na kuwasomesha. “Nishikie nikuombee chenji hapo kwa menzangu…” Aliongea huku akimuita kijana mwingine aliyekua pembeni yake na kumuomba chenji, mimi bado nilikua nimeduwaa.

Bado nilikua nawaza ni nini kilikua kimetokea mimi niko kwenye gari nina maisha mazuri wakati mtoto wa Kaka yangu anauza karanga, mchafu mchafu kachakaa na anaonekana kuchoka. Lakini hakua na makuu, wala hakutaka kuniomba chochote, alinipa chenchi yangu. “Msalimie Mama mdogo Baba, sisi ni wazima… Mama anakusalimia…”

Aliongea na kuondoka, huwezi amini nilimuangalia mpaka anapotelea bila kuweza kunyanyua mdomo kumuita. Machozi yalikua yananitoka bila kujua. “Nimefanya nini?” Nilijiuliza bila majibu. Nilikuja kustuliwa na honi za magari mengine wakiniambia kuwa niondoke kwani nawachelewesha. “Baba unaumwa? Mbona unalia?” Mwanangu mkubwa aliniuliza lakini sikua na jibu.

Nilifika nyumbani na kumuuliza mke wangu kama anawasiliana na mke mwenzake, mke wa marehemu kaka yangu. Hakua akiwasiliana naye, alikua hata hajui anaishi wapi? Nilishindwa kukaa ndani, niliamua kwenda kumtafuta, nilifika kwenye nyumba yao, kufika ndipo nilikumbuka kuwa ile nyumba ilikua ni ya shirika ambayo Kaka yangu alipewa hivyo baada ya kufariki waliondolewa na alikua anaishi mtu mwingine.

Nikakumbuka kuna sehemu Kaka alikua anajenga, nilienda nyumba ilikua haijakamilika, alikua anajenga nyumba kubwa ya ghorofa. Nilifika na kukutana na watoto wengine wa Kaka, walikua wakicheza nnje ya lile ghorofa kubwa ambalo lilikua kama Gofu. Wao walikua wadogo hata hawakunitambua, lakini mimi niliwakumbuka. Walinisalimia niliwaulizia Mama yao wakaniambia ametoka, sikua na haraka nilitaka kumsubiri kwani hata hakua na namba za simu.

Nilikaa pale mpaka kwenye saa moja hivi za usiku. Peter ndiyo alikuja na kuniona, alishangaa kuniona pale na kunisalimia, alinikaribisha ndani. Alionekana kuchoka sana lakini alijitahidi kutabasamu, alishakua kijana anaelewa. Nilimuulizia alipo Mama yake na kama atachelewa. “Nyie si mngempeleka kumuona Mama! Mnamchelewesha Baba mdogo au hamjui ana kazi zake huko za kufanya!” Aliwafokea kidogo, nilimuambia haina shida ndipo akaniambia alipo Mama yake.

Hakukua mbali sana, tuliingia kwenye Gari na kuanza safari, ndani alinichangamkia, aliniulizia kuhusu wanangu, kuhusu Shangazi zake, kuhusu Baba zake wadogo wengine na watu wengi wa familia. Alikua akimjua kila mtu lakini kwa bahati mbaya sisi ni kama tulikua tumewasahau. Mimi na ndugu zangu tulikua tukikutana mara kwa mara lakini hata mara moja tulikua hatujawahi kuwazungumzia lakini yeye ambaye hata alikua hatujui vizuri anaulizia tunaendeleaje.

Nilifika alipokua shemeji yangu, nilimuona kakaa Barabarani, karai la ndizi na kibatari kiko mbele yake. “Mama kuna mgeni wako…” Alimuita Mama yake ambaye alishtuka kuniona. Nilimuona yule shemeji yetu ambaye alikua anatupikia mara kwa mara tukienda kumsalimia. Aalikua kachoka, kakonda imebaki sura tu, alijitahidi kutasabasamu, alichangamka, alijitahidi kuonyesha kama hana shida yoyote lakini shida zilijionyesha.

Tulisalimiana, aliona aibu hata kunishika mkono akihisi atanichafua. Nilimuomba turudi nyumbani naye hakubisha, nilifika mpaka kwake ndipo nikagundua kuwa walikua wakiishi katika gofu, hata milango lilikua halina zaidi ya shuka lililotundikwa kama mlango. Kweli niliumia, aliniletea kiti nikakaa, kila nikifumbua macho nilimuona Marehemu Kaka yangu kasimama ananisuta.

Nilihisi kama ananiambia “Kweli nyie ndiyo wa kuwafanyia hivi wanangu, nyie niliowaamini nikawasomesha! Hivi kweli mke wangu ambaye nilimkataza kufanya kazi awe Mama wa nyumbani nyie nikawatafutia kazi ndiyo analea wanangu nyie na kazi nzuri hata kuwasomesha hamuwezi?” Nilishindwa kuvumilia nilimuuliza shemeji yangu nini kimetokea akaniambia, maisha.

Baada ya kupata mirathi alitegemea kuendelea kuwasomesha watoto, alitumia tumia akijua ni pesa nyingi lakini matumizi yalikua makubwa, anashtuka zishakatika nusu hapo ndipo akaamua afungue biashara, kwakua hakua na uzoefu alitapeliwa mara mbili na kupoteza kila kitu. Nilisikitika na kumuambia kwanini hakuja kuomba msaada alinikumbusha alishanipigia simu mara ziadi ya kumi zote namuambia nitamtafuta nitamtafuta.

Nilikumbuka mara ya mwisho alikuja ofisini kuniambia kuhusu ada ya watoto nikampa elfu kumi. Sikua na chakuongea zaidi nilijua sisi ndiyo tumemuangusha, Kaka yangu hakumuandaa kubeba majukumu kama yale. Alimfanya Mama wa nyumbani, alimkataza hata kutoka ndani, kila kitu alikua ananunuliwa, Kaka alikua na wivu na mara nyingi akitoka alikua anapigwa na kweli tulikua tunamuona Kaka yuko sawa na shemeji anakosea.

Hata katika mali hakua akimshirikisha zaidi ya sisi ndugu zake, hata ndugu wa shemeji alikua hawasaidii na kila mara alisema hana pesa. Niliona aibu kuendelea kuuliza, nilimuambia anyanyuke tunaondoka pale na kuanzia siku ile nitamsaidia kulea familia kwani ni jukumu letu wale ni wenetu. Sikutaka waendelee kulala pale niliwachukua na kuondoka nao. Sasa hivi watoto wamerudi shule na shemeji nimemfungulia biashara.

Nyumba nimepata watu wa kuimalizia wanataka kufungua ofisi hivyo naamini mpaka mwezi wa nane mwaka huu wataanza kuchukua kodi kidogo kidogo. Nimeandika kisa changu ili kumuomba msamaha Kaka yangu kwa kushindwa kulea familia yake na kuwaambia wanaume wenzangu kuwa hata kama una mali kiasi gani hakikisha unamuandaa mkeo kuhudumia wanao kwani ndugu wana familia zao na ukiondoka watakusahau, nawaambia kwasababu sisi tulisahau pamoja na kusaidiwa sana.

**MWISHO**

Najua watu wengi hatuwazi kuhusu kifo lakini kipo. Je, mwanaume umemuandaa mke wako kubeba majukumu ya kuhudumia wanao au unategemea ndugu na wewe mwanamke Je, umejiandaa kubeba majukumu au unasubiri yakufike kwanza?
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: