Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza wakati  akizindua bodi ya wakurugezi wa shirika la reli Tanzania (TRC) iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu.

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limepewa muda wa siku 90 ambazo ni sawa na miezi mitatu kuhakikisha maeneo yote ambayo reli inakatiza barabara kuwe na vizuizi badala ya kutegemea alama peke yake.

Uamuzi huo unakuja ikiwa ni siku chache zimepita tangu kutokea kwa ajali ya basi kugonga treni mkoani Kigoma na kusababisha watu 12 kufariki dunia na wengine 26 kujeruhiwa.

Maagizo hayo yametolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati anazindua bodi mpya ya wakurugenzi ya TRC.

Hivyo wakati anazungumza na wajumbe hao na watumishi wa TRC amesema ipo haja ya kuweka vizuizi kwenye maeneo ambayo reli inakatiza barabara.

Amesema katika suala la usalama wa raia wa nchi hii gharama isiwe kigezo cha kutowekwa vizuizi hivyo huku akitoa maagizo ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa vizuizi viwe vimewekwa.

"Hakikisheni kunakuwa na vizuizi kwenye maeneo ambayo reli inakatiza barabara, ile ajali ya Kigoma kama kungekuwa na kizuizi huenda isingetokea.

"Kuwa na alama peke yake haitoshi kwani wapo wengine macho yao hayaoni mbali, hivyo kukiwa na kizuizi hakuna anayeweza kupita,"amefafanua Waziri Mbarawa.

Amesema vizuizi hivyo vinaweza kuwa vya nguzo ambapo kutakuwa na mtu maalum atatakiwa kukaa na hata akilipwa Sh.300,000 kwa mwezi si mbaya na wala si gharama mbele ya uhai wa mtanzania, hivyo vizuizi hivyo vianze kuwekwa mara moja.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: