Na Emmanuel J. Shilatu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amezidi kuwashangaza Watu. Si Vijana, si Wazee, si Wanawake, si Wanaume, si wana CCM, si wapinzani wote wamebaki kushangazwa na uteuzi alioufanya Rais Magufuli wa Wakuu wa Mikoa na wilaya, Makatibu wakuu na Manaibu, Makatibu Mukhtasi wa Mikoa (Ras).

Kushangazwa huku kwa Watu kunatokana na namna Rais Magufuli alivyokuja na uteuzi wa kipekee. Rais Magufuli amezidi kujidhihirisha yeye ni kipenzi na anawaamini sana Vijana kwa kuwapa dhamana ya uteuzi kwenye nafasi mbalimbali tofauti kabisa na hali ilivyokuwa hapo awali ambapo Vijana walikuwa kundi la mwisho kuaminiwa.

Leo hii wale waliokuwa wanasema Serikali na chama kumejaa Wazee hawapo tena kwa maana kila kona akijaribu kumulika anakutana na Vijana walioteuliwa na wakipewa dhamana. Na yeye mwenyewe Rais Magufuli aliwahi kukiri popote pale alipowateua Vijana hawajawahi kumwangusha.

Rais Magufuli amezidi kuwashangaza Watu kutokana na kitendo chake cha kuwateua wapinzani kwenye Serikali yake. Wengi wanaongea sana kuwa Rais Magufuli anawateua wapinzani na kuwaacha makada waliokipigania chama muda mrefu. Watu hawa wanashindwa kuelewa idadi ya waliokuwa wapinzani walioteuliwa ni ndogo zaidi ukilinganisha na idadi kubwa ya walioteuliwa. Hoja ya wapinzani kuteuliwa zaidi si kweli na haina mashiko.

Pia wanaojiita makada ni lazima waelewe ndani ya CCM hakuna aliye mkongwe wala mchanga. Ilimradi upo ndani ya CCM basi kila Mtu anayo haki sawa ya kuchagua na kuchaguliwa, anayo haki sawa ya kuteuliwa na kutenguliwa.

Hata wapinzani pia wanatakiwa waelewe haki waliyokuwa nayo Wana CCM waliojiunga upinzani na kupata nafasi nyeti ndani ya upinzani ndio haki ile ile waliyonayo wapinzani waliojiunga CCM.

Ukweli utabaki pale pale kitendo cha Rais Magufuli kuteua wapinzani amejipambanua kuwa Serikali haina ubaguzi wa aina yeyote ile bali kinachoangaliwa ni uwezo wa Mtu kuchapa kazi.

Ni muhimu sana kwetu kuhubiri umoja, upendo, amani na mshikamano itatusaidia kama Taifa, kuliko kujenga makundi, mifarakano na chuki miongoni mwetu. Heko kwa Rais Magufuli kwa kujenga umoja wa kitaifa.

Pia Rais Magufuli amezidi kuwashangaza Wananwake kwa kitendo cha kuwateua Wanawake tena wenye umri mdogo zaidi kushika nafasi nyeti Serikali. Gift Msuya, Sophia Kizigo na Jokate Mwegelo ambao wameteuliwa kuwa Wakuu wa wilaya ni nembo ya uthibitisho wa upendo wa dhati alionao Rais Magufuli kwa Wanawake nchini. La maana si kuangalia historia ya maisha yao bali tutazame juu ya namna watakavyo timiza wajibu wa majukumu yao. Muhimu tuwape ushirikiano wa kutosha pindi utakapohitaji wanapotimiza majukumu yao.

Ndugu zangu, nahitimisha kwa *kumpongeza Rais Magufuli kwa uteuzi alioufanya*. Muhimu kujua mamlaka ya uteuzi wametimiza majukumu yao vyema kwa kuwateua Watu makini kabisa pasipo chembe ya ubaguzi. Rai yangu kwa Wateuliwa walinde imani na dhamana waliyopewa na Rais Magufuli kwa kuwajibika ipasavyo kwa kuwatatulia Wananchi shida zao na kutekeleza vyema ilani ya uchaguzi 2015 – 2020.

*Shilatu E.J*

0767488622
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: